Nilianza kujisikia vibaya hata kabla ya
kufunga ndoa. Nakumbuka miezi mitatu kabla wakati tukiwa katika
maandalizi maandalizi ya Bashiri kuja nyumbani kuleta mahari miguu
ilianza kuuma kiasi cha kushindwa hata kutembea. Mama ainikanda mara kwa
mara na ilikuwa ikivimba na kutoa maji kama vile jasho lakini la
baridi.
Nilienda hospitali zote lakini
sikugundulika na kitu chochote, nilipewa dawa tu za maumivu ambazo
kusema kweli hazikusaidia chochote. Ndiyo nilikuwa nimemaliza chuo hivyo
hata mchakato wa kuzunguka kutafuta kazi ilibidi niusimamishe, Bashiri
alinipa moyo na kuniambia kuwa kazi nitapata tu nishughulikie afya
yangu kwanza.
Nilifuata ushauri wake na mipango
iliendelea huku nikipata nafuu na kuzidiwa, napata nafuu nazidiwa hivyo
yani. Kutokana na hali yangu tuliamua kuchanganya sherehe zote kwamaana
ya Send off na Reception, Kitchen Party ilifanyika kwa watu wachache na
muda wote nilikuwa nimekaa. Siku ya sherehe niliingia ukumbini vizuri,
sherehe ikaanza tukakata keki, tukala chakula lakini zawadi kule
kusimama kupokea zawadi nilishindwa kabisa.
Miguu ilikuwa inawaka moto huku ikitoa
jasho la baridi, sijui nini kilikuwa kikiendelea huko chini kwani viatu
nilivyokuwa nimevaa vilijaa maji, niliwekewa kiti na MC akasema maharusi
wakae na alipoona nimezidiwa alisema watu wacheze mziki na maharusi
tuachwe wakapumzike. Watu hawakuelewa chochote kwani ingawa nilishindwa
hata kunyanyuka lakini MC alikuwa mjanja.
Aliongea kua Bwana Bashiri sasa hembu
mbebe mke wako kuonyesha upendo kuwa utamlinda na kubeba katika maisha
yako yote. Mume wangu alininyanyua na kunibeba kunitoa nnje,
nililazimisha tabasmu mpaka nilipoingia kwenye gari ambapo moja kwa moja
tulielekea Muhimbili ambapo nilikaa kwa wiki mbili bila kupata nafuu
yoyote. Walishindwa kwani walikuwa hawajui ni kitu gani kilikuwa
kikisababisha hali ile.
Miguu ilikuwa inauma kwenye mifupa,
mwanzoni ilikuwa ni mpaka magotini lakini kadri siku zilivyokuwa
zikienda maumiivu yalipanda mpaka kiunoni. Mbali na maumivu nilikua
nikitokwa na jasho la baridi kama maji, yaani nikilalia shuka au nikivaa
nguo baada ya masaa mawili nakuwa kama nimemwagiwa maji. Mwili
unachemka lakini natoa jasho la baridi.
Kutokana na maumivu sikuweza kufanya
chochote, hata kunyanyuka kwenda kujisaidia ilikuwa shida hivyo mume
wangu alikuwa na kazi ya kunibeba kila siku mpaka chooni na kunisafisha.
Anapokuwa kazini tulikuwa na mfanyakazi ambaye alikuwa akinisaidia kama
kunikausha maji lakini alikuwa hawezi kuninyanyua hivyo kazi zote za
kunibadilisha na kunisafisha ilikuwa juu ya mume wangu.
Mwaka uliisha nikiwa katika hali ile,
mume wangu alijitahidi sana akauza na viwanja vyake alivyo nunua kipindi
cha ujana na kunipeleka mpaka India lakini haikusaidia, nilipewa dawa
tu kwaajili ya kukausha jasho ambazo zilisaidia kidogo lakini maumivu
yalikuwa hayakomi, sanasana mwili ulikuwa unakakamaa tu.
*****
Yale hayakuwa aina ya maisha ambayo
nilipanga kuishi katika ndoa, kila nilichokuwa nikikiwaza kilikuwa
kinyume chake, nilimuonea sana mume wangu huruma kwani badala ya kuwa
mume alibadilika na kuwa nesi. Muda ulikuwa unaenda na kama mtoto wa
kwanza nyumbani kwao wazazi walishakata tamaa, walihitaji mjukuu na kila
siku walimsumbua kutafuta mke mwingine.
