Ni ndoto ya kila mtu anapoingia kwenye
ndoa au mahusiano kuwa na furaha. Sijawahi kukutana na mtu ambaye
anasema lengo lake la kuolewa au kuoa ni kuteseka. Lakini ni watu
wachache sana ambao wapo kwenye ndoa au mahusiano ambao wanafuraha.
Wengi huishi kwa huzuni katika wakati flani wa maisha yao ya mahusiano.
Kuna sababu nyingi kwanini wewe kwenye
mahusiano yako huna furaha na mtu pekee wakubadilisha hali hiyo ni wewe
mwenyewe. Kwa kutambua wingi wa watu ambao hawana furaha katika
mahusiano yao basi leo mpenzwa wangu katika mahusiano nimekuandalia
tabia 16 za watu ambao wana furaha katika mahusiano yao. Lakini kabla ya
kuendelea nikukumbushe kitu kimoja;
“Furaha
katika mahusiano inatokana na mambo mazuri mnayofanyiana na mnayofanya
pamoja. Kwa maana kuwa huwezi kuwa na furaha katka mahusiano yako kama
unamfanyia mwenza wako mambo mabaya, hata kama yeye anakufanyia mambo
mazuri bado nafsi itakusuta na itakuondolea furaha. Lakini pia kama
mwili mmoja mnapaswa kufanya mambo mazuri kwa pamoja, mambo ambayo
yatawapa furaha kwa pamoja”.
(1) Hawapeleki Matatizo Yao Kwa Ndugu Au Marafiki;
Wakati mwingine unaweza kudhani kuwa watu hawa hawana matatizo, lakini
ukweli nikuwa wakikutana na changamoto yoyote huongea wao kwanza kabla
ya kuanza kulalamika kwa ndugu au marafiki. Kulalamika lalamika kwa
ndugu kunafanya kutengeneza picha mbaya, ndugu kumchukia mwenza wako na
hivyo kuingilia mahusiano yenu kwa ushauri mbaya au hata kwa kumdharau
na kumdhalilisha.
(2) Hawalinganioshi Maisha Yao Na Wengine;
Wanajua kua kujilinganisha na wengine watapunguzia kujiamini na hata
wakati mwingine kuwafanya kujidharau wenyewe. Wanaridhika na walicho
nacho na huyaona mahusiano yao kama ni ya kipekee. Kujilinganisha na
mwingine ambaye hujui undani wake kunakufanya kushindana na mtu ambaye
hata humfahamu, wanandoa wenye furaha huheshimu ndoa yao na
hawailinganishi na yeyote.
(3) Hawalaumu Wenza Wao Kwa Mapungufu Yao;
Kila mmoja anajua wajibu wake na anapokosea basi hukuabli makosa kuliko
kubakia kulaumu mwingine. Wanajipima wao na kuangalia usafi wao kuliko
kufanya mambo kwa kuangalia makosa ya wengine. Kwa mfano, mke au mume
anapopitiwa na kuchepuka badala ya kumlaumu mwenzake kuwa alikuwa
hamridhishi, hujua amekosa yake akaomba msamaha, akajirudi na kuangalia
ni kwa namna gani atamfanya mwenza wake kumridhisha.
(4) Wanajua Maisha Ni Burudani, Hawachukulii Kila Kitu Siriasi; Kwao
ni kama walikutana jana, hata kama washazeeka kwenye ndoa, bado
wanataniana, bado wanatoka pamoja, wanacheza pamoja na kufanya mambo
yote ambayo huko awali walikuwa wakiyafanya. Hawasingizii majukumu na
kukasirika kasirika, wanaamua kuwa na furaha kila wakati, huchukulia
changamoto kama shemu ya maisha.
(5) Hawakosoani Wanarekebishana;
Wanajua namna ya kuongea, mwenza akikosea badala ya kumkosoa kwa dharau
huzungumza na kueleweshana. Wanajua kuwa mtu huelewa zaidi pale
unapoonge anaye taratibu, hawajifanyi kama wanajua kila kitu na kila
wakati wapo tayari kujifunza. Hakuna maneno ya ukali wala kisirani,
ukosoaji huwa ni wa kurekebisha na kufundishana.
(6) Wanaongea Kuhusu Pesa;
Wanajua kua matatizo mengi ya ndoa husababishwa na pesa, hivyo huweka
mipango mizuri kuhusu matumizi ya pesa zao. Ni wawazi katika vipato vyao
na wanapanga namna ya kutumia pamoja. Hakuna mwenye nguvu zaidi katika
kupanga matumizi ya vipato vyao hata kama havilingani au mmoja hachangii
kipato kabisa.
