Sidhani
kama kuna ambaye hajawahi kujikuta kwenye majibizano na mpenzi wake,
ziko hata nyakati mnaingia katika mlipuko wa majibizano hata mnashindwa
kujua sababu ya kujibizana kwenu. Vitu kama vile mmoja kuchelewa kurudi
nyumbani, kushindwa kuwasiliana sawa na mwingine alivyotarajia,
kushindwa kutoa msaada pale ulipohitajika, hisia za kuwepo kwa mahusiano
pembeni, tabia zisizoeleweka baina ya mmoja na simu yake ya mkononi, au
ndugu zenu kuingilia mahusiano yenu kwa namna yeyote ile. Haya ni
baadhi tu ya maeneo ambayo wengi wetu tumejikuta tunapishana kimaneno na
wapenzi wetu. Mara nyingine inatokea mmepanga kwenda kula au kunywa nje
ya nyumbani “outing” mnafika tu sehemu husika mkiwa mnasubiria chakula
au mmeshaanza kula mara mmoja wenu anatoa neno moja linaloamsha
majibizano makali sana ghafla ile raha ya kuendelea kuketi na kula pale
inaisha, mnaamua kukiacha chakula na kuamua kuondoka, tena ikiwezekana
kila mmoja kwa njia yake. Najua kama ingekuwa tuko darasani nikasema
wanyooshe mikono wale ambao hali kama hizi au zinazo fanana na hizi
zimewahi kuwatokea wengi wangenyoosha mikono.
Inabidi
kuwa makini sana kwasababu kutofautiana katika maneno kunaweza kuwa na
muendelezo bila hata ya nyie kugundua na baadae kuwapeleka pabaya.
Kwamfano, wapenzi hawa wawili wanaanza taratibu katika maongezi yao “leo tunakula nini” mmoja anauliza, mara anajibiwa “kwanza kila ukimaliza kula unaacha vyombo mezani badala ya kunisaidia hata kuvisogeza wakati unajua tuko wawili tu?”Baada ya muda kupita na majibizano kama haya kuendelea, mmoja anaanza kuchoka na kumwambia mwenzake “mimi
naona tunatofauti kubwa sana kwenye mambo ya majukumu ya hapa ndani na
kwa jinsi hii sioni kama tutawezana bora kila mtu afuate ya kwake”. Hapa
uaona kuwa majibizano yaliwahi kuanza muda mrefu huko nyuma ila
yalikuwa na muendelezo hata pasipo wapenzi hawa kugundua na hivyo
kuwapelekea kutengana.
Kutofautiana
katika maneno na mpenzi wako kunauma na unaweza ukatamani kufungua
mlango wa gari likiwa katika mwendo utoke ili tu uondokane na kinywa
chake. Hali hii inapozidi unaweza kujikuta unayatilia shaka mahusiano
yenu na kuanza kuwa na hisia za kuyasitisha. Lakini hatuwezi kuukwepa
ukweli kwamba majibizano na kutofautiana ni kitu cha asili kwenye
mahusiano yeyote, jambo hili limetiliwa mkazo na wataalamu wengi wa
mahusiano akiwemo mshauri Beth Fitzpatrick. Tafiti zinaonyesha kwamba
wapenzi wengi wanaohudhuria huduma za ushauri wamekiri kwamba matatizo
kama vile mawasiliano mabovu, kushindwa kusikiliza, kutojali, kupinga
kila kinachosemwa au kutendwa, na kutumia lugha za matusi yamekuwa
yakudumu katika mahusiano yao. Yamkini hali hii ipo pia katika mahusiano
yako.
Kama
nilivyokwisha kusema awali, kwa kule kupitia katika majibizano
hakumaanishi kwamba mahusiano yenu yanamatatizo, kinyume chake ni kwamba
mahusiano yeyote yasiyopitia majibizano na kutofautiana yanaweza kukosa
ubora unaotakiwa kimahusiano au kindoa. Maranyingine wapenzi wanaosema
hawajawahi kutofautiana au kugombana wana madhaifu mengi tofauti na vile
wanavyoonekana mbele za watu. Kule kukosa mazingira ya kutofautiana
katika mahusiano yenu kunaweza kuwa na madhara makubwa kuliko kuwa na
mazingira ya kutofautiana, wale wenye kukosa kutofautiana kimaneno
wanaweza kuwa na tabia kama vile ukatili wa kimya kimya, kunyamaziana,
kuziriana, kununiana, kunyimana tendo la ndoa na pia kukwepana. Tabia
hizi zina madhara makubwa katika mahusiano. Kama mazingira ya
kutofautiana yapo na ni dhahiri, kwanini msitofautiane? Cha muhimu ni
kuchagua kutofautiana kwa namna inayojenga na sio inayobomoa.
Na: Dr. Chris Mauki
Social, Relationship and Counseling Psychologist
UDSM/CHRISTOM SOLUTION
chrismauki57@gmail.com
No comments:
Post a Comment