Hata mimi nilitamani aoe mke mwingina au
hata atafute kimada wa kumtuliza hisia zake kwani tangu kuoana tulikuwa
hatuja kutana kimwili, kamba mwaka uliisha bila mimi na mume wangu
kufanya mapenzi. Siku moja uvumilivu ulinishinda na nikiwa katika
maumivu makali nilimshauri kuwasikiliza ndugu zake na kutafuta hata
mwanamke wa kuzaa naye tu kwani mimi sikuwa na dalili za kupona.
Aliniangalia kwa huzuni kisha
akaniuliza. “Unataka kuniambia kama ni mimi ningekuwa kwenye hali hiyo
na wewe ungeniacha ukatafuta mwanaume mwingine?’ Jibu lake lilikua
rahisi “Hapana, wewe ni mume wangu nakupenda sana…” Niliongea kwa suti
ya unyonge lakini ya kumaanisha. “Sasa kama ni hivyo mbona mimi unataka
nikusaliti…”
Nilitulia kidogo na kumuambia “Lakini
wewe ni mwanaume, unahisia, sisi wanawake tunaweza kuvumilia, lakini
wewe ni mwanaume, wazazi wako wanataka wajukuu, mimi siwezi kupona leo
wala kesho oa mwanamke mwingine hata kama hutaniacha nitafurahi kukuona
unafuraha…” Nilijitahidi kujibu kwa sauti ya kutetemeka na ya kukata
tamaa. Bashiri aliniangalia machoni kwa muda mrefu kisha akaniuliza.
“Hivi kuna fomu ambazo ulijaza kufanya
maombi ya huu ugonjwa kwa Mungu?” Aliniuliza swali ambalo sikupata jibu…
“Mimi ndiyo napaswa kukuonea huruma kutokana na maumivu uliyonayo sio
wewe kunionea huruma eti nahitaji mwanamke wakutuliza hisia zangu au
mtoto ili na mimi nionekane mwanaume!Kama siwezi kuvumilia hisia za
mwili wangu kw asababu ya ugonjw abasi sipaswi hata kuitwa mwanaume
achilia mbali mume wako!” Aliongea maneno ambayo yalinipa faraja na
kunifanya niandelee kupigana bila kukata tamaa.
Miaka miwili ilipita hali yangu ikiwa
bado haijatengamaa, nilitamani kukata tamaa lakini kila siku mume wangu
alinipa nguvu ya kuendelea kupambana. Tulienda kwennye maombi na kutumia
dawa mbalimbali za hospitalini na za kienyeji lakini haikusaidia. Watu
wengi waliamini nimelogwa lakini kutokana na imani tulimkabidhi Mungu
awe muamuzi wa yote.
Siku moja mume wangu alikuja na Mzee
mmoja pale nyumbani, wakati huo sikua najua alimpatia wapi lakini yule
mzee alikaa nyumbani pale kwa miezi sita akiondoka mara moja moja na
kukaa kama siku nne tano na kurejea. Alikuwa akija na dawa za kienyeji
za kunikanda, kunichemshia na kunywa, dawa zilikuwa chungu na kusema
keli ilikuwa kama adhabu kwani ilikuwa kutwa mara tatu na kukandwa tena
dawa za moto.
Ukichanganya na maumivu basi ilikuwa
kazi sana lakini sikua na namna nilivumilia. Kweli miezi sita ile
nilianza kupata nafuu, maumivu yaliisha kabisa ingawa bado nilikuwa
siwezi kunyanyuka, miguu haikuwa ikitoa maji tena wala kukakamaa
niliweza kukunja lakini sikuwa na nguvu ya kusimama. Baada ya kupata
nafuu ile yule mzee alituambia kuwa ameshafanya yake yaliyo ndani ya
uwezo wake sasa kilichobaki ni kumuachia Mungu, alinipa dawa za kunywa
na kumpa mume wangu jukumu la kunifanyisha mazoezi.
