Nawasalimu wa jina la YESU, jina kuu kupita majina yote. Jina langu
ninaitwa Theoflida , ni mwanamke mwenye umri wa miaka 38 mkaazi wa Mbezi
ya Kimara jijini Dar Es Salaam, japo kiasili ni mwenyeji wa wilaya ya
Ulanga, mkoani Morogoro..
Nime amua kuandika waraka huu kwa madhumuni makuu mawili, kwanza ni
kushuhudia MATENDO MAKUU ambayo YESU AMENITENDEA na pili, ni kuwa hasa
wanawake wenzangu kutojihusisha kabisa na masuala ya WAGANGA WA KIENYEJI
kwa sababu waganga wa kienyeji ni MAWAKALA WA KAZI ZA SHETANI HAPA
DUNIANI na ni MASHETANI KABISA!...
Nitaanza kwa kuelezea kisa kilicho nipelekea kuingia kichwa kichwa kwenye mikono ya wakala wa shetani..
Nilikuwa nimepanga chumba kimoja maeneo ya Tabata Mawenzi huku
nikijihusisha na biashara ya genge. Jirani na nyumba niliyokuwa
nimepanga, aliishi mwanaume mmoja na mke wake. Mwanaume huyu jina lake
linaanzia na herufi K hivyo katika maelezo yangu nitakuwa nikimtaja kwa
herufi K.
K alikuwa ni mwanaume mwenye mafanikio makubwa katika maisha mwenye kazi
nzuri. Alikuwa na nyumba zaidi ya moja, magari ya kifahari. viwanja ,
mashamba, na miradi mbalimbali iliyokuwa ikimlipa vizuri sana. Kwa ufupi
K alikuwa tajiri mwenye maisha mazuri.
K na mke wake wote walikuwa wenyeji wa wilaya ya Muleba,mkoani Kagera . Ndoa ya K na mkewe ilikuwa na umri wa mwaka mmoja...
K na mke wake waliishi maisha mazuri sana....Kwa sababu ya ugumu wa
maisha yangu, nikajikuta naanza kutamani maisha ya mke wa K.. Nikawa
natamani mimi ndo ningekuwa mke wa K na kufurahia maisha vile mke wa K
alivyo kuwa akifurahia. Nilimuona mke wa K kama mtu mwenye bahati sana
na kutamani bahati hiyo iwe yangu.
Baada ya wazo hili kukomaa ndani ya nafsi yangu, nikaanza kutafuta njia
ya kumteka K kimapenzi na kuchukua nafasi ya mke wake. Njia pekee niliyo
ona inafaa, ni kutumia uchawi.
Sasa basi, kuna rafiki yangu mmoja, anaitwa Pamela. Pamela alikuwa
anapenda sana mambo ya waganga waganga, kwa hivyo alikuwa anawajua
waganga wengi. Hata katika biashara yangu ya genge, alishanipeleka kwa
waganga kadhaa kwa ajili ya kupata dawa ya mvuto wa bishara yangu..
Nilipo mfuata Pamela, akaniambia kuna mganga mmoja, ni mkali sana wa
mambo ya mapenzi.. Mi mwenyewe nina mpango wa kumtafuta lakini najipanga
kwanza kwa sababu bei zake ni kubwa.
Pamela akasema alimfahamu mganga huyo alipokuwa katika kijiji cha
Mwalusembe, wilayani Mkuranga.. Siku hiyo kuna fumanizi lilitokea,
mwanaume alikuwa anatembea na mke wa mtu, kumbe huyo mwanamke alikuwa
amewekewa tego, huyo mwanaume alipo muingilia mwanamke huyo, wakawa
wamenasana.. Baadae ikatafutwa namba ya simu ya mume wa mwanamke. Mume
alipofika kufumania, akakuta mke wake amenasana na mgoni wake.. Akaitwa
huyo Mganga kwa sababu ndie aliye weka hilo tego, alipofika eneo la
tukio alifanya uganga wake, wale wagoni wakawa wameachana.. Tukio hilo
lilivuta watu wengi sana.. Kwa hiyo Pamela anasema, alimjulia mganga
huyu kwenye tukio hilo... Akafanikiwa kutafuta na kupata namba zake.
Pamela akanipa namba za simu za mganga huyo, nilivyo mpiugia akasema
yupo Handeni kikazi ila baada ya siku tatu atakuwa Bagamoyo ambapo
atakaa hapo kwa mwezi mzima aki agua watu wenye matatizo mbalimbali.
Kweli baada ya siku ya tatu, nikaenda hadi Bagamoyo kuonana na huyo
mganga ambaye jina lake tu ni kufuru kubwa kwa Mungu.,. Yeye anajiita
MUNGU WA KABILI ambayo tafsiri yake ni MUNGU WA PILI. Lakini pia
nilishangaa kumuona mganga mwenyewe anaokena bado kijana ambaye sidhani
kama ana fikisha miaka arobaini.
NAANZA KWA KUPIMWA MWILI WANGU KICHAWI
Mungu wa Kabili akasema kabla, hajaanza kazi ya ‘kumtengeneza’ K ,
inabidi aanze kwanza kuuangalia mwili wangu ili ajue kama ni msafi ama
mchafu.
Basi nikapewa dawa nimeze, halafu nikaambiwa Yule kuku mweusi ambaye
nilienda nae mwenyewe, nimshike kichwani. Baada ya hapo, Dokta Mungu wa
Kabili akaanza kuongea maneno yake ya kiganga huku akiwa ameshikilia
chungu chenye dawa iliyo katika mfumo wa maji maji.. Alifanya hivyo kwa
muda wa kama dakika kumi na tano hivi. Alipomaliza kufanya uganga wake,
akaniambia nimtue Yule kuku mweusi niliekuwa nimembeba kichwani. Nilipo
mtua nikashangaa kumuona kuku Yule amekufa. Niliogopa sana .
Basi Mungu wa Kabili, akaniambia mwili wangu ni mchafu sana. Roho ya
mauti imepandwa kwenye mwili wangu. Hivyo lazima anisafishe kwanza,
kutoa uchafu ulio pandikizwa mwilini wangu kichawi. Baada ya hapo ndio
tutaendelea na zoezi la kumfanyia ulozi K.
Mungu wa Kabili akaniambia niende nyumbani, nirudi siku inayo fuata
jioni ya saa kumi na mbili nikiwa na sarafu 350 za shilingi mia mbili
mbili ambazo jumla yake ni Shilingi Elfu Sabini, mchanga wa njia panda
saba, pamoja na wembe tatu..
NASAFISHWA MWILI WANGU KICHAWI.
Ilipo fika saa sita kamili za usiku, mimi , Dokta Mungu Wa Kabili pamoja
na msaidizi wake, tukaongozona hadi njia panda. Njia panda hiyo ipo
huko huko Bagamoyo porini..
