Makala haya yanasaili namna mtazamo wa awali wa watu wanaoamua kuingia
katika uhusiano wa kimapenzi unavyoweza kuathiri kwa kiasi kikubwa namna
wawili hao watakavyohusiana.
Na tunaonesha namna kiwango cha mapenzi kati yao kinatengemea masuala
matatu makuu; Ukaribu wa kihisia, tamaa ya mwili na maamuzi yao.
Tofauti ya mwanaume na mwanamke katika namna wanavyoyatazama mahusiano
kihisia. Kwa ujumla, tuliona kuwa wakati mwanamke anatarajia kujisikia
ana usalama wa kihisia kwa kupendwa, mwanaume anatarajia kujisikia yu na
usalama wa kimamlaka katika kudhibiti mahusiano. Na kadri kila mmoja
anavyoweza kuyaelewa na kuyajibu mahitaji ya mwenzake kwa usahihi,
ndivyo mawasiliano kati ya wawili hao yanavyoimarika, na hivyo kuboresha
mahusiano yao.
Katika sehemu zinazofuata tutajaribu kusaili masuala kadhaa
yanayochangia kujenga mahusiano yanayowaridhisha wenzi wawili wenye
mahitaji tofauti kama tulivyoona na kisha tutatazama namna hali hiyo ya
kuridhika inavyoweza kuondoka na kusababisha matatizo.
Lakini kabla hatujafika huko, kwa sababu aghalabu kila anayeingia kwenye
mahusiano, hutarajia mapenzi, nimeona ni vyema katika makala haya
tuangalie kwa ufupi dhana ya mapenzi kwa mtazamo wa kisaikolojia ili
kuelewa sababu zinazoweza kusababisha ama mahusiano yawe bora au kinyume
chake.
Nadharia ya mapenzi ya Stenberg
Kwa kutumia nadharia ya Robert Stenberg, mapenzi imara kati ya watu
wawili wanaotaka kuwa pamoja kimahusiano, au walio kwenye mahusiano ni
lazima yawe na pande tatu muhimu zinazotegemeana ili kuendeleza
mahusiano hayo
1) Hisia za mvuto wa kimapenzi ambapo wawili husisimkiana kimwili;
2) ukaribu wa kirafiki ambapo wawili hao hutaka kuwa pamoja muda mwingi na wakati mwingine wakijitenga na wengine; na
3) maamuzi ya kuendeleza uhusiano wao ambapo wawili hao huwekeana ahadi ya kuwa pamoja.
Matatu hayo yakiwepo, kwa mujibu wa Stenberg, basi uwezekano wa uhusiano
huo kudumu hali ukiwa imara huongezeka ingawa katika hali ya kawaida
matatu hayo yote huweza kupungua hapa na pale kutegemea na mazingira ya
kimahusiano, haiba na wakati. Tutarejea hapa baadae.
Kwa kawaida, kinapokosekana kimoja wapo kati ya hivyo vitatu, mahusiano
hayo huchukua sura tofauti tatu kama mchoro unavyoonyesha; mahusiano ya
muda mfupi (msisimko wa kifilamu), mahusiano ya siri yasiyo wazi, na
kisha mahusiano yanayodumu.
Maana yake ni kwamba, zikiwepo hisia za kimapenzi na ukaribu wa kirafiki
lakini yakakosekana maamuzi ya kuendelea kuwa pamoja, Stenberg anasema
uhusiano huo utakuwa wa muda mfupi ambao unaweza kuishia kwenye kukutana
kimwili. Uhusiano wa namna hii ni vigumu kudumu.
Lakini katika mazingira yenye hisia za kimapenzi na maamuzi ya kuwa
pamoja, lakini bila kujisikia kuwa karibu, Stenberg anasema mahusiano
yatakuwa ya siri yasiyo na uhuru unaotarajiwa. Ingawa yanaweza kudumu,
lakini kukosekana kwa ukaribu kunaweza kupunguza msisimko wa mahusiano.
Kwa upande mwingine, Stenberg anasema, inapotokea wawili wakawa na
urafiki, kwa maana ya kuwa karibu, na kisha wakawa na maamuzi ya
kuendeleza urafiki wao, wasipokuwa na hisia za kimapenzi au tamaa, basi,
kinachobaki hapo ni maamuzi yasiyo na mapenzi yanayoeleweka. Ilivyo ni
kwamba wenzi wanaoanza mahusiano kwa uelekeo huu, wanakuwa na uwezo wa
kudumisha uhusiano wao kwa muda mrefu, na kisha kuoana. Lakini katika
ndoa, hali hii ya kukosa hisia za humaanisha kuchokana, na huweza
kutafsiriwa kuwa hatua ya kuelekea kwenye matatizo ya kimahusiano.
