BILA shaka msomaji wangu uko poa, kwa wewe ambaye unasumbuliwa na shida
mbalimbali za kidunia, nakuombea kwa Mungu upate ahueni. Wiki iliyopita
tulianza kujadiliana kuhusu mada hii kama inavyojieleza. Je, wewe
unaamini kwamba kwenye mapenzi kuna uchawi? Unaamini kwamba kuna kitu
kinaitwa limbwata? Je, ni kweli mtu anaweza kwenda kwa mganga na
akafanikiwa kumpumbaza mwenzi wake akili? Nakushukuru wewe uliyetumia
muda wako kunipa majibu ya jinsi unavyoyaelewa mambo haya.
Majibu niliyoyapata yalikuwa katika makundi mawili; wapo waliosema
wanaamini ni kweli kuna uchawi katika mapenzi, wakaenda mbali na kutoa
mifano iliyowatokea au waliyoishuhudia na kuwafanya waamini kwamba kweli
kuna uchawi katika mapenzi. Msomaji wangu mmoja kutoka Unguja,
Zanzibar, alisema anao ushahidi wa jinsi mume wa rafiki yake
alivyoendewa kwa mganga na kimada wake hadi akafikia hatua ya kutelekeza
familia ya mke na watoto watatu, akahamia kwa kimada. Unaambiwa mpaka
leo hasikii haambiwi, ameikana familia yake kisa kimada.
Kundi jingine lilisema haliamini katika uchawi! Kwamba mume kumsaidia
mkewe kuosha vyombo, kufua, kupika, kumpa kila anachokitaka au kutii
kila anachoambiwa, siyo lazima awe amerogwa bali akioneshwa mapenzi ya
dhati, yupo tayari kufanya chochote ilimradi mwenzi wake afurahi! Kwa
wale walionitumia ushuhuda kuhusu limbwata, wengine wakilalamika kwamba
wenzi wao wamebadilishwa mawazo na wanawake au wanaume wa nje mpaka
kufikia hatua ya kuwakana wapenzi wao wa awali kwa sababu ya ndumba,
nataka waelewe kitu kimoja muhimu sana.
Mapenzi ya dhati yana nguvu kuliko hata mauti, vitabu mbalimbali vya
dini vinathibitisha hili. Kwamba, ukimpenda na kumuonesha mapenzi ya
dhati mwenzi wako, naye akakupenda, mkashibana, hakuna nguvu inayoweza
kuingia katikati yenu, iwe uchawi, ndumba au majini na kuwatenganisha.
Hata kama kuna mtu anautazama uhusiano wenu kwa husuda, hata akikesha
kwa waganga kwa lengo la kuwatenganisha ili yeye apate nafasi, ni sawa
na kazi bure! Penzi la dhati lina nguvu asikwambie mtu! Hata hivyo,
mapenzi ya dhati yanapokosekana ndani ya uhusiano, uwe ni uchumba, ndoa
au mahusiano ya kawaida, ni dhahiri kwamba hata vitu vidogovidogo tu,
vinaweza kuwatenganisha mkaishia kusingizia uchawi!
Kama hampendani, mtu anaweza kuingiza maneno ya kuwafitinisha tu,
mkaachana. Kama hampendani kwa dhati, ugomvi mdogo tu, unaweza
kuwatenganisha, kama ni ndoa ikavunjika, kama ni uchumba ukaishia njiani
na mambo ya namna hiyo! Kwa hiyo jambo la msingi, siyo kukimbilia kwa
waganga mambo yanapoharibika ukiamini mwenzi wako amerogwa na mpenzi wa
nje. Unachotakiwa kufanya kuanzia sasa, kabla mambo hayajaharibika, ni
kuhakikisha kila siku iendayo kwa Mungu, unaishi vizuri na mwenzi wako.
Mpende kwa dhati, kuwa mwaminifu, mjali, msamehe anapokosea, mtimizie
mahitaji yake ya msingi na usichoke kumrekebisha kwa njia nzuri ili
mwisho aje kuwa bora!
Mkiishi hivi, hata atokee mchawi kutoka kuzimu, wala hawezi kuvunja ndoa
yenu wala wewe hutahitaji kwenda kwa mganga ili kumroga au kumpumbaza
akili asikuache, mapenzi yako ndiyo yatakayokuwa uchawi tosha. Lakini
ikitokea mkaishi kwa mazoea tu, hakuna mapenzi ya dhati ndani ya nyumba,
kila mmoja anajiona yeye ni bora, kiburi, dharau, usaliti, maudhi,
uongo na kero za namna hiyo zimetawala, uhusiano wenu hauwezi kwenda
popote na ninyi ndiyo mtakuwa wachawi wa penzi lenu.
Hata ukihangaika kwa mitishamba na hirizi, kama humuoneshi mapenzi ya
dhati mwenzi wako, ni kazi bure! Siku akimpata anayemjali na kumuonesha
mapenzi ya dhati, itakula kwako. Ni hayo tu kwa leo, tukutane wiki ijayo
kwa mada nyingine murua.
Sunday, August 26, 2018
Unaamini Kuna Uchawi Katika Mapenzi? Soma Hii Inakuhusu
About Anonymous
Soratemplates is a blogger resources site is a provider of high quality blogger template with premium looking layout and robust design. The main mission of templatesyard is to provide the best quality blogger templates.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment