Nilikuwa
nikifanya kazi katika kampuni moja ya usafirishaji wa madini kutoka
Tanzania kupeleka Bang kok nchini Thailand. Kampuni yetu ikiwa ya mtu
binafsi na ilikuwa Mkoani Arusha. Mimi Sweedy Kachenje ndiye niliyekuwa idara ya usafirishaji, nikiwa afisa mauzo.
Katika
maisha yangu yote nilitegemea sana na nilihitaji kuwa na mwenzi wa
kuishi naye, kama vile familia nyingine bora ambazo kila siku zina
furaha na ridhaa. Kwa kila mmoja kuwa mwanandani wa mwenzake. Pia
nilimuomba mungu kwa kila hali si kanisani na hata nikiwa katika
mapumziko yangu, anipatie mwanamke ambaye angenifaa katika maisha
yangu.Kila siku palipokucha,niliamka nikiwa na wazo la kumpata
nimpendaye na anipendaye.Niliamini hivyo japo sikuwa na uhakika kama
kweli ningepata mtu kama huyo maishani mwangu.
Siku
zote nilijibidisha kuwa mfano bora ili niweze kupata mchumba, nilikuwa
mtiifu, nikiwa heshimu wenzangu na kushirikiana nao vema kujenga
Taifa.Kujaribu kuwa na marafiki wengi wa jinsia tofauti. Nilijitahidi
nikihisi pengine wale marafiki wangenifaa kumbahatisha wa ubani wangu.
Pamoja na yote hayo sikuweza kubahatika kupata
niliyempenda kutoka moyoni, na aliyenipenda. Nilizidi kumuomba Mungu
anishushie neema ya kumpata wa ubani wangu. Ikafikia wakati nikaomba
ushauri, lakini wale niliowaomba ushauri walionekana kuwa fukara wa
mawazo.Walinishauri wakisema kuoa ni kuoa.Eti mwanamke ningemfunza kama
angekuwa na tabia mbaya.Nikafikiri mara mia mia ushauri wao nikaona
haukuwa na maana zaidi ya upofu.
“Bw.
Kachenje inamaana uwingi wa wanawake ulimwenguni umekosa
umpendaye?”Lilikuwa swali nililoulizwa na rafiki yangu.Hatahivyo
nilishinda kumjibu na hatimaye nikamdharau.
“Inamaana
kuchagua mke wa kuishinae ni sawa na kuokota fungu la samaki sokoni ama
vipi?”Nilijiuliza bila kujijibu kwa wakati huo.
Nilishindwa
kuokota mke ilimradi mke kama vile mtu anavyookota nyanya sokoni na
kulipa pesa, nafikiri hata anayeokota nyanya nae huchagua. Japo kuna
usemi usemao mchagua nazi hupata koroma usemi huo niliupinga na
kuutupilia mbali. Niliamini usemi wa kuoa ni kuoa pengine ningefanya
hivyo basi ndoa yangu isinge kuwa na ladha ya unyumba na isingedumu
maishani.
Nilijawa
na imani kuwa mke mwema hupewa na Mungu, niliishi kwa matumaini ya
Mungu na nilitegemea msaada mkubwa kutoka kwake. Wazazi wangu Mungu
aliwapa baraka walikuwa hai wakinisubiri nioe wamuone mkwe na wajukuu
wao kabla ya kufa. Kwa bahati mbaya sikuweza
kupewa upeo wa kuona mchumba mwema ambaye angekuwa mke wangu, japo
nilikuwa na kazi nzuri na nafasi yangu kazini ilinifanya nionekane
maridadi saa zote.
Watu
wengi walioniona walinishangaa sana, kwani sikuwahi kuonekana na
mwanamke yoyote niliyeongozana naye katika maisha yangu. Si kwamba
nilikuwa na hitilafu yoyote mwilini!. Hapana nilikuwa mwanaume rijali,
na sikupenda kujihusisha na ngono,kwani magonjwa yamezagaa kama inzi
kwenye mzoga.Licha ya magonjwa, ni dhambi kubwa kuzini nje ya
ndoa.Nilitambua kwamba jambo hilo halimfurahishi muumba hata kidogo.Siku
zote nilikuwa nikijilaumu,ikafikia wakati nikitaka kuokota mwanamke
hata baa, moyo ukasita ukinitaka niwe na subira zaidi.Lakini subira gani
huumiza matumbo. Je subira hii itazaa matunda ama nikunizidishia bala
uzeeni?.Nikayatupilia mbali mawazo potofu. Nilihitaji kuwa na subira
nikihisi pengine ningempata atakaye nipenda na mimi kumpenda.
