Leo nimekuja na mada mpya ambayo
inawahusu wale ambao wametengana katika uhusiano wao. Wengi wamezoea
kukurupuka pindi wanapoacha na kuishia kutoa maneno makali kwa wenzi wao
wa zamani.
Kamwe usithubutu kumshusha thamani
mwenzi wako wa zamani. Maneno kama ‘alikuwa hanitoshelezi’ na mengine
yenye sura ya kumponda hayana nafasi. Maisha yanaendelea, usipoteze muda
wako.
Una mengi yanayohitaji utekelezaji wako.
Muda wa kumchukia mwenzi wako wa zamani na ule wa kufanya shughuli kwa
ajili ya maendeleo yako, utaupanga vipi?
Watu wengi wamekuwa kama mandondocha
kwenye mapenzi yao kutokana na tabia ya kushindwa kuchanganua busara za
kuachana. Wanakimbilia kuchukia, matokeo yake wanateseka.
Mantiki ya kumchukia mwenzi wako
mliyeachana ni matokeo ya kushindwa kuchukulia hali ya kutengana kwenu
kama ya kawaida. Unadhani ni tukio kubwa, hivyo unaupa mzigo mzito moyo
wako.
CHUKUA MFANO HUU:
Deo anampenda sana Suzane lakini anajua
fika kwamba mwenzi wake hajatulia. Hata hivyo, anashindwa kujipanga
kuchukua hatua muafaka.
Deo anakuwa mtu wa kulipuka, akiudhiwa
na mwenzi wake anatangaza kuachana naye bila kutafakari mara mbili.
Haishii hapo, anaamka na chuki mtindo mmoja, hata akimkuta barabarani
hamsalimii.
Je, hiyo ni dawa? La hasha, kwa kawaida
chuki yako itakupeleka katika mawazo mengi. Utamkumbuka kwa mabaya yake
lakini hutaishia hapo, utaanza kuyaona mazuri aliyokufanyia.
Ni kipindi hicho ambacho utaanza kuumia
zaidi. Utatamani yale mazuri yake. Inawezekana ukakosa aibu na kujikuta
wewe mwenyewe ndiyo unaomba msamaha mrudiane.
Ukiwa na chuki na mwenzi wako, maana
yake hisia zako bado zipo kwake. Akija kuzungumza na wewe ni rahisi
kumsamehe bila kuzingatia uzito wa kitu alichokufanyia.
Nakusisitiza kujua kwamba kinyume cha
mapenzi siyo chuki. Ni kutojali (kupotezea). Yaani unapokosana na mwenzi
wako, usianze bifu, badala yake anza kumpotezea na usimjali kwa
chochote.
Unahitaji kuwa huru na hisia zako.
Unapoamua kuacha basi simamia uamuzi wako. Ukizingatia mambo yafuatayo,
yatakupa msaada mkubwa wa kuvuka kipindi kigumu cha kuachana na
mwenzako.
- Mara unapoachana na mwenzi wako, hakikisha unasitisha mawasiliano naye. Iwe kwa simu, ana kwa ana na mengineyo.
- Acha kukaribisha hisia kwamba ipo siku wewe na yeye mtarudiana. Amini kuwa hiyo imetoka jumla, fanya mambo yako ukiamini kwamba mwenzi wa maisha yako anakuja.
- Fanya mambo chanya kama kujifunza vitu vipya, kufanya kazi kwa bidii, kujitolea kwa ajili ya watu wengine, kutoa misaada na kufanya mazoezi ya viungo.
Ukiyafanya haya yatakuwezesha kuondoa
mawazo hasi kwa mwenzi wako mliyeachana na kuzingatia vitu vya msingi
ambavyo vinahusu ujenzi wa maisha yako ya sasa na ya baadaye.
MUHIMU:
Achana na hulka za chuki kwa mwenzi wako
wa zamani. Tangu ulipokuwa mdogo mpaka sasa umekutana na marafiki
wangapi ambao wengine leo hawamo kwenye kumbukumbu zako?
No comments:
Post a Comment