Tulibeba, kigoda, chungu , vifaa nilivyo kuja navyo ( mchanga, wa njia
panda saba, sarafu 350, pamoja na asali nusu lita ), mawe matatu,
mishumaa ya rangi nyekundu, mkaa, pamoja na dawa nyingine zilizokuwa
kwenye vibuyu kama saba hivi.
Tulipofika eneo la njia panda, Mungu wa Kabili, alizungushia dawa
kuzunguka eneo tulipoweka vitu vyetu, akamuagiza msaidizi wake, awashe
mishumaa ambayo idadi yake ilikuwa kumi na nne, mishumaa hiyo iliwekwa
kuzunguka eneo tulilokuwa sisi. Baada ya hapo, ukawasha moto, kwenye
mafiga kisha chungu kikatengwa pale, nikaweka vitu vyangu vyote nilivyo
kuja navyo, na yeye Mungu wa Kabili, akachanganya dawa zake anazo zijua
mwenyewe…
Baada ya kama dakika arobaini hivi, zile dawa zikawa zimecheka, nikapewa
kibuyu nikaambiwa nikoge kwa kuchota maji ya kwenye chungu huku chungu
kikiwa kinachemka. Nikafanya kama nilivyo elekezwa huku mganga akiwa
anaongea vitu vyake vya kiganga ambavyo sikuweza kuvielewa..
Nilipomaliza kuoga, mganga akanichanja karibu mwili mzima, kisha
nikapakwa hiyo asali. Baada ya hapo, tukarejea kilingeni . Mungu wa
Kabili akaniambia nipumzike, ikifika saa kumi na moja alfajiri niamke
kwa ajili ya kupikwa. Akasema zoezi la kwanza lilikuwa kunisafisha na
kuniosha kwanza, ambalo limeshakamilika, kinacho fuatia ni kupikwa.
NAPIKWA KICHAWI…
Ilipofika alfajiri nilidamka, kama nilivyo agizwa na mganga kwa ajili ya
zoezi la kupikwa kichawi.. Nikaelekezwa kuingia katika chumba maalumu
ambako kulikuwa na chungu kikubwa. Ndani ya chungu hicho yaliwekwa maji
ya baharini, majani ya mti unaitwa muosha fedha ama mfedha mfedha,
majani ya mkaratusi pamoja na majani ya mti unaitwa mkuyu, halafu ndani
yake zikawekwa sarafu zilizoisha kutumika muda wake, pamoja na dawa
nyingine kama tano hivi ambazo sikuambiwa ni dawa gani…
Baada ya hapo, nikaambiwa nikatwe nywele zangu, pamoja na kucha zangu.
Baada ya kukatwa nywele zangu, vitu vyote hivyo vikachukuliwa vikafungwa
kwenye kitambaa chekundu, ndani ya kitambaa hicho zikaongezwa dawa
nyingine , halafu vikawekwa kwenye chungu kwa ajili ya kupikwa.
Katika chungu hicho pia vikawekwa visu saba, vikiwa vimesimama. Baada ya
kama dakika kumi na tano hivi, mganga akamwambia msaidizi wake, ‘ hebu
ongeza chumvi humo ‘. Nikatarajia kuona itakuwa chumvi ya kawaida ninayo
ijua mimi, ila nikashangaa kuona kinawekwa kipande cha mti..
Baadae nilikuja kugundua kuwa, katika uganga na uchawi kuna kitu
kinaitwa ‘Chumvi ya Kichawi” kazi ya chumvi ya kichawi ni kuukoleza
uchawi ama kukoleza nguvu ya dawa.
Mganga aliniambia vitu vyangu yaani nywele pamoja na kucha
vinaniwakilisha mimi, kwa hiyo kupikwa kwa vitu vyangu kunamaanisha mimi
ndio nimepikwa. Baada ya dawa kupikwa, nikapewa maji yale na kuelekezwa
kwenda kuoga. Nikaambiwa nikimaliza kuoga niende nikapumzike kwenye
chumba change hadi nitakapo pewa maelekezo mengine.
NAFANYIWA TAMBIKO LA JUA .
Ilipo fika saa sita mchana, nikapewa dawa Fulani ya kujipaka, halafu
nikapelekwa kwenye eneo la juani, ambalo chini kuna mchanga. Hairuhusiwi
kuwa katika eneo hilo ukiwa na viatu. Baada ya kukaa katika eneo hilo
kwa kama dakika arobaini hivi , mganga alianza kufanya uganga wake pale
huku akitamka maneno yake ya kiganga. Baada ya hapo, akanifuata
akanikabidhi kibuyu mkononi na kuniambia nikishike kwa mikono yangu yote
miwili kisha nizungumz nizungumze maneno yafuatayo :
“ EWE JUA! MIMI NA WEWE, TU KITU KIMOJA SASA! WEWE NI MIMI NA MIMI NI WEWE. HAKUNA MTU YOYOTE YULE AWEZAE KUTUTENGANISHA.
EWE JUA!TANGU UANZE KUWEPO, HAUJAWAHI KUISHIA NJIANI.
VIVYO HIVYO, MIMI PIA, SITO ISHIA NJIANI. NITAFANYA MAMBO YANGU YOTE,
NITAISHI MIAKA YANGU YOTE KWA KADRI MWENYEZI MUNGU ALIVYO NIKADIRIA ,
WALA HAKUNA MTU YOYOTE YULE ATAKAE WEZA KUNIZUIA, KWA CHOCHOTE KILE
NITAKACHO TAKA KUKIFANYA…
KAMA WEWE JUA UMEWAHI KUISHIA NJIANI, BASI MIMI PIA, NITAISHIA NJIANI.
NA KAMA KUNA MTU ANAWEZA KUKUZUIA WEWE JUA, BASI MIMI PIA NAWEZA
KUZUILIKA. LAKINI KWA KUWA WEWE JUA HAUJAWAHI KUISHIA NJIANI, MIMI PIA,
SINTOISHIA NJIANI. NA KWA KUWA HAKUNA MTU YOYOTE ANAYE WEZA KUKUZUIA
WEWE JUA, BASI MIMI PIA, HAKUNA MTU YOYOTE ATAKAE WEZA KUNIZUA…
Niliagizwa kutamka maneno haya mara arobaini. Kila nilipo maliza
kutamka, nilinyweshwa dawa na mganga, kutoka kwenye kibuyu alicho kuwa
nacho…
Baada ya zoezi hili kukamilika tulirejea kilingeni ili lianze zoezi la ‘ kumtengeneza’ K, mume wa mtu mwenye pesa.
NAPEWA DAWA ZA KUMTEGA “K”
Tulipo rudi kilingeni, Mungu wa Kabili akaniambia nimpe majina yangu
kamili pamoja na jina la huyo mwanaume ninae mtaka. Nikafanya kama
alivyo niambia. Akayachukua yale majina, akaandika andika vitu vyake
ambavyo sikuvijua vizuri, baada ya hapo akachukua kioo chake, akawa
anatazama kwenye hicho kioo, kisha akachukua dawa kutoka kwenye kibuyu,
akaweka kwenye chungu ambacho ndani yake kulikuwa na maji…. Baada ya
kama dakika kumi na tano hivi, akaniangalia halafu akacheka sana..
Akaniambia niweke kiganja changu kwenye kile chungu nikafanya hivyo..
Basi akachukua dawa kutoka kwenye vibuyu vitatu, ambazo alizifunga
kwenye vitambaa vitatu tofauti kila kitambaa na dawa yake, kisha akanipa
dawa hizo na kunipa maelekezo yafuatayo : Dawa ya kwanza, utakunywa na
maji ya kawaida, dawa ya pili, utaifunga kwenye mto unao lalia, halafu
dawa ya tatu utaiweka chini ya kitanda chako.
Ndani ya siku mbili hizi, kuna kitu utakiona ukiwa umelala usiku.
Kitakujia katika ndoto. Kitu hicho kina uhusiano na mwanaume unaye
mtaka. Uki kiona kitu hicho tu, basi haraka sana nipigie simu
nikuelekeze kitu cha kufanya.. Nikazichukua hizo dawa na kufanya kama
nilivyo elekezwa.
NAMUONA “ K” KWENYE NDOTO.
Siku ya kwanza sikuona chochote, ila usiku wa siku ya pili, nikiwa
nimelala usiku, niliijiwa na ndoto ya ajabu . Katika ndoto hiyo,
nilimuona K akiwa anatembea kuja mahali kilipo kibanda changu cha genge.
Alipofika kwenye kibanda changu alisimama na kuniulizia kama nina
hiriki. Kabla sijamjibu, ndoto ikakatika ghafla… Nilipo stuka na
kutazama saa ilikuwa majira ya saa sita na ushee usiku.
Hapo hapo nikampigia simu Mungu wa Kabili na kumueleza nilicho kiona
ndotoni… Akaniambia vizuri sana, kisha akaniuliza, je hilo eneo ambalo
umemuona huyo mwanaume akiwa anatembea, unalifahamu. Nikamjibu ndio
nalifahamu. Akaniambia, kesho saa kumi na mbili alfajiri, nenda kamwagie
ile dawa niliyo kwambia uitunze chini ya kitanda. Baada ya hapo
akaninisisitizia, “ Ukiisha fanya nae mapenzi, uje unione haraka
iwezekanavyo, tufanye dawa za kumfunga..
Nikafanya kama alivyo nielekeza, alfajiri ya saa kumi na mbili,
nikadamkia katika eneo hilo, kisha nikamwaga ile dawa halafu baada ya
hapo nikarudi zangu nyumbani kujiandaa na kufungua genge langu.
NAINGIA KATIKA UHUSIANO WA KIMAPENZI NA “K” MUME WA MTU.
Saa mbili asubuhi nilifungua genge langu, nakumbuka siku hiyo ilikuwa
Jumamosi. Mida ya kama saa nne hivi, K alikuja hadi gengeni kwangu na
kununua vitu mbalimbali vya genge, kama vile karoti, nazi,pilipili manga
nakadhalika na kurudi kwake.
Baada ya kama masaa mawili hivi, K alirejea tena pale gengeni kwangu, na
kuchukua vitu vingine zaidi, halafu akaomba namba yangu ya simu, aka
save namba yangu na mimi nikachukua yake, kisha akaondoka zake.
Baada ya kama nusu saa hivi, K akaanza kunitumia meseji za kunisifu.
Alianza kwa kuniambia mimi ni mwanamke mchapakazi, najituma sana , nna
hasira na maisha , nnafaa kuwa mama kwa sababu hata mume akifa anakuwa
na uhakika watoto wake anawaacha na mwanaume imara.. Mwisho wa siku
akanitongoza, na mimi sikulazia damu. Kesho yake, mimi na K tukakutana
kimwili kwenye hoteli moja iliyopo maeneo ya Mbezi Beach.
Siku hiyo K akaniambia niachane na kazi ninayo ifanya, atanitafutia
biashara nzuri ya kufanya, pia nihame pale nilipo kuwa nakaa,
atanipangia nyumba inayo endana na hadhi yake.
NAPEWA DAWA ZA KUMPUMBAZA MUME WA MTU.
Mungu wa Kabili aliniambia, nikisha fanya mapenzi na huyo mwanaume,
niende kwake ili anipe dawa za kumpumbaza. Nilipofika akaniambia, vitu
vinavyo hitajika katika kutengeneza hiyo dawa ya kumpumbaza huyo
mwanaume, ni NYWELE ZA MWANAUME MWENDAWAZIMU, NYWELE ZA MWANAUME ASIYE
SIKIA ( KIZIWI ) , NYWELE ZA MWANAUME KIPOFU AU FIMBO ILIYO TUMIWA NA
MWANAUME KIPOFU, KAMBA ILIYO TUMIKA KUMFUNGA KONDOO , pamoja na UCHAFU
WA JALALANI.
Vitu vyote hivyo vilitafutwa vikapatikana, vikachanganywa na dawa
nyingine za kichawi,kisha vikatumika kutengeneza uchawi. Nikaambiwa
nitamuwekea kwenye maji ya kuoga na nyingine nitamuwekea kwenye chakula .
Halafu nikapewa na kibuyu, ndani ya kibuyu kile kulikuwa na kipande cha
nyama. Mganga akaniambia hiyo ni nyama ya ndege wa usiku mwana wa jinni,
ambayo baadae nilikuja kujua kuwa ni Bundi wa Kichawi, ambae ni tofauti
na bundi wa kawaida.
Mganga akaniambia utapika nyama, katika nyama utakayo pika ambayo
utamuwekea ndumba, mwanaume wako, utachanganya na nyama hiyo, pamoja na
kucha zako, na nywele zako za siri.
Nilipo rudi nyumbani, nikafanya kama nilivyo elekezwa.
Baada ya kufanya uchawi huu, K alikuwa kama mwendawazimu kwangu,
hakusikia wala kuambiwa na mtu yoyote Yule. Akawa anafanya kila ninacho
taka akifanye mimi. Akaanza kuwa ananipa mali zake, magari, viwanja,
nyumba, biashara pamoja na miradi yake..
NATEGA UCHAWI WA KUTOA MIMBA YA MKE MWENZANGU.
Mapenzi yangu na K yalipamba moto, nyumba aliyo nipangishia haikuwa
mbali sana na mahali alipokuwa anaishi yeye na mkewe, wao walikuwa
wanaishi Tabata Mawenzi, mimi akanipangia nyumba nzima Tabata Kimanga.