(7) Hawawazii Mabaya Wenza Wao;
Watu wenye furaha ni wale ambao huwaza mazuri kwa wenza wao, hawana
mawazo hasi kuhusu wenza wao. Kwa mfano mwenza wao anapochelewa kurudi
huwaza labda kazi zimemzidi au kuna kitu cha maana anakifanya kuliko
kuanza kuwaza labda anachepuka. Kumuwazia mabaya mwenza wako hata kama
hajalifanya utaumia kama vile amefanya na itaondoa amani ndani ya
nyumba.
(8) Wanawasiliana;
Wanajua wenza wao si malaika kwamba watajua wanachowaza, mmoja akitaka
kitu kwa mwenza wake hasubiri mwenzake kubuni au kufikiria sana,
humuambia na kama hakiwezekani basi anaridhika. Mwenza wako si mnajimu
kwamba kila wakati atajua unawaza nini au unataka nini, muambie
unachohitaji ili akufurahishe.
(9) Hawajipangii Majukumu ya Kudumu;
Kwenye ndoa kila kitu nikusaidiana, kwamba watu wenye furaha
hawapangiana kazi kama ofisini kwamba mke ni lazima apike, afue au
afanye usafi. Mume nilazima kutoa hela ya chakula, ada na vitu vingine.
Wao hufanya chochote, mke anaweza lipa ada akanunua chakula bila
kinyongo, mume akaamua kupika au kuosha vyombo. Kwakifupi hufanya mambo
kama wenza na si kwa kutegeana eti kusema hii ni kazi ya flani?
(10) Wanasaidiana;
Yaani badala ya kulaumu tu na kulalamikia kuwa mbona wewe hujafanya hiki
na yule hajafanya kile wao husaidiana katika majukumu. Mmoja akiona
kitu hakiko sawa, akiona mwenzake hajamaliza au hayuko vizuri kufanya
kitu flani basi hukifanya bila kinyongo kwa furaha ya kumsaidia mwenza.
(11) Wanashukuru; Kila
mmoja anatambua majukumu ya mwenzake na namna anavyojitahidi
kumfurahisha mwanzake. Wanashukuru kwa kila kitu, hawashukuru tu kwa
maneno bali pia kwa vitendo na kutoa tabasamu, hata kama ni kwa kitu
kidogo tu ambacho mmoja wao atamfanyia mwingine lakini watashukuru
pamoja.
(12) Wanafanya Mambo Mengi Kwa Pamoja;
Wanajua kuwa ndoa ni pamoja na kushirikiana kufanya mambo pamoja. Si
katika majukumu ya kifamilia tu bali hata katika mambo mengine kama
michezo na burudani. Hutembea pamoja, kufanya mazoezi pamoja, kula
pamoja, kuangalia mpira pamoja na kufanya angalau kitu kimoja kwa pamoja
kamka wanandoa.
(13) Wanaungana Mkono;
Iwe ni katika kazi au hobi, watu wenye furaha huungana mkono hata kama
hawafurahii kile ambacho wenza wao wanakifanya lakini kwakuwa wanajua
kuwa kinawapa furaha basi huungana mkono. Mwanamke ambaye hapendi mpira
atamsindikiza mumewe uwanjani kama ambavyo mwanaume ambaye hata hajui
urembo ni nini atampeleka mkewe kwenye mashindano ya urembo.
(14) Wanasameheana Na Kusahau:
Hawakumbushani mambo yaliyopita, wakishasamehe basi husahau na hata
mmoja wao akirudia kosa lile lile basi hawatasme hii ndiyo tabia yako
bali watarekebishana na kusonga mbele. Hawaweki kumbukumbu ya makosa ya
wenza wao na hawana vinyongo, hutoa madukuduku yao kwa kuongea na si kwa
kulalamika pembeni na wakishaonge abasi husahau.
(15) Kila mmoja anatambua udhaifu wa mwenzake;
Kila mmoja anamjua mwenzake vizuri anatambua udhaifu wake na
amekubaliana nao, kuishi nao na pia kumsaidia mwenza wake kutokana na
udhaifu huo. Hamsengenyi wala kumnyanyapaa mwenzake kutokana na ushaifu
huo. Atamsaidia mwenza wake kuficha ushaifu huo na kuonyesha mbele za
watu kuwa mwenza wake ni mkamilifu.
(16) Wanasali Pamoja;
Labda hii ilipaswa kuwa ndiyo sifa ya kwanza lakini nimeiweka mwisho ili
kuonyesha kuwa yote hayo hayawezi kuwezekana bila Mungu. Watu wenye
furaha wanamjua Mungu na mioyo yao inaamani kwanni wanajua kua kuna
nguvu ya ziada ambayo inawalinda.
No comments:
Post a Comment