Wazazi wanatakiwa watambue kwamba kila ambacho wanakifanya kwa watoto wao, kinawatengeneza kulingana na sifa halisi. Mwana akiwa kiburi, mara nyingi hayo ni matunda ya wazazi walivyokuwa wanamvimbisha kichwa alipokuwa mdogo.
Mathalan; akiwa mdogo alikuwa mchokozi lakini haguswi, yaani haadhibiwi kabisa. Anatukana watu lakini mtu akitaka kumtandika kwa nia njema kabisa kabisa ya kumfunza adabu, mama au baba mtu anakuwa mbogo, tena anakuwa tayari kurusha ngumi. Mtoto anajifunza hilo kwamba hatakiwi kuguswa na kwamba mama au baba yake anaweza kuchafua hali ya hewa kwa ajili ya kumpigania. Hiyo ni picha ambayo huingia moja kwa moja kwenye ubongo wa mtoto kisha kumjenga.
Hujawahi kuona mtu yupo na mwenzi wake lakini mgogoro mdogo tu anaomba kuachana? Kama bado, utakuwa umewahi kushuhudia mwanaume mpenda kutimua mke kwa ugomvi mdogo au mwanamke mkimbilia kwao kwa sababu dhaifu tu.
Sababu ni kwamba wazazi hawakuwalea watoto wao katika misingi ya uvumilivu. Katika mapenzi, inafaa viwepo vipindi ambavyo wawili wanaopendana wanaweza kutofautiana na bado ikawa haiitwi ugomvi. Ustahimilivu ukachukua mkondo kisha wakaendelea kuwa pamoja.
Unakuta mwanaume anakuwa mgomvi tu ndani ya nyumba. Hakawii kushusha kipigo kwa mkewe au watoto. Usiwaze sana, pengine huo mkono mwepesi ni matokeo ya makuzi aliyopitia. Kama yeye alikuwa anapigwapigwa, unatarajia nini?
Mtoto wa kiume alikuwa anamshuhudia baba yake alivyokuwa anatoa kipigo kwa mama yake. Ndani ya akili yake, inajengeka picha kuwa mume kumpiga mke ni suala la kawaida, yaani ni sawa na mzazi kumkanya mtoto. Ugubegube huanzia hapo.
Mtoto wa kike akiwa chini ya mamlaka ya wazazi, alikuwa anashuhudia mama akimwendesha puta baba yake. Alimuona mama yake akiwa siyo mtulivu nyumbani, anazurura mpaka usiku wa manane akirudi nyumbani amelewa, hajui watoto wameshindaje.
Naye katika maisha yake ya uhusiano anaona ni kawaida kuenenda kwa mtindo uleule wa mama yake. Hamjali mumewe, yeye misele ya usiku, akirudi yupo bwiii! Mume ndiye atajua maendeleo ya watoto, mama hana analolitambua.
Hasara kubwa zaidi ni pale mume anapohoji kuhusu mwenendo wa mke wake, kwa mshangao anajibiwa: “Kwani kuna nini cha ajabu? Haya ni maisha ya kawaida tu, baba alikuwa analala nyumbani, mama anakwenda viwanja na marafiki zake lakini mbona walidumu?”
Muongozo wa maisha kwa jumla, ni taaluma inayokutaka wewe usiwe kituko kwenye jamii. Ni vizuri pia ukawa na fikra huru za kuchambua kwa urefu na mapana, tabia ya wazazi wako, kama walikuwa sahihi au vinginevyo. Wanasema akili za kuambiwa, changanya za zako.
NINI CHA KUFANYA?
Kwanza tuwe tumeshakubaliana na ukweli kwamba mzazi ni kichocheo cha mtoto kuwa mhusika bora katika mapenzi, baada ya hapo tutakuwa na mawazo yanayoshabihiana kwamba gubegube au gumegume mara nyingi ni matokeo ya malezi mabaya.
Hata hivyo, haina maana kuwa unaweza kusamehewa na kuachwa kama ulivyo eti kisa ndivyo ulivyolelewa au ndivyo ambavyo umejifunza kutoka kwa wazazi wako kutokana na picha uliyokuwa ukiishuhudia kwa baba na mama.
Niongezee pia kuwa suala la ugubegube na ugumegume ni matokeo ya malezi kwa maana kwamba inawezekana wazazi wakawa wazuri sana lakini wakashindwa kusimamia vizuri ukuaji wa watoto wao na matokeo yake kukabidhi jukumu la malezi kwa watu wengin
No comments:
Post a Comment