RAIA mmoja wa Afrika Kusini na mchumba wake kutoka nchini Ukraine
wametiwa mbaroni nchini Falme za Kiarabu kwa kufanya mapenzi kabla ya
ndoa, ndugu amebainisha.
Emlyn Culverwell, 29, na Iryna Nohai, 27, waliripotiwa kukamatwa baada
ya daktari kugundua kwamba Nohai, ambaye alikuwa na maumivu ya tumbo,
alikuwa na ujauzito.
Walikamatwa kwa kufanya mapenzi nje ya ndoa, jambo ambalo ni kinyume cha sheria nchini humo.
Mama wa Culverwell ameomba waachiwe huru, kwa kusema “kitu pekee walichofanya kibaya ni kupendana.”
Wizara ya mambo ya nje ya Afrika Kusini ilisema kwamba haitoweza
kuwasaidia wapenzi hao kwa kuwa ni suala la ndani la sheria za Falme za
Kiarabu, mtandao wa News24 uliripoti.
Serikali ya Afrika Kusini imewashauri wapenzi hao kutafuta msaada wa kisehria, mwandishi wa BBC huko Johannesburg anasema.
Hadi sasa hakuna maelezo yoyote kutoka serikali ya Falme za Kiarabu.
Culverwell na Nohai wanaripotiwa kuwa wanashikiliwa tangu mwezi Januari
mwaka huu, lakini taarifa juu ya kushikiliwa kwao zimeanza kujulikana
sasa.
Culverwell amekuwa anafanya kazi nchini Falme za Kiarabu kwa miaka mitano sasa.
Mama yake Linda aliuambia mtandao wa News24 kwamba familia yake
inajaribu “kupeleka ujumbe kwa wawili hao na kuwaambia kuwa inawapenda
na kwamba hawapaswi kuwa na wasiwasi.”
Wapenzi hao bado hawajafunguliwa mashtaka kwa kuwa mamlaka nchini humo bado wanawafanyia uchunguzi wa kiafya.
Iwapo watakutwa na hatia, wanaweza kukabiliwa na kifungo cha muda mrefu.
FacebookTwitterGoogle+WhatsAppPinterestShare
No comments:
Post a Comment