K alihama kwa mke wake, akawa anaishi nyumbani kwangu. Taarifa za K
kuishi na “mchepuko” zilimfikia mke wake, lakini hakuwa na kitu cha
kufanya kwa sababu K alikuwa ndio anamuweka mjini yeye na familia yake
na mwanamke alikuwa mama wa nyumbani tu.
Mara nyingi K alikuwa ananishauri amfukuze mke wake, ili nikaishi nae
kwenye nyumba yake, ili kuninonyesha kuwa ananipenda sana na mimi ndio
kila kitu kwake.
Ila kuna kitu kimoja, alinifundisha Mungu wa Kabili, kwamba unapokuwa
mchawi, unatakiwa uwe mnafiki. Usiache kabisa watu wajue kwamba una
jambo Fulani kwa sababu ya uchawi . Hivyo nikawa najifanya kama namuonea
huruma mke wa K lakini moyoni nilikuwa nataka afukuzwe mimi nikakae,
pale.
Kuna kitu kimoja kilikuwa kinaniumiza moyo. Mke wa K alikuwa na ujauzito
wa kama miezi mitano hivi. Sikutaka mwanamke huyo azae na K kwa sababu
nilijua, angezaa na K mtoto angekuwa kiunganishi kwao, Mimi nilitaka K
akisha achana na mke wake, basi iwe ndio moja kwa moja na kusiwe na
chochote cha kuwaunganisha. Hivyo nikaanza kupanga njama za kuharibu
ujauzito wa mke wa K kwa kutumia uchawi.
Suala hili nikalifikisha kwa Mungu Wa Kabili. Mungu wa Kabili akaniambia
nitakupa dawa utaenda kutega kwenye mlango wake. Mti huo ni wa ajabu
sana. Jina lake linafanana na jina la moja kati ya wilaya zilizopo
kusini mwa Tanzania bara.
Baada ya kupewa dawa hiyo, nikafanya ujanja nikaenda kuitega kwenye
mlango anaoutumia kupita. Alipo ruka mimba ikatoka. Kutoka kwa mimba ya
mke wa K kulinipa sababu ya kurudi kwa mganga kwa ajili ya
kuwatenganisha kabisa K na mke wake. Nilijua, majirani wangesema K
kamuacha mke wake kwa sababu mke ana matatizo ya uzazi.
NAMTENGANISHA K NA MKE WAKE.
Nikarudi kwa mganga ili tufanye uchawi wa kumtenganisha K na mke wake.
Mganga alichukua nyoya la ndege ambaye simfahamu jina lake, pamoja na
dawa ambazo sikuzijua pia, akachukua majina ya K na mke wake, akaenda
kuchoma jalalani.
Alipomaliza hapo, tukaenda kaburini, kwa ajili ya kuuzika rasmi uhusiano
wa K na mke wake. Baada ya kuzika uhusiano wa K na mkewe, yalifanyika
matanga kwa ajili ya kuomboleza “kifo’ cha ndoa ya K. Mganga alisema,
kitu kilicho kufa, kinastahili kupewa maziko ya heshima. Usipofanya
hivyo, roho ya kitu hicho itakusumbueni.
Niliporudi mjini nikakuta mke wa K kaondoka kwake, kahamia kwa dada
yake. Mimi nikahamia moja kwa moja kwa K nyumba niliyokuwa nimepangiwa
Kimanga nikamuweka mdogo wangu wa kiume.
NAANZA KUFUATILIWA NA NDUGU WA MKE WA ‘K’.
Ndugu wa mke wa K hawakufurahishwa na kuachana kwa K na mkewe, hivyo
wakafanya kila juhudi kuwapatanisha, lakini msimamo wa K ulikuwa ni ule
ule, kwamba hataki tena kuwa na mke wake na ameamua kuishi na mwanamke
mwingine ambae ni mimi. K alikataa hata kushiriki kwenye vikao vya
usuluhishi. Ndugu wote wa upande wake na upande wa mke wake wakawa
wamemsusia K.
Watu wawili hawakutaka kukubaliana na matokeo. Nao ni baba wa mke wa K,
pamoja na kaka mkubwa wa mke wa K. Watu hawa waligundua kilichotokea
kati ya K na mke wake sio hali ya kawaida bali ni nguvu za ushirikina.
Hivyo wakaamua kutafuta suluhisho kwa waganga. Walipo zunguka kwa
waganga, hawakufanikiwa, hadi wakakata tamaa kunidhuru kwa njia ya
uchawi.
Mwisho wa siku wakaamua, kunikodia majambazi, waje wanipige risasi.
Walijua mimi ndio kikwazo kwa mtoto wao kurudiana na mume wake, hivyo
njia pekee ikawa ni kifo tu.
Nilisurika kuuwawa na majambazi zaidi ya mara saba. Wakati huo Mungu wa
Kabili alikuwa Lubumbashi nchini Kongo kwa shughuli zake. Alipo rejea
nikamfuata kwa ajili ya kuomba ulinzi wake.
Kuna mnyama mmoja wa mwituni, ana ndimi mbili, yani ulimi wake una ndimi
mbili, Mungu wa Kabili akatafuta ulimi wa mnyama huyo, mavi ya chatu
pamoja na dawa zingine anazo zijua, lengo lake likiwa ni kuwatenganisha
na kuwafarakanisha baba na kaka wa mke wa K ili wasipate nafasi ya kukaa
pamoja na kunifuatilia.
Halafu baada ya hapo, akaagiza nipeleke mchanga wa kwenye kaburi la mtu
aliyepita duniani bila kuonekana, ili anitengenezee dawa ya kuwafunga
adui zangu wasinione. Pamoja na hivyo, akanipa hirizi iliyo tengenezwa
kwa Mti Mkuu wa Wachawi.
Katika ulimwengu wa wachawi, mtoto aliye kufa akiwa tumboni kwa mama ake. Huitwa mtu aliyepita duniani bila kuonekana.
Nilivyo mpelekea udongo wa kwenye kaburi la mtu aliye pita duniani bila
kuonekana, mganga akauchukua akafanya ulozi wake, halafu tukaenda wote
hadi mtoni, akaenda akatega ndumba zake, pale, kesho yake tukakuta chura
amenasa pale.
Wachawi wana amini, roho za watoto wanao kufa kabla hawajazaliwa, huwa
zinaenda kuishi mtoni kama Chura. Lakini sio chura wote wapo hivyo, ni
baadhi. Waganga wana utaalamu wao wa kujua chura yupi anahusika hapo.
Basi kaka na baba wa mke wa K, walikosana kwa ugomvi mkubwa, kiasi mtoto
akawa anamtukana baba ake mzazi tusi la mama. Na kuhusu vitisho vya
majambazi havikutokea tena
NATUMIA UCHAWI KUOKOA UHUSIANO WA KAKA ANGU.
Kaka angu ambaye nimempita miaka mitano, alikuwa anaishi kwenye nyumba
ambayo K alinipangia. Nyumba hii ilikuwa maeneo ya Tabata Kimanga. Kaka
angu alikuwa katika uhusiano wa kimapenzi na mwanamke ambaye alikuwa Baa
Medi kwenye bar inaitwa Mawenzi Garden.
