Tafadhali naomba ficha jina ila
lakini naomba ushee kisa changu kwani naamini itasaidia wasomaji wako
kujifunza kutoka kwangu. Mimi ni mwanamke wa miaka 27, niliolewa kama
miama miwili hivi iliyopita na mwanaume ambaye tulidumu katika mahusiano
kwa takribani miaka minne hivi kabla ya kufunga ndoa. Wakati tunakutana
mimi nilikuwa chuo mwaka wa kwanza na yeye tayari alikuwa anafanya
kazi.
Kusema kweli nilimpenda sana mume
wangu kabla na baada ya ndoa na hata lakini kitendo alichonifanyia
siwezi kukisahau katika maisha yangu. Mwanzo wa mapenzi yetu alikuwa
mstaarabu sana, akinihudumia kwa kila kitu, akijali hisia zangu na kila
mara kunionyesha kuwa ananijali na wakati wote tangu mwanzo alikuwa
akisema kuwa mimi ndiye mwanamke ambaye angapenda kunioa.
Ingawa nilimpenda sana na alikuwa
akionyesha kweli kuwa anamaanisha sikumuamini sana kwani nilijua wanaume
wote ni waongo. Lakini kweli alionyesha kunipenda, tatizo lake alikuwa
na wivu na hasira sana, yaani kila mara alitaka kuwa na mimi, hakutaka
niwe na marafiki wa kiume. Kila rafiki aliyekuwa akiniona naye alihisi
natembea naye na hilo lilinikwaza sana.
Nakumbuka wakati mmoja nikiwa niko ‘Discussion’ na wanafunzi wenzangu alinipigia simu nikachelewa kupokea, kwahiyo akawa amepiga kama mara mbili hivi, akaniuliza uko wapi nikamuambia nipo kwenye ‘discussion’ aliwasha gari na kuja mpaka chuo, alinikuta nipo na wakaka watatu ambao tulikuwa tunafanya ‘assigment’ alinichomoa katikati yao na kunipiga makofi mbele yao, kisha akanichukua mpaka kwenye gari lake na kuondoka na mimi.
Kitendo kile kilinikera sana kwani
mbali na kuniumiza kimwili lakini alinidhalilisha pia, lakini nilikuja
kumsamehe baada ya kuniomba sana msamaha. Madai yake iilikuwa kwanini
niwe na ‘discussion’ na wanaume pekee, ukweli nikuwa group letu lilikuwa
la watu sita wanaume watatu na wanawake watatu lakini rafiki zangu
wawili walichelewa mjini hivyo sisi tukawa tumeamua kuendelea.
Hilo lilipita na kuahidi hatarudia
tena, mambo yaliendelea vizuri akarudisha mapenzi lakini hakupunguza
wivu, aliniminya sana mpaka kunifanya kuwatenga marafiki zangu wengi ili
tu kumridhisha kwani sikutaka migogoro na yeye. Pamoja na yeye kuwa na
wivu namna hiyo na kunichunga sana lakini mara kadhaa nilifumania meseji
za wanawake wake wengine katika simu yake na nilipomuuliza ulikuwa
ugomvi ambao ulipelekea hata kunipiga.
Kwasababu hiyo niliamua
kutokumuuliza, hata nilipomkuta na mwanamke katika mazingira tata
nilijifanya kipofu kwani nilimpenda sana na nilivumilia nikiamini kuwa
iposiku atabadilika. Baada ya kumaliza chuo nilipata kazi hivyo kitu
ambacho kilikuwa kimebakia ilikuwa ni ndoa tu. Kusema kweli nilikuwa na
hamu sana ya ndoa kwani nilikuwa nikimpenda sana na kubwa kabisa nilijua
baada ya kuoana atabadilika.
Niliamini kuwa baada ya kuniweka ndani hatakuwa na wivu tena na hatakuwa akinipiga kwani tayari atakuwa akinimiliki. Kichwani nilikuwa nikiamini sababu za wivu wake nikutokana na upendo wake kwangu na hofu ya kunipoteza, niliamini baada ya ndoa itakuwa rahisi kwangu kumbadilisha.
Niliongea naye kuhusu ndoa lakini
aliniambia nisubiri “Unaharaka gani ya kuolewa?” Lilikuwa ndiyo jibu
lake na kwakuwa nilimfahamu kama mtu wa hasira basi nilikaa kimya ili
nisimuuzi. Siku moja nilichelewa kidogo kutoka kazini na wakati naondoka
mfanyakazi mwenzangu ambaye yeye alikuwa na gari na alikuwa akikaa mtaa
wa jirani na nilipokuwa nimepanga aliamua kunipa lifti.