Tutaona zaidi mbeleni.
Hatua za mahusiano ya kimapenzi?
Ukifikiri vizuri zaidi pande hizo tatu, yaani, hisia, urafiki na
maamuzi, unaweza kuona zinaweza kuelezea hatua kuu za watu kuingia
kwenye mahusiano ya kimapenzi. Kwamba, mapenzi huanza kwa mmoja kuvutiwa
kimapenzi na mtu mwingine, hali inayosababisha hatua ya kuanza kujenga
ukaribu na huyo unayevutiwa naye. Ikiwa hivyo, hatua hizi mbili hujenga
mahusiano ya karibu yenye msisimko mkubwa ambao hata hivyo hudumu kwa
muda mfupi. Huu ndio msisimko unaofikiriwa na wengi wanapoanza
mahusiano.
Msisimko huo huweza kuwapelekea wawili hao kufanya maamuzi ya kuendeleza
uhusiano wao. Lakini kadri mahusiano yanavyoendelea kuimarika katika
hatua hiyo, ukijumlisha na changamoto za maisha ambazo tutazijadili hapo
mbeleni, basi hutokea hisia zikapungua na hata kutokomea kusikojulikana
na hivyo wawili hao kubaki kuwa marafiki wa kawaida walio kwenye
uhusiano wa kudumu usio na msisimko wa kihisia za kimapenzi.
Vile vile, inaweza kutokea ukaribu wenyewe (intimacy) ukatoweka, na
hivyo wawili hao kujikuta katika mazingira ya kuwa wapenzi walioamua
kuwa pamoja tena wenye msisimko wa kimapenzi lakini wasio na mahusiano
ya karibu. Hali hii, unaweza kuiita mahusiano yanayoegemezwa na ahadi
pekee na woga wa kuvunja maamuzi yaliyokwisha fanyika awali.
Ikitokea, na msisimko nao ukatoweka, kinachobaki hapo ni ahadi, au
maamuzi, ambayo kwa mazingira hayo huendelea kukosa nguvu na hatimaye,
hatua za haraka zisipochukuliwa, huelekea kwenye matatizo ya kutengana
na kadhalika. Tutarejea hoja hii huko mbeleni.
Tunachojifunza...
Kwanza, mtazamo wa awali wa watu wanaoamua kuingia katika uhusiano wa
kimapenzi unaweza kabisa kuathiri kwa kiasi kikubwa namna wawili hao
watakavyohusiana. Na kiwango cha mapenzi kati yao kinatengemea sura hizo
tatu za mapenzi.
Kwa mfano, wapenzi wanaoanzisha mahusiano yao kwa msingi wa ukaribu wa
kirafiki wenye msisimko wa kimapenzi, bila kuwa na maamuzi ya kuendelea
kuwa pamoja, wanakabiliwa na hatari ya kujikuta wanawakiana tamaa za
kimwili, ambazo zinaweza zisiwafikishe mbali kimahusiano.
Ni vizuri basi kuhakikisha kwamba mwanaume na mwanamke, wote kwa pamoja,
wanao uelewa unaoshahibiana katika suala la matarajio yao ya jumla pale
wanapofikiri kuingia kwenye mahusiano na kwamba wanaelewa kwa hakika ni
kona ipi wanaitumia kuingilia kwenye mahusiano yao.
Kadhalika, tunajifunza kwamba mahusiano yetu huathiriwa kwa kiasi
kikubwa na kuwepo au kupotea kwa kimoja wapo kati ya hivyo vitatu, yaani
hisia, ukaribu na uamuzi. Hisia za kimwili pekee yake, hazitoshi
kudumisha mahusiano, ingawa zinaweza kusaidia kuanzisha mahusiano.
Ukaribu unapoungana na hisia unaweza kuwapeleka watu wawili kwenye hatua
ya mahusiano ya kudumu, ingawa hatari yake yaweza kubaki kuwa mahusiano
ya juu juu, lakini yenye msisimko mkubwa.
Kupotea kwa kimoja wapo kati ya hisia na ukaribu, ni hatua mbaya kwa
watu walio kwenye mahusiano ya kudumu, ambao, kwa kufumba na kufumbua
wanaweza kujikuta katika mazingira ya kuparaganyika na hivyo kuongeza
takwimu za kuachana tulizoziona hapa.
No comments:
Post a Comment