Alimuachisha kazi ya ubaa medi baada ya mimi kumuwezesha kiuchumi
kutokana na hela na mali nilizo hongwa na K pamoja na kumpa mradi mmoja
wa K ausimamie. Mdogo wangu alimpenda sana mwanamke huyo .
Ila tatizo moja la mwanamke huyo, alikuwa na tabia ya umalaya. Umalaya ulikuwa kwenye damu yake .
Basi siku moja mdogo wangu alikuja kwangu kunishitakia kuhusu tabia ya
wifi yangu. Mdogo wangu alikuwa anampenda sana mwanamke huyo, na alikuwa
hawezi kumuacha kwa sababu yoyote ile, ila alikuwa anamuumiza sana kwa
sababu ya tabia yake ya umalaya.
“ Ninampa kila kitu huyu mwanamke, ninampa hela, nimemfungulia biashara,
nimempa gari, nawasomesha wazazi wake na kusaidia familia yake,. Lakini
haridhiki tu, mwisho wa siku anatumia hela ninazo mpa kuhonga wanaume
wengine.. ( HELA , GARI NA VITU VYOT AMBAVYO MDOGO WANGU ALIKUWA AKIMPA
WIFI YANGU, VILIKUWA MALI YA K ALIZO CHUMA KWA JASHO LAKE NA MKE WAKE)
Nilimuonea huruma sana mdogo wangu, na nikaamini sio akili yake ila
atakuwa amerogwa na mwanamke Yule. ( UNAJUA UKIWA MSHIRIKINA, KILA KITU
UNAKUWA UNAAMINI KIMESABABISHWA NA USHIRIKINA )
Nikamwambia mdogo wangu usijali, kesho nitakwenda Bagamoyo kwa mtaalamu
wangu, nitamuelezea tatizo lako, halafu nitamsikia atakacho niambia,
nitakujulisha, ila usijali kama mwanamke huyo amekufanyia mambo ya
Kiswahili, itajulikana tu na utakuwa huru.
Nilipo fika kwa Mungu wa Kabili, nikamueleza kila kitu, akaniomba majina
ya mdogo wangu pamoja na jina la huyo wifi yangu, akatazama kwenye
radar zake, halafu akacheka sana.
Mungu wa Kabili akaniambia, hakuna haja ya kumfunga mwanamke huyu. Huyu
mwanamke ana sumbuliwa na damu ya umalaya. Umalaya upo kwenye damu yake.
Hata tukimfunga kwa mdogo wako, tutakuwa tunajisumbua tu, atampenda
sana mdogo wako, lakini atatoka nje tu kwa wanaume wengine. Hapa cha
msingi, afanyiwe dawa ya kumfanya aache umalaya.
Mungu wa Kabili akachukua dawa moja inaitwa GEGEZI. Hii Gegezi ina ukubwa kama tunda linaitwa DADANSI na ina mibamiba.
Halafu akachukua dawa nyingine ambayo ni chakula cha ndege mmoja wa
porini. Ndege huyo simkumbuki jina lake, ila ni mweusi, ana mdomo mrefu,
ndege huyu akilia, vinyonga wote waliopo katika eneo hilo wanakimbia,
huwa anakula vinyonga pia.,
Sasa ndege huyu huwa anakula majani ya mti Fulani wa porini ambao
nimeusahau jina lake, hayo majani ndio ambayo Mungu wa Kabili aliya
chukua.
Kitu kingine akachukua majani Fulani hivi, hayo majani ndio majani pekee
yanayo liwa na mnyama wa porini ambae chakula chake kikuu ni nyama.
Pamoja na dawa hizo akachanganya na dawa zake nyingine ambazo sikuweza
kujua ni dawa gani, halafu akaagizwa itafutwe minyoo ipatayo saba. Vito
vyote hivyo vikaunguzwa pamoja kwenye chungu, hadi vikawa unga unga
halafu vikachanganywa na mafuta ambayo sikujua ni mafuta ya kitu gani.
Mungu wa Kabili akanipa dawa hiyo akaniambia mpelekee kaka ako. Mwambie
akiwa anafanya mapenzi na huyo mwanamke wake, afanye ujanja wake,
achovye kidole chake kwenye hiyo dawa halafu akichomeke kwenye uke wa
mwanamke huyo.
Tangu siku hiyo, mwanamke huyo hatokuwa Malaya tena . Nikafanya kama
alivyo nielekeza na tangu mdogo wangu afanye hivyo, sikuwahi kumsikia
tena akinipa kesi za wifi yangu, zaidi ya kumsifia mpenzi wake ametulia.
Mwisho wa siku walifunga ndoa na kuzaa watoto.
NAMTEKA KICHAWI KIJANA WA KIARABU.
Nilimroga K kwa sababu ya pesa zake. Nikiwa kama mwanamke kamili,
nilihitaji kuwa na mwanaume ninaye mpenda kutoka moyoni mwangu. Nataka
nitoe funzo moja kwa wanaume, mnajua kila mwanamke alie olewa ambae
hajaokoka huwa ana wanaume wawili. Mwanaume wa kwanza ni mwanaume ambae
yupo nae katika ndoa, na mwanaume wa pili ni mwanaume ambae alitamani
awe nae katika ndoa. Hivyo ndivyo ilivyo kuwa kwangu.
Sasa basi, kuna kijana mmoja wa kiarabu ambae nilikuwa namzidi umri kwa
miaka minane. Kijana huyu aliishi mtaa wa pili kutoka nyumba niliyo kuwa
nikiishi na K.
Nilitokea kumpenda sana kijana huyo lakini sikuwa na namna ya kumuanza,
mnajua mwanamke kumtongoza mwanaume sio kazi rahisi. Nikaona isiwe tabu
nikaamua kwenda kwa Mungu wa Kabili, ili anipe ndumba za kumnasa kijana
huyo ambae kwa jina aliitwa Feisal.
Nilipo fika kwa Mungu wa Kabili akaniambia “ Inaonekana wewe ni mtundu
mtundu sana,. Halafu naona una mambo mengi. Sasa nitakutengenezea
uchawi, ambao utakuwa unautumia mwenyewe kumnasa mwanaume yoyote unae
mtaka. “. Mungu wa Kabili akaniambia, njia hiyo itakuwa bora kuliko mimi
kuwa naenda kumuona kila mara kwa jambo lile lile.
Mungu wa Kabili akaniambia, nitafute kopo linalo tumika chooni, nitafute
nguo za marehemu. Hapa simaanishi nguo za maiti, la hasha nina maanisha
nguo za marehemu.
Mfano wake ni kwenu kuna mtu amefariki, nguo zake zimegawiwa kwa ndugu, jamaa na marafiki, sasa nguo hizo ndio anazo zitaka.