Mara kadhaa hunipa lifti lakini
anapofika kwake hunishusha na mimi kutembea kwa miguu mpaka kwangu kwani
hakukuwa mbali sana, lakini siku hiyo kwakua nilichelewa sana aliamua
kunifikisha mpaka getini. Alinishusha na kuondoka zake, niliingia ndani
nikakuta mlango haujafungwa nikajua tu mpenzi wangu yuko ndani kwani
alikuwa na funguo zangu na alikuwa na kawaida ya kuja bila taarifa.
Nilipoingia tu nikiwa sina hili wala
lile nilikutana na kofi ambalo lilifuatiwa na teke lilionidondosha
chini, kabla hata sijajiuliza ni kitu gani mtu alinikanyaga mguu na
nikasikia ‘kaaaa’ mguu ulikuwa umevunjika. Hakujali aliendelea kunipiga
kisha akaondoka kwa hasira, wakati akinipiga alikuwa akinitukana kuwa
mimi ni Malaya na nimefikia hatua wanaume wangu wananileta mpaka
nyumbani.
Aliniacha pale nikiwa katika maumivu
makali, nilijaribu kunyanyuka lakini nilishindwa, kwa bahati nzuri
kumbe wakati ananipiga majirani walisikia na alipotoka kwa hasira
walimuona na waliposikia nalia kwa maumivu waliingia ndani na kuniona
katika ile hali wakaamua kunipeleka hospitalini kwa kunipitishia Polisi
kwanza. Ingawa nilikataa kupitia Polisi nikihofia kuwa mpenzi wangu
atafungwa lakini waligoma wakisema siwezi kutibiwa bila PF3.
Kweli mguu ulivunjika nikafungwa
POP, kule Polisi baada ya kuandika maelezo walitaka kufungua kesi lakini
niligoma kutoa ushirikiano, hiyo ni baada ya kuniomba msamaha na
kunivalisha pete nikiwa bado hospitalini. Ndugu zangu walinisihi sana
kuachana naye lakini sikusikia, aliniambia ni shetani alikuwa amempitia
na nilimuamini, aliomba msamaha sana akiahidi kubadilika.
Baada ya mimi kutokutoa ushirikiano
na yeye kutoa pesa Polisi kesi ilifutwa kabisa na nikiwa bado na POP
langu alijitambulisha kwetu rasmi ingawa walikuwa wanamjua akatoa mahari
na mipango ya ndoa ikaanza kufanyika. Kama miezi minne hivi mguu
ulishapona vizuri nikaweza kutembea bila msaada wa magongo na mwezi wa
tano baada ya kile kipigo tulifunga ndoa.
Miezi ya mwanzo ya ndoa yetu ilikuwa
mitamu na haikuchukua muda sana ndoa ilijibu, nilipata ujauzito kitu
ambacho kilizidisha furaha, akawa mtu wa furaha, akapunguza wivu na
hakukuwa na vipigo tena. Nilimshukuru Mungu kwa mabadiliko yale kwani
nilikuwa na furaha tena na mume wangu alikuwa akijua kujali kwa
vizawadi, outing za kutosha na vacation za hapa na pale.
Kusema kweli mambo yalikuwa mazuri
mpaka mimba ilipofikisha miezi minne, hapo ndipo alipobadilika na kuanza
kusema kuwa hataki nifanye kazi, mara ofisi yenu ina wanaume wengi,
wivu ukarudi na kelele zikawa haziishi. Nilimgomea kuacha kazi kwani
sikutaka kuwa Mama wa nyumbani, isitoshe kazi yenyewe ni nzuri na ina
maslahi makubwa hivyo sikuona sababu ya kuacha kazi na kubaki kuwa mama
wa nyumbani.
Mwanzoni sikujua nikwanini suala la kucha kazi limekuja ghafla wakati hapo awali alikuwa haliongelei, lakini nilipokuja kuchunguza ndipo nilipogundua kuwa kumbe alikuwa akitembea na dada mmoja pale ofisini kwetu na hakutaka mimi nijue ndipo akaona nibora niache kazi.
Siku moja wakati mimba ikiwa na kama
miezi mitano hivi alikumbushia suala la mimi kucha kazi. Ingawa
sikutaka kuzungumzia kuhusu yule dada kwani namjua hasira zake na
nilishakubali kuishi naye hivyo hivyo hata kama anachepuka lakini
nilipandwa na hasira na kuamua kumpasha ukweli kuwa sababu za kutaka
mimi kuacha kazi ilikuwa ni yule dada wa ofisini.
