Moja
ya imani ambayo imekuwa ikileta malumbano katika jamii ni kuhusu mtoto
kubemendwa, ikimaanisha mtoto aliyezaliwa kutopiga hatua za ukuaji au
kulemaa viungo vya mwili.
Dhana hii iliyoonea maeneo ya Pwani
hususan mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Lindi, Tanga na Morogoro
inaelezwa kuwa inatokana na wazazi wa mtoto kujihusisha na mapenzi pindi
anapokuwa bado mchanga.
Wengine huwaita watoto hao kwa majina ya
kukejeli ikiwamo ‘fundi viatu’, kutokana na mwonekano wa mtoto ulivyo,
kwani huwa hawezi kutembea, kutambaa wala kuongea.
Wapo wanaosema kuwa chanzo cha watoto
kupata hali hiyo, ni pale wazazi wanaposhiriki tendo la ndoa kupita
kiasi wakati mtoto akiwa bado mchanga na ananyonya.
Sababu nyingine ni mwanamke mwenye mtoto mdogo kujihusisha na uzinzi nje ya uhusiano akiwa bado ananyonyesha mtoto.
Inaelezwa kuwa mwanamke anapofanya ngono
huku mtoto akiwa ananyonya, mtoto anaweza kunyonya maziwa
yaliyochanganyika na mbegu za kiume na hivyo kumdhuru.
Wazazi wanaokumbwa na kadhia hii
huwaficha watoto wao au hata kuhama makazi kwa kuhofia aibu. Kibaya
zaidi ni pale wazazi wanapotuhumiana na kisha kufarakana kwa sababu ya
hali hiyo.
Upi ukweli?
Kwa namna tukio la kubebemendwa kwa
watoto linavyoelezwa na wanajamii, ni dhahiri linahusiana moja kwa moja
na tatizo la mtoto aliyezaliwa na kushindwa kupiga hatua za maendeleo ya
ukuaji wa kimwili, kiakili na kijamii.
Pia, inahusu watoto waliopata jeraha la
kudumu la ubongo na hivyo kupooza viungo au kuwa na viungo vyenye
kulemaa na kuchelewa kupiga hatua za ukuaji; kitaalamu tatizo hili
hujulikana kama ‘Cerebral Pulse’.
Kitabibu, mtoto mwenye ukuaji hafifu
huwa na kawaida ya kuwa mfupi na uzito huwa ni mdogo, kulinganisha na
watoto wengine wenye umri sawa.
Kwa wale waliofikia ujana wanaweza kuonekana wakiwa wamedumaa na huku wakiwa na mabadiliko yasiyo ya kawaida wakati wa balehe.
Kimsingi, kubemenda mtoto ni dhana na
imani potofu. Kisayansi na kitiba kufanya mapenzi hakusababishi mtoto
kuduma au kutokuwa na uwezo wa kukua.
Pia, sio sahihi kuwa mbegu za kiume
zinaweza kupenya na kuingia katika mfumo wa damu wa mama na kufika
katika vifuko vya maziwa na kisha kumwathiri mtoto anayenyonya.
Kwa kawaida mbegu hizo hubebwa na
majimaji mazito na hatimaye kuingia katika nyumba ya uzazi na kubaki
huko. Zinazobaki hushuka na kutoka ukeni mwanamke anapokuwa amesimama na
nyingine huvunjwahuvunjwa au kuharibiwa na vimeng’enya vya mwili na
kutoka pamoja na uchafu mwingine.
Inawezekana kama baadhi ya watu
wanavyosema, wazee wa zamani walitunga uongo huu, ili kuwatisha watu
wasishiriki tendo la ndoa baada ya mwanamke kujifungua.
Ni kweli siyo vyema kushiriki tendo la
ndoa mara baada ya kujifungua. Kitaalamu tunashauri angalau zipite wiki
sita au siku 40, kama ilivyozoeleka kijamii; hii inaepusha kupata
maambukizi ikiwamo ya nyumba ya uzazi.
