Kama nilivyoanza mwanzo....usisome kama una machozi ya karibu...
“Nilipofika nyumbani usiku ule, mke wangu aliponitayarishia chakula,
nilimshika mkono na kumwambia, Kuna kitu nataka nikwambie. Mke wangu
alikaa chini na kula chakula kimya akiwa tayari kunisikiliza. Tena
nikagundua macho yake yalionyesha anaumizwa.
Nilishindwa hata namna ya kuanza kufumbua kinywa changu. Lakini ilibidi nimwambie ili ajue nilikuwa nikifikiri nini juu yake.
Nataka kukupa talaka. Nilianza kusema kwa utulivu. Alionekana kutokereka
na maneno yangu badala yake aliniuliza kwa sauti ya upole ‘kwa nini?’
Sikumjibu swali lake. Kutojibu kulimfanya akasirike. Akatupa kijiko na
akanikaripia, ‘wewe si mwanamume!’ Usiku ule, hakukuwa na maongezi kati
yetu. Alikuwa akilia kwa kwikwi.
Nilifahamu kwamba alitaka kujua ni nini kimetokea kwenye ndoa yetu.
Lakini kwa hakika nisingeweza kumpa jibu wala sababu ya kuridhisha;
alionekana si mali kitu kwangu penzi langu lilihamia kwa Mary.
Sikumpenda tena mke wangu mawazo yote yalikuwa kwa Mary.
Kwa kweli nilimdharau mke wangu!
Huku moyo wangu ukijua wazi kwamba nafanya kosa, niliandika talaka
ambayo ilionyesha kwamba yeye (mke wangu) angepata nyumba yetu, gari na
atakuwa na hisa 30% ya kampuni yetu.
Aliangalia talaka ile na kuichana vipande vipande.
Mke ambaye tumeishi nami kwa miaka 10 alionekana mgeni machoni mwangu.
Nilimuonea huruma kwa muda, rasilimali na nguvu alizopoteza lakini
sikuweza kurudi nyuma kwa sababu Mary aliuteka moyo wangu kisawasawa.
Hatimaye mke wangu alilia kwa sauti mbele yangu, jambo ambalo kwa hakika nilitarajia. Kwangu mimi kilio chake kilinipa nafuu.
Wazo la kuachana na mke wangu limenisumbua kwa majuma kadhaa na sasa limeendelea kuimarika na kuwa jambo la hakika zaidi.
Siku iliyofuata nilikuja nyumbani kwa kuchelewa sana nikakuta mke wangu
akiandika jambo mezani. Sikutamani hata kula chakula alichonipikia
nilikwenda moja kwa moja chumbani na usingizi ulinichukua mara moja kwa
sababu nilikuwa nimechoka baada ya kula raha za kufa mtu na Mary
Usiku nilishtuka usingizini mke wangu alikuwa bado akiandika.
Sikujali kabisa nikajifunika vyema shuka na kulala tena. Asubuhi yake
alinikabidhi masharti ya talaka yake: hakutaka kitu chochote kutoka
kwangu lakini alihitaji apate angalau mwezi mmoja wa kujiandaa kabla
hajaachika. Akaomba kwamba katika kipindi hicho cha mwezi mmoja sote
mimi na yeye tujitahidi kuishi maisha ya upendo au kawaida kwa kadiri
itakavyowezekana.
Sababu yake ilikuwa ndogo lakini muhimu: mwanetu wa kiume alikuwa
akikaribia kufanya mtihani katika mwezi uliofuata kwa hiyo hakupenda
mtoto aathirike kisaikolojia kwa sababu ya kuachana kwetu. Hili halikuwa
tatizo kwangu, nilikubali mpango wake. Lakini alikuwa na sharti la
ziada, aliniomba nikumbuke jinsi nilivyombeba siku za fungate yetu hasa
siku ya harusi yetu.
Akaniomba na kunisihi kwamba katika kipindi hicho cha mwezi mmoja niwe
nambeba kutoka kitandani kwetu mpaka mlango wa kutokea kila asubuhi.
Nilidhani anakaribia kuwa kichaa. Ili kufanya siku zetu za mwisho zisiwe
na migogoro nilikubaliana na masharti yake ya ajabu.
Nilimsimulia Mary kuhusu masharti ya kuachana na mke wangu. Mary
alicheka sana, aliona ni ujinga. ‘Hata akitumia ujanja wa namna gani
talaka ni lazima’, alisema Mary tena kwa dharau. Mimi na mke wangu
hatukuwahi kugusana tangu nilipomweleza dhamira ya kumtaliki. Kwa hiyo
nilipombeba kwa mara ya kwanza sote tulinuniana. Mwanetu alifurahi sana
na kupiga makofi nyuma yetu, ‘aah baba kambeba mama mikononi mwake’.
Maneno yake yalinichoma moyoni moja kwa moja. Kutoka chumbani kwetu hadi
sebuleni, halafu tena mpaka mlangoni, ni zaidi ya mita kumi nimembeba
mke wangu. Alifumba macho na kusema kwa sauti laini na ya upole;
usimwambie mwanetu juu ya talaka. Nilikubali kwa kichwa, ingawa
nilijisikia vibaya.
Nilimuweka chini nje ya nyumba.
