UJUMBE MUHIMU KWA WAZAZI NA WALEZI
Ujumbe huu umekusudiwa uwafikie wazazi pamoja na walezi. Ni ujumbe wenye taarifa muhimu ambazo watu wanazihitaji kwa ajili ya afya bora na ulinzi wa watoto. Zingatia sana ushauri wote na ufanyie kazi kwa afya bora na usalama wa watoto na vijana wako.
- Afya za kinamama na watoto zinaweza kuboreshwa kwa kiwango kikubwa endapo uzazi utapangwa kwa kuzingatia nafasi ya walau miaka miwili tangu kuzaliwa kwa mtoto hadi kubeba ujauzito mwingine. Kupata ujauzito kabla ya umri wa miaka 18 au baada ya umri wa miaka 35 huongeza hatari za kiafya kwa mama na mtoto. Wanawake na wanaume (vijana na watu wazima) hawana budi kufahamu faida za kiafya zinazotokana na upangaji uzazi ili waweze kufanya maamuzi ya busara wao wenyewe.
- Kina mama wote wajawazito wanapaswa kuonana na daktari kwa ajili ya kuhudumiwa wakati wakiwa wajawazito na baada tu ya kujifungua, vilevile wanapaswa kujifungulia mahali ambapo wataweza kupata usaidizi wa mtaalamu wa ukunga. Akina mama wajawazito (na jamii kwa ujumla) tunawaasa waache tabia ya kutumia dawa bila kupata ushauri kutoka kwa mtaalamu wa afya. Kwani kufanya hivyo kuna weza kusababisha ukuaji duni wa ujauzito(mtoto aliye tumboni) na kupelekea mtoto kuzaliwa akiwa na matatizo mbalimbali katika viungo vyake hali ambayo tunaita ni ulemavu. Pia ujauzito unaweza kuharibika kabisa kutokana na kutumia baadhi ya dawa zilizokatazwa kutumiwa na akina mama wajawazito na wanaonyonyesha. Kina mama wote wajawazito pamoja na jamaa zao wanao wajibu wa kuzitambua dalili zozote za hatari wakati wa kipindi cha ujauzito na kipindi cha baada ya kujifungua pamoja na umuhimu wa kumuona daktari pale inapobidi. Aidha wanapaswa wawe wamejiandaa kimipango na kiuwezo kwa ajili ya kupata huduma ya mkunga wakati wa kujifungua na wakati wowote endapo patazuka tatizo la ghafla baada ya kujifungua.
- Watoto huanza kujifunza mara tu wanapozaliwa. Hukua na kujifunza vyema zaidi pale wanapolelewa katika mazingira ya kuwajali, kuwapenda na kuwafurahia wanapotenda jambo, pamoja na kupata lishe bora na huduma nzuri za afya. Kuwatia moyo watoto bila kuwabagua kijinsia, wao kujijali na kujieleza pamoja na kucheza na kuendeleza vipaji vyao huwasaidia kujifunza na kukuwa kijamii, kimwili, kihisia na kiakili.
- Maziwa ya mama pekee ndiyo chakula na kinywaji bora kwa mtoto kuliko vyote katika kipindi cha miezi sita tangu azaliwe. Baada ya miezi sita mtoto hana budi kuongezewa na vyakula vingine vyenye lishe bora na kuendelea kunyonya hadi atakapofikia umri wa miaka miwili au zaidi kwa ajili ya mahitaji yake ya kukuwa kimwili na kiakili.
- Lishe duni wakati wa ujauzito au katika kipindi cha miaka miwili ya mwanzo ya mtoto huweza kuathiri ukuaji wa mtoto kimwili na kiakili katika maisha yake yote. Watoto huhitaji lishe kamili yenye mchanganyiko wa vyakula vya kujenga mwili na vya kutia mwili nguvu. Vilevile huhitaji vitamini na madini kama vile madini ya chuma na vitamini A, kwa ajili ya ukuaji na afya bora. Tangu kuzaliwa hadi kufikia umri wa mwaka 1 watoto wanapaswa kupimwa uzito kila mwezi na kuanzia mwaka 1 hadi 2 wapimwe walau katika kila miezi mitatu. Endapo mtoto ataonyesha dalili za kudumaa kiukuaji, apelekwe kwa daktari.
- Kila mtoto ni lazima akamilishe idadi ya chanjo anazostahili kupata. Upataji wa chanjo katika mwaka wa kwanza na wa pili baada ya kuzaliwa ni jambo muhimu sana kwa mtoto kwa kuwa humkinga dhidi ya magonjwa yanayoweza kumdumaza kiukuaji, kumsababishia ulemavu au hata kifo. Kina mama wote wa umri wa kuzaa, wakiwemo wasichana wanapaswa kukingwa dhidi ya maradhi mbalimbali ikiwemo tetenasi na mengine kwa ajili ya manufaa yao wenyewe na ya watoto watakaowazaa baadaye. Endapo mama hajakamilisha chanjo, itabidi apate chanzo hizo zinazohitajika atakapoenda kliniki. Hivyo ni muhimu kuhudhuria kliniki wakati wa ujauzito na baada kujifungua ili kupata chanjo hizo kwa mama na mtoto. Ni jukumu la mama kupata taarifa hizo za chanjo kwa daktari au mtoa huduma za afya mwingine.
- Mtoto mwenye maradhi ya kuharisha huhitaji majimaji mengi na yanayofaa mwilini mwake, maziwa ya mama na maji yaliyotengenezwa maalumu kwa ajili ya watoto wanaoharisha (ORS), na endapo umri wa mtoto ni zaidi ya miezi sita, apewe pia vinywaji vingine pamoja na vyakula vinavyokubalika kilishe. Apewe dawa ya kufunga kuharisha kwa ajili ya kupunguza makali ya ugonjwa. Endapo choo(kinyesi) cha mtoto anayeharisha kina mchanganyiko wa damu au ni cha majimaji sana na kama anaharisha mara kwa mara, hizo ni dalili za hatari kwa mtoto hivyo apelekwe hospitali bila kucheleweshwa.