Umri
wangu ulisogea kufikia miaka arobaini. Hali ambayo iliwaogopesha sana
wazazi wangu, waliokuwa wazee wa kujikongoja. Nilizaliwa mtoto pekee wa
kiume na dada zangu watatu.
Wazazi
wangu walichoka na maneno yangu. “Bado umri wa kuona. Nitaoa Mungu
akipenda, mke mwema hupewa na Mungu” Miaka yote huwa nilikuwa najitetea
hivyo .
Ulifika
wakati baba na mama walitaka kuniachia laana baada ya kuwadanganya
zaidi ya miaka kumi toka nipate pesa na kuwajengea nyumba. Walitaka
wawaone wajukuu wao kabla ya kufariki, walijua umri walio kuwa
nao,wasingeishi miaka mitano ama saba mbeleni wangepoteza maisha.
Kwa
kuwaridhisha na kukwepa radhi za wazazi niliwaomba wanitafutie Mke.
Niliamini mke ambaye ningepewa na wazazi angenifaa maishani. “Baba
akimpenda binti, hata mimi sina budi kumpenda” nilijisemea mwenyewe
baada ya kuwapa kazi ya kunichagulia msichana mwenye
sifa zote zile mwanamke anatakiwa kuwa nazo. Ni miongoni mwa nidhamu
kwa mume. Nilikuwa na furaha kidogo, kwani nilijiona niliyejaa Ukungu wa
kutopendwa na kutopenda.
Kwa
ujumla sikujua ilikuwa ni mitihani ya Mungu kwani mimi ni miongoni mwa
vijana waliokuwa wakicheka vijana waliochaguliwa wachumba na wazazi wao,
hakuna kitendo nilichokichukia kama kuchaguliwa msichana na wazazi.
Nilikuwa na imani ya kijana akichaguliwa mke basi hata ndoa ingejaa
migogoro isiyoisha na pengine ikavunjika.
**********
Kampuni
yetu iliitwa JOPHU MINING TRANSPORT CO LTD, mwenye Kampuni yetu,
alijulikana kwa jina la Mzee Jophu Kundy . Ndiye alikuwa Mkurugenzi na
mmiliki wa Kampuni.
Kipindi
cha miaka ya sabini kulikuwa hakuna gonjwa la Ukimwi, kama lilikuwepo
basi ilikuwa halijajulikana kama sasa. Nilikuwa nikienda Nchi Thailand
kila wiki kuuza madini aina ya Tanzanite. Siku zote nilikuwa na urafiki wa karibu na mmiliki wetu Mzee Jophu. Hakuna hata mtu mmoja aliyethubutu kuongea na mzee Jophu aliyeonekana mwenye uso wa ukali saa zote. Haikuwahi kupita siku bila mzee Jophu kuita “Sweedy njoo” nk.Alikuwa kazoea jina langu , pia alinipenda kama mwanae.
Siku
moja niliondoka katika uwanja wa Kia (Kilimanjaro International
Airport) nikielekea Nchini Thailand, Bang kok.Vaaa yangu toshani
kielelezo kwa mtu asiyenifahamu,kusema mimi ni
mtu mwenye pesa za kunifanya niitwe tajiri. Nilivaa suti ya kijivu,chini
nilivalia viatu vya mchongoko,vijana wa sasa huviita ‘Mkuki
moyoni’,mkono wa kushoto nilishikilia ‘breefcase’lililojaa madini ya
Tanzanite.Pia nilivalia miwani ya jua,iliyosababisha vigumu kuona macho
yangu.
Nilikuwa
nimebeba madini gram 5000gm. Sawa sawa na kilo tano Kg 5. Kilo mbili
ilikuwa ni rangi ya blue colour A na kilo tatu (3kg) yalikuwa ni rangi
ya mkojo, kwa wale wakazi wa Mererani wanajua vizuri wakiona na rangi ya
coke ile maji ya kunywa ilikuwa (gm 50).
Ndege
iliacha aridhi ya Tanzania mnamo saa nne unusu asubuhi, ambako
ilichanja mawimbi angani saa mbili na sekunde ya kumi iltua uwanja wa
kimataifa Bang kok.Nilifanikiwa kushuka salama nikiwa mtu wa tano.
