Kwenye
maisha kuna nyakati za kutofautiana, kukasirishana. Katika hali ya kawada kipindi
hiki huwa ni za hatari kwa sababu husababisha nyufa kubwa za uhusiano katika
jamii.
Sote
tunajua, watu hupigana, huachana, hujeruhiana, hutukanana, hudhalilishana wakiwa
na hasira. Hata hivyo, si wote wanaojua wafanye nini wanapojikuta wameingia
kwenye hatua hiyo mbaya.
Msomaji
wangu, hebu jaribu kukumbuka ugomvi mmoja uliotokea kati yako na mwenzako na
ikiwezekana jikumbushe mlivyoanza! Utabaini kuwa mlianza kama utani na
mkajikuta mmefura kwa hasira, mkatwangana makonde, mkatamkiana maneno makali ya
kuudhi na pengine mkafikia uamuzi mbaya.
Yote
hii ni kwa sababu mlikosa elimu ya mazungumzo. Ingekuwa mmoja wenu hasa yule
aliyekuwa wa pili kukasirika anafahamu hatua za kuzungumza na mtu aliyekasirika
angechukua jukumu la kutuliza machafuko na kuleta amani kwenye jamii.
Ungana
nami leo katika kutafakari hatua zifuatazo zinazoweza kusaidia kuzungumza na
mtu aliyekasirika.
MPUNGUZE
MHEMKO
Hasira
hujaza kifua, huathiri mzunguko wa damu na ufahamu. Mtu aliyekasirika huwa vigumu kwake kusikiliza au kutazama mambo kwa jicho la
tatu. Mwenye hasira huwa hafikirii matokea yajayo badala yake hutazama zaidi
tukio na jinsi ya kupata ushindi iwe kwa maneno au kwa mapambano.
Katika
hali ya namna hiyo, mtu mwingine akija na busara za kutaka kumgeuza haraka
haraka hawezi kumuelewa. Muhimu hapo ni kuacha kumwadama, kujibizana naye,
kumshawishi asikilize badala yake mpe nafasi ya kusema atakavyo, abwate ajuavyo
huku wewe ukimuitikia na kumkubalia lawama zake. “Basi ndugu yangu mwenye
makosa ni mimi.” Kauli za aina hii zitampunguza hasira kwani atajiona msindi.
MSOME
SAIKOLOJIA YAKE
Kwa
kumfahamu mpenzi/ndugu yako kwa kina itakuwa rahisi kwako kumtambua kuwa
amepunguza hasira na kurudi katika hali yake ya kawaida. Ukisha fahamu hilo
chukua jukumu la kumsoma kisaikojia ili kujua kama yuko kwenye hali nzuri ya
kusikiliza yale uliyotaka kumwambia wakati alipokuwa na hasira.
Zoezi
hili linaweza kuchukua saa kadhaa na wakati mwingine hata siku mbili. Lengo ni
nini? Ni kupata matokeo sahihi ya kuondoa chuki za mwenzako na kumfundisha
madhara ya kukasirika. “Ndugu yangu nakupenda sana, lakini juzi uliniumiza,
uliniambia mimi malaya kwa kosa ambalo sikufanya?” Bila shaka muda huo atakusikiliza
zaidi kuliko ungebishana naye alipokuwa
na hasira.
MRUHUSU
AKUJIBU
Pamoja
na kumsoma kisaikojia na kumwambia kinagaubaga makosa yake, usimzuie kujitetea,
mpe nafasi ya kuzungumzia kilichomkasirisha. “Unaona bado unanitukana, sasa
naamini siku ile ulikuwa umedhamilia.” Usisiseme hivyo, mwache ajibu hoja hata
kama atakuwa anakukandamiza na kuzidi kujijengea ushindi. Mvumilie aoshe ubongo
wake.
EPUKA
MARUMBANO
Kama
nilivyosema hapo juu wengine huwa wagumu kuelewa, ni watu wa kuficha udhaifu
wao na kutopenda kuonekana wamekosea. Watu wa namna hii unapowarejeshea
mazungumzo wanaweza kujikuta wanahamaki
tena.
“Kwa
hiyo ulikuwa unasemaje…nilifanya ndiyo,… wewe unaamuaje?” Mkifika kwenye alama
hiyo usikubali kurumbana naye mwache aseme halafu wewe ingia kwenye hatua ya
tano.
MUOMBE
MSAMAHA
Hata
kama atakuwa yeye ndiye mwenye makosa na amekataa kukiri, usijali, chukua jukumu
la kumuomba msamaha na kueleza tena nia yako ya kumazungumzo ilikuwa ni
kuelewana si kugombana. Kumbuka hata kama amekiri kosa, bado unatakiwa kumuomba
radhi kwa kurejea yaliyopita. “Ndugu yangu inawezekana nikawa nimekuudhi tena kwa
niliyosema, nakuomba sana tusameheane.”
Bila
shaka kwa haya machache msomaji wangu utakuwa umejifunza na kuchukua hatua za
kuzuia migogoro mikubwa inayotokana na hasira. Katika maisha tusikubali
kuruhusu hasira zitumike kutuchumia janga la majuto.
No comments:
Post a Comment