- Kwa watoto wengi, magonjwa ya kikohozi na mafua hupona yenyewe bila kutumia dawa. Hata hivyo endapo mtoto mwenye kikohozi na homa anaonyesha dalili za kupumua harakaharaka au kwa shida, hiyo ni hali ya hatari kwa mtoto hivyo inabidi apelekwe hospitali bila kucheleweshwa.
- Magonjwa mengi huweza kuzuilika kwa njia ya kudumisha usafi: kunawa mikono kwa sabuni na maji (au kwa kitu kingine kinachoondosha uchafu kama vile majivu na maji) baada ya kutoka chooni au kumfuta mtoto aliyejisaidia kwa karatasi au kitambaa safi na laini, kutupa kinyesi chooni, au mbali na maeneo ya michezo, maeneo ya kukaa, na vyanzo vya maji, kunawa mikono kabla ya kushika chakula, kutumia maji salama, kutibu au kuchemsha maji ya kunywa ambayo hayatoki katika chanzo salama, na kutunza vyakula na maji katika hali ya usafi.
- Malaria, ugonjwa ambao huambukizwa kwa njia ya kuumwa na mbu, huweza kusababisha kifo. Mahali popote ambapo pana ugonjwa wa malaria watu walale kwenye vyandarua vilivyowekwa dawa. Mtoto yeyote mwenye dalili za homa afanyiwe uchunguzi na daktari kwa ajili ya kupatiwa matibabu na akandwe kwa uangalifu kwa maji ya kawaida (sio baridi). Katika maeneo yenye malaria, kinamama wajawazito watumie dawa za kuzuia malaria kama watakavyoshauriwa na daktari, ikiwa ni pamoja na kumeza dawa za kuwakinga na malaria SP ambazo hupewa kliniki.
- VVU (virusi vinavyodhoofisha kinga ya mwili), virusi vinavyosababisha UKIMWI (upungufu wa kinga mwilini), vinaweza kuzuilika na kudhibitiwa kwa dawa, japo havitibiki. VVU huweza kuenezwa kwa njia ya kujamiiana na mtu mwenye virusi hivyo bila kutumia kinga; kwa njia ya kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa ujauzito, kujifungua au kunyonyesha; na kwa njia ya damu kupitia kwenye sindano za hospitalini, sindano za kawaida au vitu vingine vyenye makali ya kukata au kutoboa. Utoaji wa elimu ya VVU kwa watu wote pamoja na mapambano dhidi ya unyanyapaa na ubaguzi havina budi kuwa sehemu ya maisha yetu ya kila siku ikiwa ni pamoja utoaji wa elimu kuhusu uzuiaji na upimaji wa VVU, pamoja na uhudumiaji wa waathirika. Kutambua mapema pamoja na kutoa tiba kwa watoto na kwa watu wazima huweza kuepusha vifo na kuwajengea waathirika matumaini ya maisha marefu na yenye afya. Watoto pamoja na familia zilizoathirika kwa VVU wanapaswa kupatiwa msaada wa matibabu na lishe pamoja na huduma za ustawi wa jamii. Watu wote wanaoishi na VVU wanapaswa kuzifahamu haki zao.
- Wasichana na wavulana hawana budi kupewa ulinzi sawa katika familia zao, shuleni na kwenye jamii. Endapo ulinzi wa namna hiyo ukikosekana, watoto hukabiliwa na hatari zaidi ya kukumbwa na vurugu, udhalilishwaji kingono, unyonywaji, utumikishwaji, tabia chafu pamoja na kubaguliwa. Kuishi pamoja na familia , uandikishaji wa vizazi, upatikanaji wa huduma za msingi, mfumo wa sheria unaozingatia haki za watoto, pamoja na ushiriki wa watoto katika kujijengea maarifa na stadi za kujilinda wenyewe, ni mambo ya msingi katika ujenzi wa mazingira mazuri kwa watoto kwa ajili ya kuendeleza uwezo wao na kufanikisha malengo yao.
- Majeraha mengi mabaya yanayoweza kusababisha ulemavu au hata vifo huweza kuzuilika endapo wazazi au walezi wengine watawalea watoto wadogo kwa uangalifu, watawawekea mazingira salama na kuwafundisha namna ya kuepuka ajali na majeraha.
- Familia pamoja na jamii kwa jumla ni lazima wawe tayari kukabiliana na dharura wakati wowote. Katika majanga, migogoro, magonjwa ya mlipuko au ya msambao, watoto na kinamama wanapaswa kuhudumiwa kwanza, ikiwa ni pamoja na kupewa huduma muhimu za afya, lishe ya kutosha, kuungwa mkono katika unyonyeshaji wa watoto na kupewa ulinzi dhidi ya vurugu, udhalilishwaji na unyonywaji. Watoto wapewe nafasi ya kushiriki katika burudani na ya kujifunza katika sehemu salama na zenye kuwajali watoto na katika maeneo yenye nafasi ya kutosha kwa ajili ya kuwajenga kiutu na kwa kujiamini. Watoto hawana budi kulelewa na wazazi au watu wazima katika familia zao ili waweze kujisikia huru na salama.
Tunawatakia afya njema!
Ujumbe huu umeletwa kwako na Mtaalam wa Uuguzi, Ukunga na Malezi Ndugu Juma Mbiku.
No comments:
Post a Comment