Sikuweza kwenda kwenye soko siku hiyo, nilielekea kwenye maegesho ya
gari za kukodi amabako nilikodi gari.
“Halo.kutoka hapa hadi Care lodge ni kiasi gani cha pesa?”
“Dola tano.Karibu”
“Sikuweza
kubishana sana kwani niliamini kauli ya ‘nipunguzie bwana’ ni huku
kwetu.Alinifungulia mlango wa mbele, nilivuta mguu wangu wa kulia na
kuingia ndani mlango wa mbele kulia mwa dereva.Gari hilo lilikuwa ‘Left
hand’.Nilienda moja kwa moja kwenye hoteli iliyoitwa CARE LODRGE .Dereva
alitumia kama dakika nne kuingia lango la hoteli hiyo.Nilipofika,
nilimlipa ujira wake, nikaelekea ofisi za kupokelea wageni(Mapokezi).
Sikutaka kwenda kufanya biashara kwa wakati huo. Niliamua kujipumzisha
kutokana na uchovu wa safari, jambo la kushangaza nilichokiona mbele ya
macho yangu sikuweza kuamini macho yangu kama
yalikuwa sawa sawa ama vipi, nilijaribu kupikicha macho pengine ni ule
ukungu wa kutokuwahi kupenda. Lakini cha ajabu moyo wangu ulisimama kama
sekunde kadhaa, kisha ukaendelea mapigo yake yakawa ya taratibu mno,
ambayo sikuweza hata kuyasikia. Nilihisi jasho jepesi likitiririka,
kwanza nilijitazama kisha nikamtazama mtu huyo, hata hivyo sikuamini kwamba kwa uzuri wake kamwe ningependwa mtu mweusi tena Mtanzania?.
Niliona
mwanadada mmoja aliyekuwa amekaa karibu na muhudumu wa mapokezi katika
hoteli hiyo, msichana huyo alikuwa Mzungu si mzungu, muhindi si muhindi,
mwarabu si mwarabu hata kwenye weusi hakuwepo. Baada ya dakika tano,
nikiwa nimemtumbulia jicho la matamanio, alinisalimia .
“Kaka habari yako”
“Nzuri,
sijui nyie”nilijibu salamu kwa wote,nikiwa bado sijabandua jicho usoni
mwake.Sikushughulika na huyu mwingine,macho yangu tayari yalishapata
chakula.Nilimtizama hamu haikuniisha nikatabani abaki pale pale macho
yangu ya shibe.
“Mimi mzima”aliitikia msichana huyo na aliyefuata ni wamapokezi.
“Hata mimi mzima pia” walinisalimia.
Sikupenda
kukaa na ule mzigo wenye thamani kubwa niliandikisha jina langu na
kuchukua chumba namba kumi.Kila nilipotaka kuondoka kuelekea chumba
nilicholipia ,nilisita na kubakia mdomo wazi,mwili ulibweteka nikitamani
kufahamiana zaidi na mwanadada yule.Niliamua kujilazimiza kuondoka
ingawa nafisi ilitukutika,nilipofungua mlango wangu,niligeuka kumtizama
yule mlimbwendekama vile nikihakikisha kama atakuwa pale.Nilimuona nae
akinitizama.
“Mtoto
mtoto,Duu!.Tembea uone mengi”Niliongea akilini nikiwa nafungua
mlango,katika kuzungusha funguo mlango ukatii sheria ,ukanipa nafasi ya
kuingia.Nilihifadhi Breefcase yangu haraka na kufungua mlango kutoka
nje.Nilikuwa nimeshikilia funguo,nikajikuta nikiziachia bila
kujijua.Yote ni baada ya kumwona yule binti akiwa ametoka chumba
kilichokuwa mkabala na changu.
“Kumbe
chumba nilichochukua kilikuwa karibu na chumba cha Binti yule
niliyesalimiana nae muda mfupi tangu nifike pale.”Nilijisemea moyoni
kiwa nimeacha mdomo wazi ,nikimtizama ,alikuwa kajifunga taulo nyepesi
kabisa.Tayari kwa sasa alikuwa kanipa mgongo,kila alipovuta hatua ,
makalio yake yalitikisikia kama mawimbi ya maji baharini.Miguu yake
minene iliyobeba umbile la wastani lilijivuta kwa madaha.Nilijikuta
nikimtizama hadi alipoishia.