Kwa kawaida wiki za mwanzo baada ya
kujifungua mazingira ya uke yanakuwa na unyevu pamoja na mabaki au
majimaji yaliyochanganyika na damu ambayo yanaweza kuwa ni mazalia ya
vimelea. Mabaki hayo yanaweza kuacha kutoka baada ya wiki mbili mpaka
nne.
Sababu za kitabibu zinazochangia mtoto kutokukua
Watoto wenye tatizo la ukuaji, huonekana
wakiwa na ukuaji hafifu kwa upande wa tabia za kimaumbile, ikiwamo
kushindwa kutambaa, kukaa, kusimama na kutembea. Pia, huwa na maendeleo
ya taratibu kiakili, kijamii na tabia zinazoashiria jinsia yake ikiwamo
kubalehe.Kwa kawaida mtoto hupitia hatua mbalimbali za ukuaji na kila
hatua huwa na tabia zake. Kwa mfano, mtoto anapokuwa mchanga ndani ya
miezi miwili anatakiwa awe amekaza shingo au anapokuwa na mwezi mmoja
awe anatabasamu kwa watu wa karibu.
Yapo matatizo mengi ya kitabibu yanayoweza kusababisha mtoto asiweze kupiga hatua za ukuaji kama kawaida.
Tatizo hili linaweza kuonekana zaidi
katika jamii zenye hali duni za kiuchumi, ikiwamo maeneo yenye ukame,
vita vya wenyewe kwa wenyewe na wakimbizi.
Mtoto kama hapati maziwa ya mama na
lishe (kwa waliofikia miezi sita na kuendelea) kama invyopendekezwa,
anaweza kukumbwa na tatizo hili.
Kwa mfano, mtoto mdogo wa chini ya miezi
sita anatakiwa kunywa maziwa ya mama pekee; anyonyeshwe angalau mara
nane mpaka 10 kwa siku.
Inawezekana mama akawa hana ujuzi wa
kumnyonyesha katika mtindo sahihi, hivyo kuchangia mtoto kutopata maziwa
ya kutosha. Aidha, ni makosa kuwaanzishia watoto vyakula vya kulikiza
(vya kawaida) kabla ya kufikia umri wa miezi sita.
Sababu nyingine ni mtoto kulishwa
chakula katika mazingira yasiyofaa kama vile kulishwa akiwa anatazama
runinga, kuwa eneo lenye fujo au kutolishwa kwa ratiba.
Matatizo mengine ni pamoja na hitilafu
katika chembe za urithi hali inayochangia kupata mtindio wa ubongo,
kitabibu hujulikana kama Down syndrome na kuzaliwa na hitilafu katika
ogani kubwa ikiwamo moyo na figo.
Pia, matatizo ya tezi zinazozalisha
kichochezi cha ukuaji wa mwili, madhara katika ubongo au mfumo wa fahamu
ambayo yanaweza kusababisha mtoto kushindwa kula, maradhi ya moyo na
mapafu yanayoweza kusababisha utawanyaji hafifu wa oksijeni na
virutubisho mwilini.
Upungufu wa damu na matatizo katika
chembe za damu, matatizo sugu ya kiafya mfumo wa chakula, kupata jeraha
la ubongo wakati kuzaliwa (cerebral palsy) na ujauzito kupata madhara na
kujifungua njiti au uzito mdogo sana.
Sababu nyingine ni pamoja na kuumizwa kihisia kutokana na kuondokewa na wazazi, kutengwa au majanga ya kijamii.
Wito kwa jamii
Kitaalamu hakuna dhana ya kubemenda
mtoto hasa tukio hilo linapohusianishwa na kitendo cha kujamiiana.
Tatizo la ukuaji kwa watoto linatokana na sababu za kiafya na
kimazingira.
Wazazi wazingatie elimu ya afya
inayotolewa katika vituo vya huduma za afya vinavyotambulika. Kina mama
wahakikishe wanafika katika kiliniki za wajawazito na kupata huduma na
ushauri.
No comments:
Post a Comment