Kwa kawaida wasichana hupata mafunzo ya unyago ndani ya nyumba siyo porini. unyago wa wasichana ni mgumu kuuelezea tofauti na ule wa wavulana maana mambo mengi hufanyika na wanawake kwa siri kubwa. Wamakonde wanaamini kuwa kueleza ovyo ovyo mintarafu mafundisho ya unyago kwa wasichana mtu huweza kuandamwa na balaa hivyo basi ni mwiko mkubwa kusema sema hadharani. Kamwe siyo rahisi kumithilisha mafundisho yale wapatayo wavulana na wasichana.Kwa jumla wasichana wanaohusika yawapasa kuvumilia taabu na magumu mengi pindi wawapo katika unyago. Ni marufuku kwa msichana kulia au kulalamika kwa sauti hata kama angeandamwa na maumivu makali namna gani. Hutawishwa kwa muda fulani pengine kwa muda fulani pengine kwa kipindi kirefu hadi ajaliwapo kupata mchumba.Maisha yote toka utoto hadi umri wa kuvunja ungo kwa msichana wa kimakonde hufuata madhehebu ya unyago yajulikanayo kama chiputu.Wamakonde wanaamini kuwa kwa msichana bila kupitia mafunzo ya unyago kwa jinsi ya mila na desturi yao matunda ya ndoa hayangefikia au yasingekuwa mema kwa sababu msichana yeyote asiyepitia unyago huhesabiwa kama mwanamke haramu. Mara nyingi hasa siku hizi wasichana hupata mimba kabla kabisa ya kupatiwa elimu ya unyago. Wanao angukiwa na mkasa kama huo hawapatiwi tena mafunzo ya unyago ambayo ni msingi kabisa wa maisha yao.Hupachikwa jina anahaku popote aendako. Wazazi hushikwa na majuto sana iwapo binti yao ameingia katika mkumbo huu wa akina anahaku.
Anahaku huwa hawana raha maana huwakosa marafiki au huadhiriwa.Mafunzo ya unyago huanza mapema sana hasa kwa watoto walio watundu na watukutu. Wasichana wengine huwa wamekwisha kulumuka mwongo yaani kuvunja ungo kabla ya kuingia kwenye unyago. Hao hutofautishwa na wenzi wao kwa kuwavisha vidani viitwavyoinano (kundolela inano) kwa kupasua katikati mbegu ya mti uitwao mkangaula.Kamwe unyago haupangwi hivi ili ufanyike wakati msichana apatapo hedhi mara ya kwanza ili kama imetokea bahati hiyo basi Bi mkubwa yaani Likolo hutengeneza imale. Likolo hujipaka imale maungoni mwake na mwa walombo wengine ili kujikinga wasije wakapata upofu wa macho katika kushirikiana nao.Kama ilivyo elezwa hapo nyuma kwamba matendo ya madabwa yafanyikayo hayasemwi ovyo. Wasichana wa dini za kikristo hawapatiwi tena mafunzo ya unyago kwa ukamilifu bali hupewa mabugo ambayo ni mafunzo mafupi nayo hudumu kwa muda wa siku saba hivi. Hufundishwa juu ya miiko wajibu na matarajio ya mama wa Kimakonde katika jamii.Wasichana wote kabla ya kuingia unyagoni hujulikana kama anahaku wengi wanamahaku na baada ya kufundwa hujulikana kama mwali wengi wanawali. Akina mama hujikusanya pamoja na kufanya shauri la kuwapeleka binti zao kwenye chiputu. Wakisha afikiana humchagua Likolo kuwa ndiye mkuu wa taaluma za unyago. Ujira huo hutofautiana baina ya kijiji na kijiji kutegemea uhusiano na uelewa uliopo kati yao. Nyumba ya kutolea mafunzo hayoinande yanole huchaguliwa.Jioni ya siku iliyochaguliwa kuwa ndiyo ya kuanzia mafunzo ya unyago kila msichana atakaye hudhuria mafunzo hushikwa kukamula na wakala fulani ambao wameidhinishwa na wazazi.
Wakala wa kuwakamata wasichana wanaweza kuwa ni wifi nnamuwe wake au mwanamke yeyote yule ambaye anajuana na yule msichana vya kutosha. Mwanamke ambaye ni wakala asiye shemeji yake huitwa ankamwe-nole.Baada ya kumshika msichana hupelekwa kwa mama yake. Mama binti mwenyewe pamoja na nnombo huenda pamoja hadi kule inande yanole. Wakaribiapo inande yanole huimba nyimbo za kumwandaa yule binti anaye sindikizwa kwenye chiputu. Wanapo wasili hapo wasichana huamkiana kwa kugonganishwa vichwa vyao ikiwa ndio ishara ya kuhimiza uhusiano mzuri kati yao kwa muda wote watakapo kuwa pamoja.
Nitaendelea kuwadondoshea siri zaidi kesho, Inshaallah!
MUENDELEZO....
No comments:
Post a Comment