****
Hali yangu ilianza kutengamaa, kila siku
asubuhi na jioni mume wangu alikuwa akinifanyisha mazoezi. Kwa mara
yakwanza tangu kuingia kwenye ndoa, niliweza kumuangalia mume wangu na
kuanza kumuona kama alivyo bila maumivu. Siku moja wakati akinifanyisha
mazoezi, nilimkodolea macho, alikuwa amekonda kupita kiasi, kusema kweli
kila siku nilikuwa naye lakini siku ile ndiyo niliona tofauti.
Yaani alikuwa amepungua na kuwa kama
mtoto, uso wake ulionekana hauna nuru ingawa kila mara alikuwa
akilazimishia tabasamu lakini alionekana kweli na mawazo. Nilijipa moyo
nikiamini labda ni sababu ya ugonjwa wangu ndiyo ulikuwa unammaliza
kutokana na mawazo, siku nilimuomba kuangalia picha zetu za harusi kweli
alikuwa amekonda sana kuliko hata nilivyowaza awali.
Nilishindwa kuvumilia na kumuuliza nini
kilikuwa kinamsumbua tofauti na hali yangu, aliishia kutabsamu na kusema
hakuna kitu ni maisha tu nikipona na yeye atakuwa sawa. Lakini ukweli
mume wangu hakuja kuwa sawa tena. Sikumoja mume wangu aliingia chumbani,
nilishaanza kupata nafuu ingawa bado nilikuwa siwezi kunyanyuka wala
kufanya chochote.
Alionekana kuwa na huzuni kuliko kawaida
yake, ingawa alijaribu kutabasmau lakini nilimuona kabisa akilengwa
lengwa na machozi. Aliongea na kunikalisha kitandani kisha nayeye akakaa
pembeni yangu na kuniambia. “Mke wangu kuna kitu naomba unisaidie,
yaani uniahidi kukifanya, nakuomba sana unahidi kitu hicho na hata iweje
usijekubadilisha mawazo, naomba sana…”
Aliongea huku akilengwa lengwa kwa
machozi, nilimuambia hakuna hata haja ya kuuliza nilikuwa tayari kufanya
kitu chochote. Alisisitiza niahidi kufanya na mimi niliahidi huku
nikinyanyua mikono yangu kumkumbatia. “Mke wangu naomba nikifa uolewe
tena na kama Mungu akikujalia mtoto basi kama ni wakiume umpe jina langu
na kama ni wakike basi jina la kati liwe la kwangu…”
Aliongea machozi yakimtoka, sikutaka
kumsikiliza kwanini anaongelea kufa nilijaribu kumtuliza lakini
aliniomba ni muahidi hicho kitu. Alirudia zaidi ya mara kumi ndipo
nilipomuahidi kua nitafanya hivyo. Baada ya kumuahidi aliniambia kuwa
yeye hawezi ishi mdua mrefu, aliamua kunificha lakini anajua hana muda
hivyo kuamua kuniambia. Mwaka mmoja uliopita aligundulika kuwa ana kansa
ya damu na ilikuwa katika hatua mbaya.
Hakutaka kuniambia kutokana na ugonjwa
wangu lakini Daktari aliyekuwa anamhudumia alimuambia kuwa hana zaidi ya
mwaka ila mpaka wakati ananiambia ilikua ni karibu miaka mwili kitu
ambacho ilikuwa ni kama miujiza. Aliniambia hajisikii vizuri na kaamua
kuniambia kwani hata nguvu ya kunihudumia hana tena. Kweli mume wangu
alikuwa amechoka na hali yake ilikuwa mbaya.
Sijui nilipata wapi nguvu lakini
nilijikuta nasimama, ingawa sikusimama kwa muda mrefu lakini sikutaka
kulia, nilijitahidi kuzuia machozi na kumkumbatia mume wangu. Ilikuwa ni
karibu miaka mitatu tangu tuoane na katika muda wote huo tulikuwa hata
hatujakutana kimwili, alivumilia ugonjwa wangu tangu siku ya kwanza ya
ndoa yetu na mimi nilimuomba Mungu anipe nguvu hata niwezie kumhudumia
lanini haikutokea. Sikuweza kusimama tena mpaka sasa wakati naaandika
hapa.