Kwa
kweli nilimpenda na niliamini angenifaa kuwa mwezi wangu na pambo la
ndani. Hata hivyo niliumia moyoni je kama akinikubali nitafanya nini
kama baba na mama watakuwa wamenipatia mchumba wa kumuoa?.Wazo hilo
lilinijia na nikaamua kulitupilia mbali. Lakini ngoja nisiumize kichwa
sijui nitakubaliwa au laa! Kwani nitese nafsi yangu? Nilizidi kuwaza
wakati namalizia kufunga chumba. Pasipo kutegemea mara nambona tena
akiwa kashikilia mafuta ya lotion. Safari hii alikuwa anakuja kwa
mbele,niliweza kufaidi kuisawiri sura yake vema, ilioonyesha umahiri wa
muumba.Tembe yake ungeweza kudhania kachoka vile,lakini hapana ukweli
halisi.Ule ndio mwendo wake halisi,ikafikia hatua nikadhani hakanyagi
chini, kwa jinsi alivyotembea utafikiri anaionea aridhi huruma.
Nikajikuta moyo ukinipasuka “paaa” nikiwa na mshangaa nae alinitolea
tabasamu nono! lililoshamiri usoni mwake.Tena likiwa limeambatana na
mwanya mzuri.Nilishikwa na butwaa kama dakika kadhaa, nikajikuta ubongo
ukifa ganzi. Tulibaki macho pima, hapo nilijua dhahiri kama kunapimana
hivi.Nikajitizama na kumtizama kwa mara ya pili. Mapigo y a moyo
yakaanza kupungua.Hata hivyo nilishindwa kuvumilia yote niliyoyaona kwa
safari hii.
“Samahani dada naweza kujua jina lako”alikuwa kesha nikaribia.
“Yaa!. Jina langu ni Jeniffer John”
“Sawa . Ahsante unajina zuri. Naitwa Sweedy Kachenje” nilijitambulisha nikilamba midomo yangu kuua aibu flani iliyochomoza kama mshale wa sekunde na kupotea.
Tuliongea
mengi na Jeniffer nae hakuwa mvivu wa kujibu maswali na chochote
nilichomuelezea, niliamini ndoto yangu ilitimia, yule mwanamke
niliyempata angeweza kufunika pengo kubwa maishani mwangu. Hata hivyo
katika mazungumzo yetu alinitamkia kwa kinywa chake kuwa nae ananipenda
sana, kuliko hata mimi ninavyompenda. Ni binti aliyeukonga moyo wangu na
kuuteka kila sehemu ya viungo vya mwili wangu, “Kweli subira huvuta
heri” niliongea kimya kimya kwenye mtiririko wa mawazo.
Jennifer
alikuwa ni mchanganyiko wa Mzungu na mwafrika (chotara) na ni msichana
aliyetoka Bara la Africa kama mimi, tofauti ni kwamba yeye alitokea
Africa ya kusini, na mimi nilitokea Tanzania. Wala hakujali Nchi
niliyotoka kuwa ilikuwa ya kimaskini, inamaana alinipenda na umasikini
wangu. Tuliongea na kujikuta mawazo yetu yakiwa sawa, kwa kutaka
kunionyesha upendo alikubali ombi langu la kutaka anisindikize
kuupitisha usiku uliojaa raha za kila aina. Alidiriki kuacha chumba
chake na kuja kulala na mimi, nilimgusia suala la ndoa nalo alilikubali
alikuwa tayari kubadili uraia kuwa Mtanzania. Lakini kama angekuwa
Mtanzania aliyekuwa Afrika ya Kusini umwambie arudi aolewe Tanzania,
angeruka hata futi mia.
Kwa
upande wa mapenzi nilikoga na penzi motomoto, hakuwa mvivu wa
kujishughulisha, tulisaidiana kupitisha usiku huo mwanana uliojaa mahaba
ya kila aina, si mlimani tulipanda vichochoroni tulipita kwa nia imara
ya kumridhisha Jeniffer aliyeonekana mgeni kwenye ulimwengu huo. Asubuhi
kulipopambazuka nilimuaga Jennifer na kuelekea soko la madini ya
Tanzanite, lililoitwa King Life. Kabla ya kuondoka nilimuachia namba ya
simu email address yangu kwa mawasiliano. Na niliamua kufanya hivyo ili
kuwahi na kuwaeleza wazazi habari mpya, wasihangaike kunitafutia mchumba
kwani nilishampata mrembo. Nilifanikiwa kuuza madini yote kwa bei nzuri
na kurudi Tanzania.
No comments:
Post a Comment