Huwezi amini ilikuwa ni kama mimi
ndiyo ninachepuka, aliwaka na kuanza matusi, alinitukana sana, kwakuwa
najua hasira zake niliamua kukaa kimya na hilo pia lilikuwa kosa,
alianza kunipiga akisema kuwa nina dharau, alinipiga sana sehemu
mbalimbali bila kujali kuwa nilikuwa mjamzito, mimi sikufanya chochote
kila mara nilijikunja ili kuzuia kupigwa tumboni.
Baada ya kumaliza kunipiga
alinichukua na kwenda kunifungia stoo kisha yeye akaenda kulala. Kusema
kweli nilipatwa na maumivu makali ambayo katika maisha yangu nilikuwa
sijawahi kuyapata hasa eneo la tumbo na chini ya kitovu, damu zilianza
kutoka na hapo ndipo nilijua kuwa nimempoteza mwanangu, nilijaribu
kupiga kelele kumuambia mimba imetoka lakini hakusikia mpaka asubuhi
ndipo alinifungulia.
Alinikuta nikiwa nimeshapoteza
fahamu, mabonge bonge ya damu yapo chini. Alinichukua kunipeleka
hospitali lakini kwa uoga alinipeleka katika kliniki tu ya rafiki yake
ambaye alimuambia kuwa mimba imetoka, nilisafishwa na bila kumuambia mtu
yeyote alinirudisha nyumbani. Siku nzima alikuwa akiniomba msamaha
lakini sikuwa tayari kumsamehe, kila nilipowaza mtoto wangu hasira
zilinipanda nakuwa mtu wakulia tu.
Wiki nzima alinihudumia yeye
mwenyewe, nilianza kupata nafuu, sikumuambia mtu yeyote hata ndugu zangu
kwani walishanikataza kuolewa na yule mtu, kuhusu mimba niliwaambia tu
nilidondoka ghafla na mimba ikatoka. Wiki mbili baadaye nikiwa bado
nyumbani kwakuwa kazini walijua mimba yangu imetoka tumbo lilianza kuuma
tena, zamu hii kwa nguvu zaidi na vitu vyeusi kama uchafu kuanza
kunitoka ukeni.
Nilimpigia mume wangu ambaye alikuja
na kunikuta nimezidiwa, alinirudisha kwa yule yule daktari wake ambapo
nilikaa huko siku mbili na hali ilipokuwa mbaya zaidi ndipo
aliponipeleka Muhimbili, aliwambia kuwa nilipata ajali mimba ikatoka
nakwenda kusafishwa, waliponichunguza ndipo waliposema kuwa nilisafishwa
vibaya na kizazi kuguswa na kilishaoza ndiyo maana natokwa na uchafu na
maumivu.
Hawakuwa na namna zaidi ya kukitoa
kabisa na kunisafisha kwani kilishaharibika sana. Ilikuwa ni huzuni
sana, nililia na kuzimia mara tano baada ya zile habari. Ndoto yangu ya
kuwa Mama ilikuwa imesishia pale, mume wangu alijaribu kunituliza na
kunifariji lakini haikusaidia, alinipa moyo kuwa alikuwa akinipenda mimi
na si mtoto lakini wapi bado niliumia na sikuwa na mtu wa kumuambia
maumivu yangu.
Nilikaa hospitalini kwa wiki moja na
nilianza kujisikia vizuri kimwili nikaruhusiwa, nilitamani kuachana na
mume wangu lakini nilishindwa. Kuna mambo mawili ambayo yalinizuia,
kwanza ilikuwa ni namna ya kuwaambia ndugu zangu sababu za kuachana na
mume wangu wakati walijua kuwa ndoa yetu inafuraha na kilichotokea ni
ajali tu ya kawaida, hasa ikizingatiwa hawakujua kwamba nimepoteza
kizazi.
Pili niliwaza ni mwanaume gani
angeweza kunioa hasa akijua kuwa siwezi kumpatia mtoto? Nilijua kuwa
hakuna mwanaume ambaye angeweza kunivumilia tofauti na mume wangu hasa
ikizingatiwa kuwa yeye ndiyo alinisababishia lile tatizo. Nilivumilia na
maisha yaliendelea furaha ilirejea kwa muda mchache mpaka nilipogundua
kuwa amempa mimba mwanamke mwingine tofauti kabisa na yule wa ofisini.
