UCHUNGUZI
unaonesha kuwa kila mtu anapenda kujitegemea, lakini wengi wanashindwa kufanya
hivyo kwa sababu ya kukosa kitu wanachokiamini, nacho ni kutokuwa na uwezo wa
kufanya hivyo!
“Napenda
sana kujitegemea lakini sina uwezo,” wengi hutamka hivyo unapowauliza kwa nini
wanazeekea kwenye maisha ya utegemezi. Sababu ya kukosa uwezo imewafanya baadhi
ya watu kuwa tayari kupokea kila aina ya manyanyaso na mwisho wa yote
wanajipoza kwa kulia.
Swali la
kujiuliza: Ni nani aliyezaliwa
anajitegemea? Jibu ni hakuna, hapa ndipo penye msingi wa mada hii ambayo
naamini kupitia vipengele vifuatavyo msomaji wangu utajifunza jinsi ya kuanza
maisha ya kujitegemea.
MTAZAMO
Kikwazo cha
kwanza kinachowafanya watu waishi maisha ya utegemezi ni mtazamo. Wengi wanaamini wana haki ya kulelewa na
wazazi/ndugu, lakini wanashindwa kujiuliza wataishi katika utegemezi mpaka lini
na wanaowategemea wakifariki dunia wataishije?
Kazi ya
kwanza katika kuyaelekea maisha ya kujitegemea ni kubadili mtazamo wa maisha
tegemezi na kuona umuhimu wa kujitegemea.
Maana yangu hapa ni kuyachukia maisha ya kumtegemea mtu na kutamani
maisha ya kujitegemea ambayo ni huru na yenye raha.
KUJITEGEMEA
NDANI YA UTEGEMEZI
Baada ya
kubadilisha mtazamo, mhusika ni lazima aanze maisha ya kujitegemea ndani ya
utegemezi. Msingi wa kipengele hiki ni huu; kuna baadhi ya watu wanabweteka mno
na kutaka wafanyiwe kila kitu na walezi wao ambapo hata andazi la shilingi 100
wanataka wanunuliwe! Kisingingizio ni kilekile, kwamba hawana uwezo ingawa fedha
kama shilingi mia mbili wanazipata.
Kujifunza
kujitegemea lazima kuanzie ndani ya maisha ya kutegemea, mfano kama jukumu la
baba ni kununua mboga na wewe umebahatika kupata kiasi cha fedha kwa njia
yoyote hata ya kupewa, usizifiche, badala yake lichukue jukumu la baba na
kulifanya wewe. Tabia hii inajenga
msingi wa uwajibikaji ambao ndiyo nguzo ya maisha ya kujitegemea.
Chukia
maisha ya kufanyiwa kila kitu, jihangaishe kwa kazi ya aina yoyote, jiwekee
utaratibu wa kuhudumia familia yako, weka msingi wa kuheshimu fedha,
usiendekeze tabia ya kupata fedha na kuacha kufanya jambo la maana nyumbani
kisa unamtegemea mtu atakununulia hiki na kile na kuzifanya fedha zako ziwe za
kutapanya ovyo. Ukijizoeza hivyo hutaweza kujitegemea.
Kwa leo naomba
niishie hapa, ila nikuache na swali hili:
Ni mara ngapi umekuwa ukimsaidia
mlezi wako kukabiliana na changamoto za kuendesha maisha? Kama unafanya hivyo tambua umeanza mazoezi ya
kujitegemea, endelea kufanya hivyo lakini kama umebweteka tu nyumbani tambua
uzee utakukuta ukiwa mtumwa wa mtu.
KUJIAMINI
Vikwazo au shaka juu ya kuweza kumudu maisha
ya kujitegemea vimewafanya wengi wasijiamini. “Kwa kipato hiki nitaweza kweli
kuendesha maisha yangu, nilipe kodi ya nyumba, chakula, mavazi na mahitaji
mengine?” Maswali ya aina hii mara nyingi yamekuwa na majibu ya haitawezekana!
Tabia ya
akili hasa katika kufikiria mambo yajayo ni kujenga hofu ambayo wakati mwingine
haihitajiki; wenye kujiamini pekee ndiyo ambao hutupilia mbali hofu na
kujiamini ndiyo walioofanikiwa katika maisha yao.
Kwa msingi
huo, unapofikiria maisha ya kujitegemea usiwaze sana juu ya kuwezekana kwa
mambo, jiamini kuwa utaweza, ukifanya hivyo utaweza; siku zote mwenye shaka
havuki mto!
KUCHUKUA
HATUA
Hatua
nyingine muhimu baada ya kupita vipengele nilivyoanisha hapo juu ni hiki cha
kuchukua hatua. Watu wengi wamekuwa wakipanga kujitegeme, lakini kila mwaka
wanaahilisha kufanya hivyo. “Nafikiri nitahama mwaka ujao.” Mwaka ukifika
anapanga kufanya hivyo mwaka unaofuata matokeo yake anazeeka akiwa kwenye
maisha tegemezi.
Ushauri
wangu, baada ya kujiamini kuwa unaweza chukua hatua ya kutoka mahali ulipo,
jambo kubwa la kuzingatia hapa ni kuhakikisha kuwa uchukuaji hatua lazima
uambatane na ushauri mzuri kutoka kwa ndugu na jamaa na hasa wale uliokuwa
unaishi nao kama wanakuunga mkono katika suala hilo.
KUTORUDI
NYUMA
Uchunguzi
unaonesha kuwa wapo watu ambao hupitia hatua zote za kuelekea kujitegemea,
lakini wanapozikabili changamoto za maisha hayo huamua kurudi mahali wapokuwa
wanaishi jambo ambalo huwaongezea fedheha na mara nyingine kuwaathiri
kisaikolojia.
Unapokuwa
umeanza maisha ya kujitegemea suala la kurudi ulipotoka lisiwe la kawaida. Kumbuka
unapokuwa na wazo la “nikishindwa narudi kwa baba,” huwezi kujituma, hutapambana
na changamoto za maisha binafsi kwa vile kinga yako haitakuwa kwako bali kule
ulikotoka, kushindwa itakuwa ni sehemu yako.
ONGEZA
MARAFIKI
Unapokuwa
kwenye maisha ya kujitegemea hakikisha kuwa unajitahidi kupunguza maadui. Fanya
kila linalowezekana kuongeza marafiki ambao siku zote ndiyo nguzo muhimu
nyakati za shida. Kumbuka kazi ya rafiki ni kufariji na adui kuangamiza!
Baada ya
kusema hayo, naamini mada hii itawasaidia wengi, furaha yangu ni kusikia baada
miezi, miaka michache kuwa watu wengi walijitegemea kutokana na hamasa
waliyoipata kwenye soma hili!
No comments:
Post a Comment