Moja ya mambo ya ajabu unayoweza kuwa ushawahi kuyasikia ni kwamba mara nyingine uamuzi wako wa kuwa mwanaume mwema sana na unayejitahidi kufanya uhusiano wako wa kimapenzi uwe mzuri muda wote unaweza kukugharimu na kujikuta unaachwa kabisa.
Haitakiwi kuwa hivyo lakini mara nyingine inatokea, na inatokea kwa sababu wazo la mwenza wako kuhusu uhusiano wa kimapenzi laweza likawa tofauti na ulionao wewe. Wengine wana mawazo hasi kuhusu jinsi uhusiano/ndoa inavyotakiwa kuwa.
Hii ndio sababu hutakiwi kuanzisha uhusiano wa kimapenzi na mtu asiye na vipaumbele sawa na vya kwako au asiye na mtazamo mmoja wa kimaisha kama ulionao wewe.
Usipozingatia hilo, utajikuta unaingia kwenye uhusiano na mtu ambaye hatakujali vya kutosha kwakuwa labda humfokei au kumpiga anapokukosea – au utajikuta ameshakupanda kichwani na kuanza kukudai mambo ambayo huwezi kuyatimiza lakini ukajikuta unajitutumua kumtimizia kwa sababu unataka kumfurahisha mpenzi wako na analijua jambo hilo.
Kwa sababu baadhi ya wanaume wanapenda kulinda siri na kuwaachia uhuru wapenzi wao, wanajikuta wakiwapa ruhusa wanawake zao kwenda popote wanapojisikia bila kuwafatilia wanachofanya.
Nini kinafata baada ya hapo? Mwanamke anatoka, anatafuta mchepuko na kukusaliti. Mwisho inakufanya wewe mwanaume uonekane mjinga mbele ya wengine.
Tatizo ni kwamba tabia hii inaibuka kutokana na mazoea ya watu kuingia kwenye uhusiano wakiwa wameficha tabia zao halisi na kuja kufungua makucha yao baada ya kuona ameshaishi na wewe kwa muda mrefu kiasi kwamba huwezi tena kumuacha.
Hii inasababisha wanaume walioathirika kutokana na tabia kama hizi kutoka kwa waliokuwa wapenzi wao wasiweze kuwaamini wanawake wengine tena kwa kuona kwamba wote ni sawa na wale waliowaumiza na kusababisha wasiweze kuwaonesha wenza wao wapya mapenzi kwa kiwango cha juu wakihofia kuumizwa tena.
Kuwa mpole, mkarimu na mwenye upendo wa hali ya juu kwa mpenzi wako ndio jambo linalotarajiwa kwenye uhusiano. Mtu hatakiwi kufanywa ajisikie vibaya kwa kumuonesha mapenzi ya kweli mwenza wake.
Kama wewe unakuwa muaminifu na mwema kwa mpenzi wako lakini umekuwa unadharauliwa au ukaachwa kutokana na tabia hiyo, kaa ukiwa na amani kabisa kwamba lawama za kuvunjika kwa uhusiano huo hazikuhusu wewe – lawama ni za mpenzi wako aliyeshindwa kujua wewe umekuwa mwema kiasi gani kwake.
No comments:
Post a Comment