UCHUNGUZI
unaonesha kuwa, watu wengi waliopata kuulizwa swali lililopo kwenye kichwa cha
makala haya walipendelea zaidi kupendwa.
Ni nadra
sana mtu kujinung’unikia juu ya udhaifu
wa kutopenda, kuliko lawama za kuwalaumu wengine kuwa hawampendi.
Je hivi
ndivyo mambo yanavyotakiwa kuwa? Jibu ni hapana; kwani sayansi ya ufahamu na
nafsi haielekezi hivyo kwa sababu upendo ni sawa na mbawa za ndege ambazo
huwezi kusema bawa la kushoto ni muhimu kuliko la kulia.
Chunguza kwa
kujiweka kwenye fungu la mtu wa kupendwa usiyekuwa na chembe hata ya upendo kwa
wenzako.
Jaribu
kuufungua moyo wako upokee mapenzi ya wengine tu bila kurejesha chochote kwao.
Kisha angalia furaha ya moyo wako, bila shaka upendo hautakukidhi, utajiona uko
kwenye upungufu fulani.
Ukiachana na
hilo weka maisha yako kwenye kupenda tu na usirejeshewe mapenzi ya wenzako,
hapo napo utabaini kuwa moyo wako una ganzi na uhitaji wa furaha timilifu;
naamini lipo jambo la kukubaliana kwenye mambo haya mawili.
Ikiwa hivi
ndivyo, tujiulize inakuwaje watu wengi huwa wanatamani kupendwa? Jibu rahisi ni
kuwa, wengi hukwepa gharama za kupenda.
Maana katika
hali ya kawaida kupenda huambatana na gharama na wakati mwingine kukubali kuwa
mtumwa wa mtu fulani, kujitoa kwa ajili ya kutimiza upendo kwa wengine.
Hata hivyo,
uchunguzi unaonesha kuwa, wachagua kupedwa kwa msukumo wa kukwepa gharama
hawajawahi kujitoa kwenye ukweli wa upendo kuwa sawa na mbawa za ndege kwani
hata wakiacha kupenda bado wanagharimika.
Ni wazi;
kumvutia mtu akupende nako kuna shida zake na kibaya zaidi utumwa utegemezi wa
akili na mahitaji ni gharama inayotajwa kuwa kubwa na mbaya zaidi.
Umewahi
kujiuliza mateso ambayo huyapata wanaopendwa pale wanapobaini kuwa waliowapenda
wamewaacha.
Kwa kuwa
siyo msingi wa mada hii kuelezea hayo; ni bora kurejea kwenye msingi wa somo
letu kwa kuweka wazi jambo moja kuwa, upendo ni mbegu inayoota na kuzaa matunda
ya jinsi yake.
Ukitaka
kuyafanya maisha yako yawe mazuri, yatoe mafanikio mengi, basi ifanye mbegu ya
upendo aliyoipanda mumeo/ mkeo, ndugu jamaa na rafiki zako izae moyoni mwako.
Usiishie
kutafuta wa kukupenda jaribu kutafuta wa kumpenda pia hata kama utaniuliza
swali zoefu kuwa wengine hata hawapendeki; hicho usikifanye kuwa kikwazo cha
maisha yako ya furaha kwa sababu hujui unayeishi naye ameletwa duniani kufanya
nini na lini ataondoka.
Kwa
kumalizia makala haya hebu yaweke maisha yako kwenye kipimo. Ni mara ngapi
umejisifia mbele za wenzako kuwa unapendwa? Je upendo huo umekuwa na maana
kwenye maisha yako?
Mtafakari
mpenzi wako, muunganishe na hisia zako kisha ujipime amekuletea furaha
toshelevu? Ikiwa moyo wako unaona bado haujatosheka naye tambua kuwa hujalipa
upendo wake na kwamba unajitesa moyoni na kuuongopea ulimwengu kuwa unapendwa.
Baada ya
kutazama hilo, jaribu kugeuza upande mwingine
kwa kujiuliza upendo wako umekuletea furaha timilifu. Unalidhika
kumpenda mtoto wako kiasi cha kusikia furaha isiyo na kifani? Kama kuna dosari
hufiki kwenye kilele tambua unaudanganya ulimwengu. Upendo wa kweli haupo!
Kwa leo
naomba niishie hapa wakati mwingine nitachambua zaidi somo hili kwa kuangalia
misingi ya upendo na kuelezea aina zake kwa undani zaidi. Asante kwa kuwa nami
karibu tena Alhamisi ijayo kwenye mada nyingine nzuri zaidi!
No comments:
Post a Comment