TUNAISHI kwenye ulimwengu
unaoenda kasi sana kiasi kwamba usipokuwa makini, unaweza kujikuta
ukimpoteza mtu uliyempenda sana maishani kwa sababu tu ya kujua namna ya
kwenda naye sawa wakati ukiendelea na mchakamchaka wa kukimbizana na
maisha!
Inafahamika kwamba mapenzi ni
hisia lakini ni wachache wanaoweza kueleza jinsi ya kufanya hisia za
mapenzi ziendelee kuwa hai. Siku hizi ndoa nyingi zinaendelea kuwepo kwa
sababu ya kudra tu, unakuta mume na mke wanaishi kwa sababu ya mazoea
tu lakini si kwa sababu ya mapenzi!
Wengine wanakwambia kabisa,
‘mapenzi yalikuwa wakati tunaanzana’! Wanaishi tu ilimradi siku
zinaenda, ilimradi wanawalea watoto lakini si kwa sababu ya upendo kati
yao.
Wengine wanafikia hatua hata ya
kulala mzungu wa nne au kutengana vyumba kabisa! Kwa nje mnawaona kama
wanapendana lakini kumbe ndani kuna ufa mkubwa kati yao, hakuna tena
mapenzi kati yao.
Cha ajabu, utakuta watu hawahawa
ambao leo wanaishi kimazoea, wakati wanaanzana walikuwa wakioneshana
mapenzi motomoto! Walikuwa wakigandana kama ruba, walikuwa wakioneshana
kila aina ya bashasha za kimapenzi.
Ukiuliza nini kimetokea? Hakuna
mwenye majibu, maudhi ya mara kwa mara yamekuwa kitu cha kawaida kwao,
usaliti, kutoheshimiana na kujibizana hovyo kumewafikisha hapo walipo,
hakuna tena mapenzi, Wazungu wanasema No More Love!
Hata pale inapotokea maelewano
yakapatikana, mnapokutana faragha, hakuna tena msisimko kama zamani, kwa
wanaume wanaanza kupatwa na tatizo lingine la kupungukiwa na nguvu za
kiume wakati wanawake wao wanapoteza kabisa hamu ya tendo.
Utafiti wa kisayansi, unaonesha
kwamba mwanaume anapokosa hisia, dalili zinazoonekana kwa haraka ni
ukosefu wa nguvu za kiume! Lakini cha kushangaza, mwanaume huyu ambaye
mkewe anamlalamikia kwamba hamtoshelezi kwenye tendo, ikitokea amepata
mchepuko, huko nje ‘anapafomu’ kwa kiwango cha juu kabisa, akirudi ndani
mambo ni yaleyale.
Mwanamke pia anayepoteza hamu ya tendo kwa mumewe, ambaye
hafurahii tena kuwa faragha na
mumewe, ikitokea amekutana na mchepuko huko nje, utashangaa analifurahia
mno tendo na pengine ‘akafika’ kwa urahisi kabisa, akirudi ndani mambo
ni yaleyale.
Kwa maelezo haya, ni dhahiri
kwamba unaona umuhimu wa hisia katika mapenzi! Ili mapenzi yawe matamu,
ili uhusiano udumu, ni lazima kila mmoja awe na hisia na mwenzake. Hata
hivyo, hisia haziji tu zenyewe, zinajengwa!
Hisia za mapenzi ni kama bustani
ya maua, haiwezi kustawi wala maua hayawezi kuchanua na kutoa harufu
nzuri kama huitunzi bustani yako KILA SIKU! Hisia za mapenzi siyo kitu
cha kuja na kupita, unatakiwa ushughulike na hisia za mwenzi wako kila
siku.
Hatua ya kwanza kabisa
unayotakiwa kuifanya, unapoona unaishi kwenye maisha ambayo hisia za
mapenzi kati yako na mwenzi wako hazipo tena, ni kuanza kujiweka karibu
na mwenzi wako.
Kama hukuwa na mazoea ya kuwahi
kurudi nyumbani, au ukiwa nyumbani unakuwa bize na mambo mengine,
badilisha utaratibu, anza kutenga muda wa kutosha wa kukaa naye karibu
na kuwa mnyenyekevu kwake!
Siyo unawahi kurudi nyumbani
halafu muda wote mna kazi ya kubishana na kulumbana! Jifanye mjinga,
jishushe na muoneshe kwamba unampenda! Hata kama alikuwa na dukuduku
lake moyoni, litaanza kupungua, ataanza kuzungumza na wewe, ataanza
kukuchangamkia na hapo utakuwa umefanikiwa kuanza safari ya kuziamsha
upya hisia zake.
Tafuta muda wa kutoka naye ‘out’,
mpeleke maeneo mliyozoea kwenda kipindi mapenzi yenu yalipokuwa
motomoto, taratibu hisia zitakuwa zinaendelea kuongezeka kidogokidogo.

No comments:
Post a Comment