Artikel Terbaru

Responsive Ads Here

Tuesday, January 16, 2018

HAYA NI MAPENZI KWELI AMA?????????



MAPENZI ni pasua kichwa. Yanaumiza na kuwachanganya wengi. Kwa upande wa pili, mapenzi ni mazuri, matamu na yanasisimua sana. Ni namna ya kujipanga tu.


Ukitaka kuwa kwenye mateso au furaha ni wewe tu! Rafiki zangu, tunaendelea na mada yetu iliyoanza wiki iliyopita ambapo leo tunafikia tamati. Nawashukuru wote ambao mnanitumia meseji za kunipongeza kwa darasa ninalotoa.
Tunaangalia namna ya kujua penzi la dhati hasa kwa wasichana ambao hudanganyika na kukaa kwenye urafiki usio na dira kwa muda mrefu (zaidi ya miaka mitatu).
Wiki iliyopita nilifafanua mengi lakini niliishia pale nilipouliza, mwenzi wako yukoje? Tabia zake zinaeleweka? Anaonekana ana nia ya kuendelea na wewe hadi kufikia kwenye ndoa? Hapo ndipo tunapoanzia leo.
MCHUNGUZE
Huwezi kumjua kabla hujamchunguza. Tenga muda wa kumchunguza vizuri mpenzi wako. Achana na tabia za kukutana naye kwa ajili ya faragha tu, baada ya hapo huna muda naye.
Ikiwa utapata muda wa kuwa naye karibu kwa muda kidogo, utagundua mambo mengi. Namna anavyokupa thamani kama mwenzi wake na mengineyo, yanaweza kukupa picha ya kuwa upo kwenye uhusiano na mtu wa namna gani.

DALILI ZA KUCHOKWA
Ikiwa mpenzi wako amekuchoka na anataka kukuacha lakini hana sababu, kuna mambo kadhaa utayaona kutoka kwake. Inatakiwa kuwa makini sana kuyasoma na kuyagundua.
Kwanza hataki muonane mara kwa mara. Visingizo vyake sasa vitakuwa ni kazi. Kila wakati atakuwa anasingizia kuwa yupo bize na kazi au ratiba zimeingiliana.
Ili kutambua kuwa hii ni sababu ya kutunga, ratiba yake ya zamani haikuwa ngumu, kazi atakuwa anafanya ileile katika mazingira yaleyale, lakini sababu kubwa hapo ni kwamba atakuwa amekuchoka na hataki kuonana na wewe kwa sababu si mwanamke wa ndoto zake.
Hatapenda mawasiliano ya mara kwa mara. Wakati mwingine unaweza kumpigia asipokee, baadaye akakutumia ujumbe wa kisingizio kilekile – bize. Ukimtumia meseji atachelewa kujibu lakini majibu yake yatakuwa kwa kifupi sana.
Ikiwa utaonana naye, hatapenda mazungumzo mengi, kubwa kwake itakuwa kukutana kimwili, maana kwa sasa hana cha muhimu kwako zaidi ya ngono tu! Lingine ni kwamba, hatataka uiguse simu yake kabisa.
Hata kama si kwa kumchunguza lakini atakuwa makini sana na simu. Anakuwa makini kwa sababu anajua kuna mambo ambayo hapendi uyajue. Ukiona dalili hizi ujue wazi kuwa, urafiki wenu una mashaka na kinachosubiriwa hapo ni kutafutiwa sababu tu ili uachike.

PETE YA UCHUMBA VIPI?
Kuna wengine hudanganyika na pete za uchumba wanazovalishwa vichochoroni. Hajafika kwa wazazi, pete wanavalishana hotelini au kwenye nyumba za wageni.
Pete isiharibu mustakabali wa maisha yako. Kuna shida gani kununua pete ya laki tatu, ukavalishwa halafu akajihakikishia kuwa na mtu wa kumpa starehe?
Kama kweli anakupenda anatakiwa kujitokeza nyumbani ili ajitambulishe na kukamilisha taratibu zote ili muwe huru. Kuna uchumba wa kiini macho, kuwa nao makini.
Mwingine anaweza kufika hadi nyumbani, akakuvalisha pete lakini ukiangalia mwenendo wake utagundua kuwa si mwenye lengo la kweli la kufikia kwenye ndoa.

ANGALIA MBELE
Mwamuzi wa mwisho wa maisha yako ni wewe mwenyewe. Usidanganyike. Ukiona hakuna kinachoeleweka ni vyema kama utachukua uamuzi. Hata kama utakuwa mgumu, lakini ni afadhali ufanye hivyo ili uwe huru.
Inawezekana kung’ang’ania kwako uhusiano usio na mwelekeo ndiyo kujikosesha mwanaume mwenye msimamo na nia ya dhati ya kukuoa. Fikiri kwa makini kisha ufanye uamuzi sahihi.
Ni vyema sasa kama utapima, kabla ya kuendelea kupoteza muda wako kwa kisingizio cha urafiki. Muda haukusubiri, unakwenda mbele. Amua sasa!
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Saikolojia ya Uhusiano anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Kwa sasa anaandaa kitabu chake kipya cha Maisha ya Ndoa.

No comments:

Post a Comment