Alienda kituoni kusubiri basi la kazini kwake nami nikaendesha gari
kwenda ofisini kwangu. Siku ya pili, zoezi lilikuwa rahisi kwetu sote.
Aliegemea kifuani pangu. Nilisikia harufu nzuri ya uturi aliofukiza
kwenye blauzi yake. Nikagundua kwamba sijamuangalia kwa makini mke wangu
kwa kipindi kirefu sana. Nikagundua hakuwa binti tena. Kulikuwa na
mikunjo usoni na nywele zake zilianza kuwa nyeupe! Ndoa yetu imekula
urembo wake. Kwa dakika moja nikafikiri kwa nini namfanyia hivi.
Siku ya nne nilipombeba hisia za mapenzi kati yetu zilirejea. Huyu ni
mwanamke aliyejitoa kuishi nami na tumeishi kwa miaka kumi sasa. Siku ya
tano na ya sita ilikuwa wazi kwamba mapenzi yetu yalikuwa yakimea upya.
Sikumwambia Mary kuhusu jambo hili. Kadiri mwezi ulivyokaribia kwisha
niliona raha kumbeba mke wangu na zoezi likawa rahisi zaidi. Pengine
kufanya kazi hii kila siku kuliniimarisha zaidi.
Alikuwa akichagua nini cha kuvaa asubuhi. Alichagua mavazi kadhaa
hakupata linalomfaa. Kisha akaguna, ‘nguo zangu zote zimekuwa kubwa’.
Nikagundua kwamba mke wangu amepungua sana, nadhani ndiyo maana niliweza
kumbeba kirahisi. Ghafla jambo likanichoma... mke wangu ana uchungu na
maumivu makuu moyoni mwake. Bila kujitambua nikamgusa kichwa chake. Mara
mtoto wetu akatokeza na kusema ‘baba ni wakati wa kumbeba mama muende
kazini’. Kwake kumuona baba akimbeba mama likawa ni jambo la furaha
sana. Mke wangu alimuonyesha ishara mwanetu asogee karibu na
akamkumbatia kwa upendo mkuu. Niligeuza uso wangu nisije nikabadili
mawazo katika dakika ya mwisho. Kisha nikambeba mikononi mwangu kutoka
chumbani, sebuleni halafu mpaka mlangoni. Mkono wake laini ulikuwa
umeizunguka shingo yangu kwa upendo. Nilimkumbatia mwili wake; ilikuwa
ni mithili ya siku ya ndoa yetu. Lakini wepesi wake ulinitia mashaka.
Siku ya mwisho nilipombeba nilipata shida hata kupiga hatua moja. Mtoto
wetu alishakwenda shuleni. Nilimshika kwa karibu na kumwambia sikubaini
kwamba maisha yetu yalikosa upendo. Nikaenda zangu ofisini…. Nikashuka
garini hata bila kufunga mlango. Maana nilihisi nikichelewa tu ninaweza
kubadili nilichoamua.... nikapand ngazi. Mary alifungua mlango
nikamwambia, ‘Samahani, Mary, sihitaji tena kumtaliki mke wangu’.
Akaniangalia kwa kustaajabu, halafu akagusa kichwa changu. Akaniuliza
‘Unaumwa?’ Nikaondoa mkono wake kichwani kwangu. ‘Samahani, Mary,
nimesema sitaki kumtaliki mke wangu. Nadhani ndoa yangu haikuwa na
furaha kwa sababu sikuthamini undani wa maisha yetu, mimi na mke wangu,
si kwamba hatupendani. Nimetambua hilo tangu nilipombeba siku ya ndoa
yetu nilitakiwa kumbeba siku zote za maisha yetu, nampenda mke wangu
sitamuacha mpaka kifo kitakapotutenganisha.’
Ikawa kama Mary alizinduka usingizini. Akanizaba kibao cha nguvu,
akajiegemeza mlangoni na kuanza kulia. Nikashuka ngazi na kuondoka
zangu. Nikaingia kwenye duka la maua nikaagiza maua mengi mazuri kwa
ajili ya mke wangu. Muuzaji akaniuliza aandike nini kwenye kadi.
Nikatabasamu na kuandika “Nitakubeba kila asubuhi mke wangu mpaka kifo
kitakapotutenga
nisha”. Jioni ile nilifika nyumbani na maua mikononi mwangu, tabasamu
kubwa usoni nikakimbia mpaka chumbani, nikapokelewa na maiti ya mke
wangu kitandani.
Kumbe mke wangu alikuwa akisumbuliwa na saratani kwa miezi kadhaa nami
nilishindwa kubaini kwa sababu nilihamishia akili yangu kwa Mary. Alijua
kwamba angekufa karibuni na alitaka asiniingize katika chuki na mwanetu
kama ningelazimisha talaka mapema.
Angalau machoni mwa mwanangu naonekana ni mume mwema.
Mungu nisaidie Nisifike huku mimi.
Monday, August 27, 2018
Kama Una Moyo Mwepesi Usisome Stori Hii, Wengi Wamelia Sana
About Anonymous
Soratemplates is a blogger resources site is a provider of high quality blogger template with premium looking layout and robust design. The main mission of templatesyard is to provide the best quality blogger templates.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment