Ni Ijumaa nyingine nzuri ninapokukaribisha msomaji wangu katika zulia jekundu la uwanja wetu huu ambao ni maalum kwa mambo yahusuyo uhusiano wa kimapenzi. Mada ambayo ningependa kujadiliana nawe msomaji wangu ni kama inavyojieleza kwenye kichwa cha habari.
Yawezekana wewe ni mwanaume au mwanamke
ambaye unafanya kazi na umpendaye, awe ni mke, mchumba au mpenzi. Je,
kuna faida gani unazozipata kutokana na kufanya kazi ofisi moja na
umpendaye? Vipi kuhusu hasara na changamoto?
Bila kujali kama mmekutana sehemu ya
kazi na kuanzisha uhusiano wa kimapenzi au mlianza kabla lakini baadaye
mkajikuta mkifanya kazi sehemu moja, lazima ujue kwamba zipo faida
lakini kama hiyo haitoshi, zipo changamoto nyingi ambazo ni lazima ujue
namna ya kuzishughulikia ili kuwa na uhusiano bora wa kimapenzi na amani
ya nafsi yako.
FAIDA KUBWA
Faida kubwa ya kufanya kazi pamoja ni
kwamba unapata muda wa kutosha wa kuwa karibu na mwenzi wako. Kwa wale
ambao wana hulka ya wivu au wanashindwa kuwaamini wenzi wao, kufanya
kazi pamoja huwasaidia kutulia kwa sababu watakuwa na uhakika na mahali
walipo au shughuli wanayoifanya wenzi wao kwa sababu wanawaona na
wanashinda nao siku nzima.
CHANGAMOTO ZAKE
Changamoto za kufanya kazi ofisi moja na
umpendaye, huwa ni nyingi kuliko faida na usipokuwa makini zinaweza
kusababisha kuyumba, kulegalega au kuvunjika kabisa kwa uhusiano wako wa
kimapenzi na umpendaye.
Changamoto ya kwanza na kubwa huwa ni
kushindwa kutenganisha mambo ya nyumbani na mambo ya kazini. Kama jana
usiku mlikorofishana na mwenzi wako, uwezekano mkubwa ni kwamba chuki za
nyumbani utazileta kazini na matokeo yake, ufanisi wa kazi utapungua.
Pia, kihulka binadamu ameumbwa kuwa na
muda wa kukutana na watu wengine, kubadilishana mawazo na kuingiza vitu
vipya kichwani. Sasa inapotokea wewe na mwenzi wako mnafanya kazi
pamoja, ni kwamba mtajikuta muda mwingi mkiutumia pamoja na kushindwa
kuchanganyika na watu wengine, jambo ambalo kitaalamu husababisha msongo
wa mawazo.
Changamoto nyingine, ni pale inapotokea
mmoja kati yenu ameharibu kazi. Kwa kawaida, mabosi huwa wakali
inapotokea mfanyakazi amefanya kosa lililosababisha hasara, iwe ni kwa
bahati mbaya au makusudi.
Mabosi wengine hufikia hatua ya
kuwafokea au kuwaadhibu waliofanya uzembe huo. Utajisikiaje mwenzi wako
anapoadhibiwa mbele yako kwa sababu amefanya makosa kazini?
Vipi kuhusu mwenzi wako anapokorofishana
na wafanyakazi wenzake? Wahenga walisema vikombe vinapokaa kabatini
pamoja, havitakosa kugongana. Hivyo mwenzi wako anapofanya kazi, ni
lazima itatokea akakorofishana na wafanyakazi wenzake.
Je, utajisikiaje kusikia mwenzi wako
akitukanana au kupandishiana na mtu mwingine kwa sababu ya kazi?
Kimsingi utaambulia ‘stress’ za kutosha ambazo huenda zikapunguza
ufanisi wako wa kazi.
NINI CHA KUFANYA?
Licha ya changamoto nilizozieleza hapo
juu, wapo wapendanao wengi ambao huweza kudumu na kuishi maisha ya
furaha japokuwa wanafanya kazi ofisi moja. Hata wewe unaweza kuwa na
uhusiano bora licha ya kuwa unafanya kazi ofisi moja na mwenzi wako
endapo utazingatia mambo ya msingi ambayo nitakufafanulia kwa kina
kwenye sehemu ya pili ya makala haya.
Usikose wiki ijayo ambapo tutaangalia
kwa kina mbinu za kupambana na matatizo yanayotokea kazini kwa sababu ya
kufanya kazi ofisi moja na mwenzi wako.
No comments:
Post a Comment