“Nina mke asiyeniamini kabisa,” aliniambia bwana mmoja hivi majuzi.
“Hana imani kabisa na mimi. Juzi kati hapa nimemkuta anachunguza simu
yangu. Tuligombana sana.” Nilimwuliza kwa nini anafikiri mke wake
hamwamini. “Basi tu ndivyo alivyo. Hata ufanyaje hana imani.”
Sote, kama alivyo bwana huyu, tuna hitaji la kuaminiwa. Tunatamani watu
wasiwe na mashaka na sisi. Tunatamani watu waamini yale tunayowaambia.
Pengine nawe, kama huyu bwana umewahi ‘kuwadai’ watu wakuamini.
Umekwenda kwa rafiki, mathalani, kumkopa fedha. Rafiki yako anasita.
Hakuamini. Kutokuaminiwa kunaumiza hisia kwa sababu, kama tulivyosema,
kuaminiwa ni hitaji la kila mtu. Hata mwongo naye anapenda watu
wamwamini.
Ufanye nini sasa??? Twende pamoja....
A. Kuaminiwa ni matokeo
Mambo mengi hayaendi bila kuaminiwa. Kazini, wakubwa wa kazi wanapenda
mtu anayeaminika. Bila kuaminika, huwezi kupata mafanikio.
Mfanyabiashara naye, anapoaminiwa na watu anakuwa kwenye nafasi kubwa ya
kupata mafanikio.
Urafiki kati ya watu wawili, hali kadhalika, unategemea kwa kiasi
kikubwa namna watu hao wanavyoaminiana. Huwezi kuwa na urafiki mzuri na
mtu kama hamuaminiani. Kuaminiwa ni msingi wa mahusiano yoyote ya karibu
na hata shughuli zinazohusisha watu zaidi ya mmoja.
Kuaminiwa, hata hivyo, si tukio la siku moja wala haki inayoweza
kuidaiwa kwa watu. Mke hawezi kudai ‘aaminiwe’ na mume wake. Mume hali
kadhalika. Kuaminika ni zao la tabia zetu. Kuaminiwa ni sawa miamala ya
Benki. Unaweza kuchukua kile ulichokiweka. Huwezi kudai zaidi. Fanya
mambo matatu uaminiwe.
B. Sema ukweli daima
Fikiria uko mahali na rafiki yako ukamsikia akimdanganya mwenzake kwenye
simu. Hata kama aliyedanganywa ni mwingine, kwa vyovyote vile imani
yako kwa aliyedanganya inapungua. Uongo unapunguza kuaminika.
Ukitaka kuaminika, jenga tabia ya kusema ukweli. Epuka kusema kitu
usichomaanisha kwa lengo tu la kuwafurahisha watu. Usimdanganye mtu hata
kama unajua hatagundua. Ukitambulika kama mtu mwenye tabia ya kusema
ukweli unawafanya watu wasiwe na wasiwasi na maneno yako. Utaaminika.
C. Timiza ahadi zako
Ni rahisi sana kutoa ahadi hasa kama hujiamini na unatamani kuwaridhisha
watu. Hata hivyo, ni vizuri kuelewa kuwa ahadi ni kipimo cha ukomavu
wako. Usipotekeleza ahadi zako watu wanakuchukulia kama mtu asiye na
ukomavu. Huwezi kuaminika katika mazingira unayoonekana huna ukomavu.
Kuliko kutoa ahadi kwa lengo la kumridhisha mtu, ni bora usiahidi
kabisa. Punguza matarajio ya watu kwako, kisha fanya jitihada za kuzidi
matarajio hayo. Unapoahidi kufanya kitu, tekeleza. Ukishindwa
kutekeleza, kuwa mwuungwana. Omba msamaha. Kwa namna hii watu
watakuamini.
D. Heshimu uheshimike
Mtu asiyeheshimika ni vigumu kuaminiwa. Wapo watu wanaaminiwa kirahisi
kwa sababu tu wamejijengea taswira ya heshima kwa jamii. Heshima ni
zaidi ya vitu ulivyonavyo na namna unavyoonekana. Heshima kubwa
unayoweza kupewa na watu inategemea vile unavyowaheshimu. Ukitaka
kuheshimiwa, heshimu watu.
Unapokuwa na tabia ya kuwadharau watu; kujiona bora kuliko wengine; watu
wanakudharau. Hata wale unaowazidi wanastahili heshima. Hata
wanaokukosea na kukutendea mabaya wanastahili heshima. Ukijenga tabia ya
kulipa ubaya kwa wema utashangazwa na matokeo.
Jambo la kukumbuka ni kwamba watu wanaweza kupoteza imani na wewe kimya
kimya. Si kila mtu anaweza kukutangazia kuwa hana imani na wewe. Linda
sana tunda la uaminifu. Imani ikipotea, ni vigumu kuirejesha.
E. Jifunze kwenda na muda
Watu wengine wanashindwa kuaminiwa kwa sababu ya kutotunza au kwenda
muda ipasavyo. Unaaambiwa uje muda fulani kwa mfano saa 7 kamili mchana
wewe unakuja saa 8 kasoro huku ukiwa na sababu lukuki (nyingine zisizo
na maana). Hii ni tofauti kabisa na wenzetu wazungu ambao wao huenda na
muda kisawasawa (Sijamaanisha waafrika/watanzania wote hatuendi na
muda). Kwa taarifa yako ni kuwa watu hupimwa uaminifu kwa uwezo wao wa
kutumia muda vizuri.
Habari njema, hata hivyo, ni kwamba kadri unavyojiwekea mazingira ya kuaminika, ndivyo utakavyoendelea kuaminika.
"When you're honest from the beginning you don't have to lie to cover up
the lie you already told. Honesty is always the best policy"
No comments:
Post a Comment