Mungu wa Kabili, akaniambia niwe na uhakika kwamba nguo nilizo pewa ni
nguo za marehemu kweli, hilo la kwanza, lakini pili niwe na uhakika
kwamba marehemu huyo alikufa kifo cha Mungu na sio kachukuliwa msukule.
Nikamuuliza nitajuaje kuhusu mambo hayo, akaniambia ni rahisi sana. Wewe
ukizipata nguo za marehemu, au mtu atakae kuuzia nguo za marehemu, basi
akuonyeshe mahali lilipo kaburi la marehemu, halafu utakuja kwangu
nikuelekeze cha kufanya.
( KATIKA ULIMWENGU WA WACHAWI, NGUO ZA MAREHEMU NI BIASHARA KUBWA SANA,
KUNA WATU WANAISHI KWA KUFANYA BIASHARA YA KUUZA NGUO ZA MAREHEMU
MBALIMBALI..MIMI MWENYEWE NILIUZIWA NGUO ZA MAREHEMU KWA BEI MBAYA ).
Baada ya kufanikiwa kupata nguo za marehemu, pamoja na kuonyeshwa mahali
lilipo kaburi la huyo marehemu, nilirejea kwa Mungu wa Kabili.
Mungu wa Kabili alizichukua zile nguo, akakata kipande kidogo kwenye
shati moja, akapaka mafuta ambayo sikujua ni mafuta ya nini, akazifunga
kwenye kitambaa chekundu, akaweza kwenye kibuyu, ndani ya kibuyu hicho
akaweka yai la kuku mweusi, sindano saba pamoja na mafuta mengine ambayo
sikujua ni mafuta ya nini ila wao wachawi na waganga wanayaita mafuta
ya usiku, kisha akakifunga kile kibuyu, halafu akanikabidhi, akaniambia,
ikifika usiku wa saa moja , nenda hadi kwenye hilo kaburi, kisha
ukiweke kibuyu hicho juu ya hilo kaburi kwa kukilaza., halafu asubuhi
pita katika kaburi hilo uangalie kwa makini kibuyu hicho, ukikikuta bado
kimelala kama ulivyo kiacha basi ujue huyo marehemu kweli amekufa kifo
cha Mungu, lakini ukikuta kimesimama, basi marehemu huyo bado yupo hapa
hapa duniani, amechukuliwa msukule.
Nikafanya kama alivyo niagiza, na kweli kesho yake nikakuta kibuyu
kimelala kama nilivyo kiweka. Mungu wa Kabili akaniambia nguo hizo
zinafaa kwa ajili ya kutengeneza dawa hiyo.
Basi akachukua hizo nguo, akaziunguza kwenye chungu cheusi pamoja na
dawa nyingine kama aina kumi na mbili, halafu akazihifadhi kwenye kibuyu
na kunikabidhi, pamoja dawa zingine kwenye vifuko vitatu.
Akaniambia, ukimtaka mwanaume yoyote Yule, utamuita kwa kutumia dawa
hii… Mwanaume utakae muita sauti yako ataisikia na kuitii mara moja kama
ambavyo marehemu huyo alivyoitwa na Mungu na kuitii sauti yake.
Mungu wa Kabili akaniambia huo ni uchawi mkubwa sana katika mapenzi,
hakuna mwanaume nitakae muita na akakataa kuitika. Uchawi huu hautumiki
katika mapenzi tu, hata kama mambo mengine, ilimradi unacho taka wewe ni
kumuita mtu.
Kitu kingine akaniambia, ukimuita mwanaume kwa kutumia uchawi huu zaidi
ya mara saba, halafu akakataa kuitika, basi jua kwamba mwanaume huyo
kinga yake ni kubwa sana.
Sasa basi ukisha ligundua hilo, unatakiwa kutuma nyoka wa kichawi kuua
kinga ya mwanaume huyo. Ukisha ua hiyo kinga, muite tena mwanaume huyo
na atakuja haraka sana.
Nyoka huyu sio nyoka wa kawaida kama nyoka wengine. Ni nyoka wa kichawi.
Ni jinni. Mungu wa Kabili akanikalisha kwenye kigoda na kuniambia, “
Nitamtengeneza nyoka huyu, halafu nitakukabidhi, umtunze vizuri kwa
kufuata masharti yake…”
Katika kumtengeneza nyoka wa kichawi, Mungu wa Kabili akachukua kitovu
cha mtoto. ( KUWENI MAKINI SANA NA MAHALI MNAPOVITUPA VITOVU VYA WATOTO
WENU.. KATIKA ULIMWENGU WA WACHAWI VITUVO VYA WATOTO NI BIASHARA KUBWA
SANA… KITOVU CHA MTOTO KINAPOENDA KUTUPWA, AMA KUFUKIWA, KATIKA WATU
WANAO PEWA JUKUMU LA KUVITUPA, HUWA KUNA MMOJA WAPO ANAWEZA KUWA SIO
MUAMINIFU, HUENDA KUFUKUA MAHALI KILIPOFUKIWA NA KWENDA KUKIUZA KWA
WACHAWI NA WAGANGA )
Alipochukua hicho kitovu, akakifunga kwenye mti wa mnyonyo, halafu
akanyunyizia dawa kutoka kwenye vichupa kama saba. Baada ya hapo
akachukua uzi mwekundu, akafunga vifundo saba kwenye kamba hiyo, halafu
akatupa kwenda chini, ilipotua tu, ikageuka kuwa nyoka. Akamshika huyo
nyoka, akamuhifadhi kwenye kibuyu cheusi, chenye shanga juu, akafunga na
kitambaa cheusi na kunikabidhi.. Akanielekeza jinsi ya kumtuma nyoka
huyo kufanya kazi mbalimbali pamoja na masharti yake.
Kuhusu lile kopo la chooni, Mungu wa Kabili akaniambia amelitumia
kutengeneza dawa ya kujua siri za watu. Dawa hiyo itanisaidia kujua kama
mwanaume niliye nae ana hela au hana hela, ana mke au hana mke. Ana
watoto au hana watoto.
Kingine akanikabidhi ua ambalo natakiwa kulipanda nyumbani. Kupitia ua
hilo nitakuwa ninajua kama mwanaume ambae nipo nae amepata hela au la.
Kitu cha mwisho, akaniambia, kwa sababu nnaonekana nnapenda sana
wanaume, inabidi anipe dawa ya kuwatengeneza wanaume nitakao kuwa nao na
kuwafanya kutokuwa na uwezo wa kufanya mapenzi na wanawake wengine
isipokuwa mimi tu. Hii itasaidia kuniepusha na magonjwa kama vile ukimwi
nakadhalika.
