Artikel Terbaru

Responsive Ads Here

Sunday, July 30, 2017

HIVI WANAWAKE TATIZO LENU NI NINI MBONA HIVIIIII??



KUNA msemo: “Wanawake mwalimu wao ni kipofu.” Mimi siuamini kwa maana umekaa kiukandamizaji zaidi. Haujengi heshima kwa mtu wa jinsi ya kike tangu anazaliwa mpaka anapoingia kaburini. Binafsi naamini wapo wenye uelewa mkubwa lakini wanashambuliwa na mapokeo ya samaki mmoja akioza.
Ni msemo ambao ukiingia kwenye vichwa vya watu unaweza kuwafanya wanaume wawadharau hata mama zao. Mama anatoa mafundisho lakini kijana anasikiliza, linaingilia sikio la kwanza na kutokea la pili. Kichwani anajiongeza: “Aah, hawa si mwalimu wao kipofu?”

Msemo huo unamaanisha kuwa wanawake huwa hawajui waendako. Kwamba njia ya kupita walifundishwa na mwalimu mwenye ulemavu wa macho. Siupendi kwa sababu siyo tu hauna ladha nzuri kwa mwanamke bali pia kwa mtu mwenye ulemavu husika. Unadhalilisha kupita kiasi.
Tangu nikiwa na umri mdogo, nilipenda sana kusikiliza busara za watu walionizidi umri. Niliamini wananijenga na kweli walifanya hivyo. Mtazamo huo, ulinifanya nijue mengi nikiwa na umri mdogo. Hata haya ninayoandika na kushauri, yanatokana na elimu niliyopata kwenye kada tofauti.
Wakati huo sijui ndani ya mwanamke kuna nini, mtu mmoja aliniambia: “Mdogo wangu Luqman, napenda unavyopenda kukaa na sisi wakubwa. Unaweza kuwa na busara katika maisha yako lakini usipokuwa mwangalifu, mwanamke anaweza kukufanya uonekane mwendawazimu mtaani.
“Siku ukiwa na mwanamke, jaribu sana kuwa mwangalifu. Unaweza kumpa kila atakacho lakini mwisho akakuuguza uendawazimu. Ukatembea barabarani unazungumza peke yako kama kichaa au ukiwa nyumbani ukashinda unabwabwaja maneno yasiyoeleweka mpaka majirani wakakuona mwendawazimu.
“Mkeo anaweza kutoka nyumbani anakwenda kumtembelea shangazi yake, kwa kumthamini na kwa sababu huna gari, ukampa fedha ya kukodi teksi. Akitoka njiani, anakutana na dereva teksi anampa lifti. Huwezi kuamini, huyo aliyempa lifti ndiye atamuona bora, mwenye roho nzuri kuliko wewe uliyempa fedha ya kuchukua teksi.
“Matokeo yake ni kwamba akishamuona ni mkarimu sana, anakuwa mnyenyekevu hata kwenye maeneo mengine. Mwisho wanakuwa wapenzi. Hiyo ndiyo tabia ya mwanamke, atasahau mema yako, hatajali watoto mnaolea.” Huyo mtu aliyeniambia maneno hayo anaitwa Jaffari, ni mtu mzima hivi sasa. Enzi hizo nilikuwa nasoma sekondari Mwanza.
Ukweli upo wapi? Ninachoweza kueleza ni kwamba wapo wanawake waungwana mno hapa duniani. Wanadumisha mapenzi ya dhati bila kusaliti licha ya kukumbana na vishawishi kemkemu. Wanajua thamani ya wapenzi wao pamoja na changamoto zinazoweza kuwakabili katika maisha.
Hata hivyo, kuna aina ya wanawake ambao Jaffari alikutana nao ndiyo maana akasema hivyo. Isingekuwa rahisi kutoa maneno hayo pasipo kuona kitu. Inawezekana alitendwa na mkewe au alishuhudia kitu kwa rafiki yake, hivyo kumpa tafsiri aliyojijengea kuhusu wanawake.
Tukishika moja kuwa kuna kitu alijionea, basi ni vema kuwazungumzia wanawake ambao walimfanya akawa na mtazamo huo. Hao ndiyo wanaowaharibia wengine mpaka wanakosa thamani. Mtu anatendwa na mkewe lakini lawama anazielekeza kwa wanawake wote kwamba eti ndivyo walivyo!
Katika hili, busara zimuongoze kila mwanamke kuwa halisi (to be real) kwa wapenzi wao. Jambo ambalo mtu hapendi afanyiwe, basi asianze kumfanyia mwenzake. Heshima, uoga na ‘breki’ katika kauli, vinapaswa kuzingatiwa. Kusaliti maana yake umekosa uoga, heshima na busara ya maisha.
Hekima ni ipi? Kuendelea kuwa na mwenzi ambaye hana heshima juu yako, hakuhofii kwa chochote, wala busara ya maisha haimuongozi kutenda yaliyo mema kwa ajili ya ustawi wa familia yenu. Bila shaka, hekima inafaa kukuongoza kuchukua uamuzi kwa ajili ya furaha na amani ya kudumu baadaye.
Nitoe hoja kuwa hata wanaume wapo matatizo mtindo mmoja, kwa hiyo na wanawake wapo wenye hulka tofauti. Kama huyo wako ni pasua kichwa, basi wapo waliojaliwa utulivu, heshima, hekima na maarifa ya kudumisha uhusiano. Ikiwa huyo anakunyima furaha, angalia kama unaweza kujivua gamba, kwani wapo wanawake wema.
Mungu hajaumba mtu akamfanya kuwa mbaya kwa asilimia 100. 

No comments:

Post a Comment