Ingawa nimeweza kupona lakini magoti
yangu hayana nguvu kuubeba mwili wangu hivyo nalazimika kutumia kiti cha
magurudumu. Mume wangu alifariki mwezi mmoja baada tu ya kunipa zile
taarifa na kila siku katika mwezi huo alisisitiza niolewe ili niwe na
furaha. Ni mwaka wa pili sasa, sijaolewa na sidhani kama nitakuja kuwa
na furaha, naweza kufanya kazi zangu lakini sijui kama nitaweza
kuufungua moyo wangu tena.
******
Kila siku maneno ya mume wangu hunijia,
najua alitaka niwe na furaha na kila siku na muomba anipe mwanaume wa
kunipa furaha. Natamani sana nimzalie mtoto ili tu abebe jina lake,
nadhani hicho ndiyo kitu ambacho kinanipa nguvu mpaka sasa. Mungu
alinipa Mume akanipa na Nesi. Alijitoa kwaajili yangu akiwa mzima na
hata baada ya kugundua kuwa ni mgonjwa aliweka ugonjwa wangu mbele na
kunihudumia mimi kwanza.
Natamani kuandika mengi ila leo niishie
hapa. Lengo la kuandika kisa changu hiki nikuwaasa tu nyie mlioko katika
ndoa kuwa msipoteze muda wenu katika kunyanyasana na kuudhiana, katika
kugombana, kuna muda mchache sana wa kupendana na kila siku utakua
ukijuta kama hukumpenda mwenza wako ipasavyo. Mapenzi ni furaha, ingawa
ndoa yangu yote ilikuwa ya mateso lakini yalikuwa ni mateso ya ugonjwa,
ilikua ni ndoa ya amani na mume wangu kila siku alihakikisha natabasmau.
Alifanya kila kitu ili kuhakikisha kuwa
nina furaha hakuchoka kunifanya nitabasamu hata nikiwa katikati ya
maumivu makali. Nakumbuka alijua napenda sana kuvaa viatu virefu hivyo
karibu kila mwezi aliniletea zawadi ya viatu na kila viatu vipya
vilipotoka alikuwa akiniletea. Alivipanga ndani na kuniambia hakutaka
fasheni inipite hivyo nikipona nita vaavvyote. Mpaka sasa sijaweza
kuvvaa kwani bado sijaweza kutembea ila naamini ipo siku Mungu
atanisimamisha na nitaweza kutembea na nitavivaa vyote kwaajili yake.
Naomba nimalizie hapa, samahanini kwa
stori ndefu nitafurahi sana kama utatumia sekunde chache kushea stori
yangu. Lengo langu ni kwa yule anayesoma awe mwanamke au mwanaume
kumpenda sana mtu aliyenaye na kumuonyesha mapenzi ya kweli kwani siku
akiondoka utatafuta mtu wa kumuonyesha mapenzi itashindikana. Mimi nina
mambo mengi ya kumkumbuka Mume wangu, hembu jiulize wewe ukiondoka leo
mume au mke wako atakukumbuka kwa nini? Atakukumbuka kwa mazuri au
mateso uliyompa?
Ahsante sana kaka, huwa natumia muda
wangu mwingi kwenye ukurasa wako nikisoma unachoandika kuhusu mapenzi.
Watu wengi wanachezea upendo wanaoonyeshwa leo kwakuwa wanadhani labda
hautakoma, siku ukikoma ndipo watajuta. Mungu awabariki wote na
awasaidie msije kujuta kwa mnayowafanyia wapenzi wenu bali
muwatengenezee kumbukumbu nzuri na kuwapa faraja kila siku.
Kumbuka kuna siku utatamani kumuambia
mko au mumeo unampenda lakini hatakuwepo kukusikia, kuna siku utatamani
kumnunulia zawadi na kumpa tabasamu, kuna siku utatamani kutoka na
familia nzima kufurahia maisha lakini mwenza wako hatakuwepo. Kwanini
unatumia muda wko mwingi kutengeneza ugomvi, chuki na manyanyaso kwa
mwenza wako. Ahsante sana kaka Iddi kwa kukubali kukiandika kisa changu
na kunisikiliza, Mungu awabariki wote mliosoma kis ahiki na kitumieni
kusambaza upendo.
***MWISHO***
No comments:
Post a Comment