Mungu wa Kabili akanipa mti mmoja mrefu, akaniambia katika mti huo,
utatumia zaafarani nyekundu au ya njano, kuandika majina ya wanaume wote
ambao upo nao kimapenzi pamoja na jina lako, ukisfanya hivyo, nenda
kautegeshee barabarani, ukishagongwa na gari tu, basi wanaume hao
watakuwa wakikutana na wanawake wengine, uume wao unakuwa haufanyi kazi.
Nilivyo rudi nyumbani nikafanya kama nilivyo elekezwa na kweli Yule
kijana alikuja mara moja tangu nilipo muita. Nilifurahi sana kumpata
Feisal. Pamoja na kwamba nilikuwa nimemuita kichawi ila nilikuwa
namuheshimu sana kwa sababu nilikuwa nampenda toka moyoni mwangu.
Baada ya kama wiki mbili tangu nianzee uhusiano wangu na Feisal,
nikagundua Feisal ana tatizo la ukosefu wa nguvu za kiume. Uwezo wake
kitandani ulikuwa mdogo sana.
Kama kawaida yangu nikaenda kumuona Mungu wa Kabili. Mungu wa Kabili
akanipa dawa moja inaitwa KISHINDO. Akaniambia utakuwa unachemsha unampa
anakunywa glasi moja asubuhi na nyingine anakunywa jioni, kwa siku kumi
mfululizo. Nikafanya kama alivyo nielekeza. Baada ya kumpa Feisal dawa
hiyo, nilijilaumu kwanini nilifanya hivyo. Uwezo wake kitandani ulikuwa
wa ajabu, alikuwa anashiriki tendo kwa muda mrefu sana na alikuwa
akirudia mara nyingi bila kuchoka…
NAMFANYIA VITUKO K
Katika muda wote huo, nilikuwa bado ninaishi na K kwenye nyumba yake ya
Tabata Mawenzi. K alikuwa kama Ndondocha kwangu. Kwanza nilikuwa simpi
unyumba na nilikuwa nafanya kila kitu ninacho taka kukifanya tena mbele
yake.
Feisal alikuwa anakuja nalala nae chumbani, K analala pepe yake kwenye
chumba kingine. Alikuwa anafanya kazi zote kama vile kufua, kufanya
usafi na kila aina ya kazi ambayo houseboy anatakiwa kuifanya.
Na katika kipindi hiki K alikuwa ameshafukuzwa kazi kutokana na uzembe
kazini. Mimi mwenyewe nilimpiga marufuku kwenda kazini kwa mwezi mmoja,
nilimwambia achague kitu kimoja kati ya kwenda kazini au kufanya kazi
zangu.
Sasa basi nikawa namfanyia K vituko, lengo langu nikitaka aondoke
mwenyewe aniachie nyumba na mali zake. Hakuwa na faida yoyote tena
kwangu. Kazi ameshafukuzwa , mali zake zote pamoja na biashara zake
ninazimiliki mimi.
Basi kila nilipokuwa nikifanya mapenzi na Feisal nikawa napiga kelele
ili kumuudhi K. Na hivi Feisal alikuwa anatumia muda mrefu basi na
kelele zangu zikawa za muda mrefu. Lakini wapi, K wala hata hakuonyesha
dalili ya kwamba anaweza kuondoka , undondocha ulikuwa umetamalaki
kwenye kichwa chake.
Kwa kutumia ndumba hizo nilizo pewa na Mungu Wa Kabili, niliwateka kichawi wanaume wengi na kuvunja ndoa nyingi sana.
K ANAAMUA KURUDI KIJIJINI
Nilipoona K hana dalili ya kuondoka pamoja na kumfanyia vituko lukuki,
nikaona niende kwa Mungu wa Kabili ili kama kuna uwezekano wa kumfukuza K
kichawi.
Nilipofika kwa Mungu wa Kabili, akafanya dawa zake, halafu ikatengenezwa
ngalawa ndogo, nikaambiwa nipeleke nguo yoyote ya K . Nguo ya K
ikafanyiwa uchawi halafu ikafungwa kwenye hiyo ngalawa, tukaenda
baharini kutegea wakati bahari imesafiri tukaenda kuiweka ngalawa , maji
yalipokuja yakaondoka na hiyo ngalawa, kesho yake tu, K mwenyewe
akasema anataka kwenda kusalimia kijijini kwao amepakumbuka. Nilifurahi
sana niliposikia hivyo, nikamfungia nguo zake, nikampa na nauli pamoja
na hela ya kula njiani..
Kalivyo rudi kwao, baadhi ya ndugu zake hawakuridhishwa na hali ya K
pamoja na maelezo yake. Mtu aliyekuwa tegemeo la ukoo mzima, ghafla
anarudi kijijini akiwa hana kitu na maelezo yake yanatatanisha. Wakaamua
kufunga safari hadi mjini ili kufuatilia mali za ndugu yao. Nilipo pata
taarifa zao, nikaenda kuwashitaki kwa Mungu wa kabili, wote
walipeperuka na sikusikia chochote kuhusu watu hao.
NAINGILIA NDOA YA WALOKOLE.
Nilitokea kumtamani mwanaume mmoja mlokole alieishi mtaa wa pili kutokea
nilipokuwa naishi. Huyu nilimpenda kama nilivyo mpenda Feisal. Alikuwa
mkaka mzuri anae jipenda sana. Kwa jina aliitwa Erasto. Kikwazo kikubwa
kwa Erasto ilikuwa, kwanza alikuwa ameokoka na pili alikuwa na mke
ambaye alikuwa ameokoka pia. Mke wa Erasto alikuwa na ujauzito mkubwa tu
wa kama miezi mitano au sita .
Nasema kuokoka ilikuwa kikwazo kwa sababu Mungu wa Kabili Alisha
nishauri niwe makini sana na walokole kwa sababu wana nguvu za ajabu.
Ila akaniambia kuna walokole wa waina mbili., mlokole wa ukweli na
mlokole feki. ..
Hivyo basi kama umemempenda mwanaume wa kilokole, unatakiwa kwanza
umpime kichawi kujua kama ni mlokole wa ukweli ama mlokole feki.
Akaniambia uchawi unao tumika kupima nguvu ya mlokole, sio uchawi wa
kitoto, hauwezi kufanywa na mtu yoyote, akaniambia kama itatokea
nimempenda mwanaume wa kilokole, basi niende kwake halafu yeye atampima
kama mlokole huyo ni orijino au feki.. Kama ni orijino una achana nae
kwanza unatafuta njia nyingine ya kumpata, lakini kama ni feki,unamvuta
kama watu wengine.
Akaniambia, ukimpenda mwanaume wa kilokole orijino ni bora utumie njia
za kawaida kumteka, kuliko njia za kichawi, kwa sababu kwa njia za
kawaida, ataishia kukukemea tu,. Lakini kwa njia ya uchawi, utapigwa
shot. Hakuniambia ni shoti gani.
TUNATUMIA UCHAWI KUPIMA ULOKOLE WA ERASTO.
