Habari
rafiki na mpenzi msomaji wa Amka Mtanzania? Na karibu tena katika
makala yetu ya leo ili tuweze kujifunza. Katika makala yetu ya leo
tutajifunza njaa zinazowasumbua wanandoa katika maisha yao ya ndoa.
Kuzifahamu njaa zinazowasumbua wanandoa tafadhali twende sanjari mpaka
mwisho wa makala hii.
Kumekuwa
na mitazamo hasi sana juu ya maisha ya ndoa. Kabla mtu hajaingia ndani
ya maisha ya ndoa tayari akili yake imeshajazwa mitazamo hasi juu ya
maisha ya ndoa. Mtu aliyepatwa na matatizo katika maisha yake ya ndoa
naye atakwenda kuwaaminisha watu juu ya matatizo yake juu ya ndoa. Siyo
kwamba katika maisha ya ndoa hakuna changamoto la hasha zipo kama
kawaida kama vile kwenye kazi, biashara, ujasiriamali nakadhalika. Hivyo
kwenye jambo lolote changamoto haziepukiki. Kweli itakuweka huru na
usipoujua ukweli utapata shida sana.
Maisha
ya ndoa unayotaka kuishi unayatengeneza wewe mwenyewe na si vinginevyo
hivyo usipoteze muda wa kuhangaika tengeneza yale maisha ambayo
unayataka kuishi na usisikilize kelele za watu ambazo zitakuwekea ukungu
katika macho yako na kushindwa kuona mbele. Na waswahili wanasema
ukiona vyaelea ujue vimeundwa kwa hiyo, hata wewe unaweza kuviunda
katika maisha yako ya ndoa. Katika
hali ya kawaida hakuna mtu asiyeijua njaa, mtu akiwa na njaa anapoteza
kabisa nguvu na hata ufanisi wa kazi aliyokuwa anafanya unapotea, kwa
hiyo njaa huwa inalegeza watu kama akikosa kula chakula na kushiba.
Vivyo hivyo, kila mwanandoa ana njaa yake yaani mwanaume ana njaa yake
katika maisha ya ndoa hali kadhalika kwa mwanamke naye ana njaa yake.
Kwa maana hiyo, kila mwanandoa anahitaji ashibishwe njaa yake na mwenza
wake.
Ikitokea
sasa wanandoa hao yaani wawili hao kutoshibishana njaa zao ndio
matatizo huanzia hapo. Na tunajua ya kwamba wawili hao kila mmoja ana
njaa yake. Hivi ikitokea mtu ana njaa ya chakula halafu pale
anapotegemea kupata chakula ili ashibishe njaa yake hapati ataendelea
kusubiri kubaki na njaa yake? Jibu ni kwamba lazima atatafuta sehemu
ambayo ataweza kupata chakula ili aweze kushibisha njaa yake.
Ndugu
msomaji, kama kila mwanandoa ameshindwa kumshibisha mwenzake basi ujue
lazima atatafuta chakula sehemu nyingine ili kuweza kukidhi njaa yake.
Hivyo basi, kumbe ni wajibu wa kila mwanandoa kuhakikisha anamshibisha
mwenzake njaa yake. Zifuatazo ni njaa mbili zinazowasumbua wanandoa endapo hawatashibishana; 1. Njaa ya mwanamke ni upendo; Mwanamke
anahitaji upendo kuliko vitu vingine, hata katika vitabu vya dini
vinasema; enyi waume, wapendeni wake zenu. Ampendaye mkewe hujipenda
mwenyewe, mwanaume anatakiwa kujitoa kwelikweli kumpenda mke wake kama
tunavyojua upendo ndio falsafa kubwa sana katika maisha ya binadamu,
upendo huvumilia, hufadhili, hauhusudu. Hivyo basi njaa ya mwanamke ni
kupendwa. Wewe kama mwanaume unatakiwa kumpenda mke wako kwa moyo wako
wote bila kujali udhaifu wake. Hii ndio njaa ya wanawake wanahitaji
upendo katika maisha ya ndoa. 2. Njaa ya mwanaume ni kuheshimiwa; Mwanaume
njaa yake kubwa ni kuheshimiwa katika maisha ya ndoa. Sasa ikitokea
mwanaume anakosa kuheshimiwa na mke wake katika maisha ya ndoa hivyo
anakuwa amekosa kushibishwa njaa yake. Na kama akikosa kushiba ndio
matatizo huanzia hapo itamlazimu kutafuta kushibishwa njaa yake nje.
Hivyo kama wewe ni mwanamke unatakiwa kumshibisha mume wako njaa yake ya
kumtii. Kama
wanandoa wanashindwa kushibishana njaa zao, hivyo wanajitengenezea
shimo wao wenyewe. Watu wanajisahau sana katika kutimiza majukumu yao
katika maisha ya ndoa hatimaye wanaruhusu haki za kibinadamu kuingia
maisha ya ndoa, kama wanandoa mkishaingiza haki za kibinadamu katika
maisha ya ndoa yaani hamsini kwa hamsini kama wanavyodai lazima
mtapoteza mwelekeo tu. Kwa hiyo kila mtu ana njaa yake kama tulivyoona
hapo juu sasa mkishayaingiza mambo haya ya kidunia mtakosa kushibishana
njaa zenu.
No comments:
Post a Comment