Nilinyamaza tu kwani nilijua kama
ningeongea ingeleta shida, ingekuwa kipigo isitoshe sikutegemea kama
angekaa tu na mimi bila kutafuta mtoto sehemu nyingine, hata mimi
nilitamani awe na mtoto nilitamani kulea na nilijipa moyo kama
angenileteea basi ningemlea bila kinyongo chochote. Lakini haikuwa hivyo
bila ugomvwi wowote bila kutegemea siku moja tu aliniambia.
Siwezi kuishi na mwanamke ambaye hazai, nimevumilia lakini nimeshindwa, sasa hapa kwangu utakuwa unafanya nini? Kungekua na shida nyingine labda mirija imeziba tungehangaika pamoja ila huna kizazi na huwezi kupata mtoto, tutaishi hivi mpaka lini. Mimi tayari nina mtu ana mimba yangu hivyo anataka kuja kuishi humu.
Najua nimechangia wewe kuwa hivyo lakindi ndiyo ishatokea sina chakufanya, siwezi kukurudishia kizazi chako lakini pia siwezi kukudanganya kuwa sitaki mtoto, namhitajisa na na nahitaji kuwa na familia. Mimi naona tu uondoke, sinakinyongo na wewe lakini siwezi kuishi na wewe tena, siwezi kuigiza tena.
Aliongea taratibu sana, macho yake
yalionyesha kuwa alikuwa anamaanisha alichokuwa akikiongea na hakuwa
tayari kurudi nyuma. Nnilimuangalia mara mbili nikajua hakuna kitu
ambacho ningesema kitakachoweza kubadilisha maamuzi yake. Nilijikuta
nasema tu “Sawa” basi sikuonge aneno lolote, hata alipotaka kugawana
mali, sijui kunipa gari na vitu vingine nilimuangalia tu.
Akili yangu nika ilifunga, sikutaka
kuchukua chochote. Siku iliyofuata nilikusanya kila kitu nilichokuwa
nimenunua na hela yangu na kuondoka, alijaribu kunisihi tugawane kila
kitu lakini nilikataa, nilitaka kuanza maisha yangu upya bila yeye. Sasa
hivi naishi mwenyewe na nina jaribu kutafuta furaha tena, sihitaji tena
mwanaume najikita kwenye kazi.
Tupo kwenye mchakato wa talaka rasmi ya kiserikali, ndugu hawajui sababu lakini wanahisi tu labda yeye ndiyo alinipiiga ingawa nawakatalia. Nimeamua kumsamehe kwaajili ya amani yangu mwenyewe na namuombea Mungu furaha katika mahusiano yake mapya, namuombea mwanamke mwenzangu yasijekumkuta kama yangu na naamini kama ana akili amejifunza hawezi kupiga mwanamke tena.
Najua siwezi kuzaa lakini hiyo
haimaanishi kuwa siwezi kuwa Mama, kuna watoto yatima wengi wapo mitaani
wanatafuta wazazi na mipango yangu sasa ni kutafuta pesa ili
nikifikisha miaka 33 niwe na nyumba yangu na maisha mazuri ya kuweza
kulea watoto wawili ambao nina mpango wa ku wa ‘adopt’ kuwa wangu
kabisa.
Kuhusu wanaume nadhani kwa sasa sina
hisia kabisa, nikiwaona nawaona kama wanawake wenzangu tu, siwachukii
lakini sina hamu nao. Sababu ya kuamua kushea maisha yangu ni ili
mabinti wadogo wajifunze kuwa huwezi tu kumbadilisha mtu tabia, vumilia
kila kitu ila kama anakupiga usivumilie, usiingie kwenye ndoa ukadhani
unaweza mbadilisha mwanaume ni ngumu, mwanaume hubaidlika pale anapoamua
kubadilika yeye mwenyewe.
Najua unapokuwa katikati ya mapenzi
huoni, macho hufungwa na kujipa moyo kwa kuangalia mazuri yamwenza wako
ila usiwe kipofu kuona yaliyowazi. Ana wanawake wengi unamvumilia tena
anakuonyesha na haoni kama ni kitu kibaya, anakupiga unavumilia, siku
akikuvunja mguu au kukupa ulemavu wa kudumu ndipo utajutia kama mimi
atakucha kwakuwa hutakuwa na vigezo ulivyokuwa navyo awali vilivyomfanya
akupende.
No comments:
Post a Comment