Ili kujua kama mlokole ni orijino au feki, wachawi hutumia nzi. Hivyo
basi Mungu wa Kabili alianza kufanya uchawi ili kupima kama Erasto ana
nguvu za Mungu au hana nguvu za Mungu.
Siku hiyo Mungu wa Kabili akachukua bakora ya kichawi ambayo
imetengenezwa kwa mti wa Mkomoro, Mganga akaniambia mti huo wa mkomoro
ni mti wenye nguvu nyingi sana za kichawi na wachawi huutumia kwa mambo
mengi ikiwa ni pamoja na kufufua wafu.
Mungu wa Kabili akaanza kwa kuwaita inzi na kisha kuwatuma waende kwa
Erasto ili kujua kama ana nguvu za Mungu au la. Lilikuja kundi la nzi
wengi, na walipo tua tu kwenye fimbo yake wote wakapasuka pale pale.
Mungu wa Kabili akaniambia kwa kunisisitiza, achana kwanza na huyu
Erasto, kesho ninasafiri kwenda Mkuranga , nitakuwa huko kwa siku saba
tunaenda kupika uganga . Nitakapo rudi tutaangalia njia nyingine ya
kumteka Erasto.
Waganga na wachawi huwa wanakuwaga na MWAKA WA UCHAWI ama MWAKA WA
UGANGA, kama ambavyo kuna MWAKA WA FEDHA, MWAKA WA MASOMO nakadhalika.
Unapofika mwaka wa uganga, waganga hukutana mzimuni na kupika uchawi,
ambao huuzwa kwa waganga mbalimbali. Jambo hilo hufanyika kila mwaka.
Mungu wa Kabili alikuwa anaelekea Mkuranga kwa ajili ya kusimamia zoezi
la upikaji wa uchawi unaoitwa MANGUBE. Kwa hiyo Mungu wa Kabili
akaniambia nisubiri kwanza mpaka wiki mbili zipite ndio tuje tukae
tupange cha kufanya juu ya Erasto, kwa sababu baada ya kutoka Mkuranga
alikuwa anaelekea Liwale Lindi.
Sikuwa na jinsi zaidi ya kukubaliana na maagizo ya Mungu wa Kabili.
NAMTUMIA ERASTO NYOKA WA KICHAWI.
Baada ya siku tatu uvumilivu ukanishinda, nikaamua liwalo na liwe, kama kuna baya litanitokea, Mungu wa Kabili atanisaidia.
Usiku wa saa sita siku hiyo, nikamchomea Erasto, dawa ya kumvuta kwangu
kichawi. Kwa kawaida nikishachoma dawa, usiku huwa naota nafanya mapenzi
na mwanaume nilie mchomea dawa na kesho yake, kabla ya saa sita
mwanaume huyo huwa ananitafuta, lakini kwa Erasto ikawa tofauti. Sikuona
chochote. Nikachoma kwa siku saba mfululizo hakuna chochote.
Nikakumbuka Mungu wa Kabili aliniambiaga kwamba, kama nikichoma dawa ya
kumuita mtu na mtu huyo asije, basi nijue kuwa mtu huyo ana kinga kubwa,
kwa hiyo natakiwa nimtumie nyoka wa kichawi, nyoka huyo ataenda kuvunja
kinga ya mtu huyo.
Siku hiyo usiku wa saa sita, nikaenda kuchukua kile kibuyu ambacho
kilitumika kumuhifadhi Yule nyoka, nikamtuma nyoka huyo aende kuigonga
na kuivunja kinga ya Erasto. Nilipomaliza kunena maneno yangu nikafungua
kile kibuyu ili nyoka atoke, nyoka alipotoka akanigonga kwenye mguu na
kutokomea.
Nilipiga kelele za ajabu, house girl wangu akaenda kuwaamsha majirani na
kupiga simu ya kaka angu, nikapelekwa hospitali, hospitali nikapimwa
lakini hakikuonekana kitu, wala haikuonekana kama nina sumu yoyote
mwilini, lakini nilikuwa nasikia maumivu makali sana yaliyokuwa yanakuja
na kuondoka, nikapewa dawa za kuzuia maumivu lakini wapi. Ilipofika
asubuhi maumivu yakawa yameisha lakini nikawa nimepooza upande mmoja.
Nikamwambia kaka angu apige simu ya Mungu wa Kabili, lakini Mungu wa
Kabili alipopigiwa na kuelezewa kilicho tokea, akawa mkali sana, kwanza
akasema alinionya nisifanye chochote halafu pili akasema hawezi
kunisaidia kwa namna yoyote ile.
Sikuwa na jinsi zaidi ya kumueleza kaka angu ukweli. Kilicho fuatia
tukaanza kuzunguka kwa waganga wa kienyeji kwa ajili ya tiba yangu
lakini wapi. Baada ya wiki mbili nilipelekwa kwa Mungu wa Kabili
Bagamoyo angalu aione hali yangu ilivyo labda anaweza kunionea huruma
lakini, akakataa kata kata…. Msimamo wake ulikuwa ni ule ule, nimefanya
jambo ambalo alinikataza kulifanya na pia hana uwezo wa kunisaidia.
Zaidi aliniambia hatima yangu ni kifo.
Tulizunguka kwa waganga wa kila aina na kila sehemu lakini wapi hali yangu ikazidi kuwa mbaya.
Siku moja ndugu yangu mmoja wa upande wa mama angu, alikuja kuniona
baada ya kusikia nimepooza. Baada ya kumsimulia kuhusu kisa changu
alisikitika sana. Nikapelekwa kwenye kanisa moja la kiroho na kuombewa.
Siku tatu tangu nianze kuombewa nilitapika vitu vingi sana vya ajabu
ajabu, kama vile kucha, nywele, damu nakadhalika, na taratibu hali yangu
ikaanza kutengemaa na hatimaye nikapona kabisa.
Namshukuru Mungu sasa hivi nimeokoka, nimempokea Yesu kama Bwana na
Mwokozi wa maisha yangu. Mali za K nimezirudisha na sasa ninaishi maisha
yangu halali kwenye chumba cha kupanga maeneo ya Mbezi Ya Kimara.
Ninaumia sana moyoni kuona, nimeseababisha mateso kwa wanawake wenzangu,
nimevunja ndoa za watu. Nimeamua kumtumikia Mungu katika maisha yangu
yote. Ninawaomba msamaha wale wote nilio waharibia maisha.
CHA MWISHO NA KIKUBWA.. NAWATAHADHARISHA WANAWAKE WENZANGU KUHUSU WAGANGA WA KIENYEJI
Monday, June 11, 2018
Ushuhuda: Nilimlisha Mume wa Mtu Limbwata la Nyama ya Bundi
About Anonymous
Soratemplates is a blogger resources site is a provider of high quality blogger template with premium looking layout and robust design. The main mission of templatesyard is to provide the best quality blogger templates.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment