Dakika chache za kwanza tunapokutana na wapenzi wetu baada ya kuachana kwa kitambo kifupi zinaumuhimu sana.
Kitambo hiki ni kile ambacho labda mpenzi wako alikuwa kazini au
safarini, umepita muda fulani hamjaonana, yamkini moyoni ulitamani
kumwona au hata kule kuhisi kumkosa (kummiss) kulishaanza kupoa, jiulize
mara utakapomwona, labda ni uwanja wa ndege, kituo cha basi, au
amefungua mlango tu kuingia nyumbani. Je unafanya nini?. Kile utakaco
kifanya hapa kina nafasi kubwa katika kuua taratibu penzi na ukaribu
wenu (intimacy) au kulijenga kwa kasi kubwa. Ni uchaguzi wako, ingawa
unashauriwa kufanya haya yafuatayo.
1. Jiandae wewe mwenyewe kiakili
Kabla
hamjaonana uso kwa uso andaa vema akili yako kumlaki mpenzi wako.
Fikiri mawazo mazuri na siyo yaliyo mabaya kumhusu yeye. Usiwaze
kumwagia lawama mara tu utakapomwona. Wengine mara tu wamwonapo mpenzi
ameingia huanza kukurupuka kuuliza kama
kaja na zawadi, na ole wake ukute kasahau huo moto utakao waka hapo!
Panga nafsini mwako kitu au tukio la kufurahisha utakalomfanyia mara
ukimwona. Mara nyingine unaweza kumuuliza kwa simu muda atakapowasili
ili uweze kujiandaa vile unavyodhani.
2. Jiangalie muonekano wako
Dakika
ya kwanza tu mnapotazamana yaweza kuathiri muendelezo mzima wa siku
yenu. Muonekano wako wa uso, tabasamu lako, harufu yako (nzuri au
mbaya) vyaweza kumdaka au kumkimbiza mpenzi wako, haswa yule wa kiume.
wanaume pia nao wanachakufanya hapa, haupaswi kupokewa ukiwa rafurafu,
mchafu, unatoa harufu mbaya ya mwili au ya viatu. Jiangalie, nywele na
ndevu zako zikoje, meno yako yanaonekanaje na hata ngozi yako hususani
ya usoni. Mwonekano wako huzungumza zaidi vile unavyojiona wewe
mwenyewe. Hauhitaji kusema mimi sijipendi, bali kuonekana kwako kutatoa
ujumbe. Jaribu uwezavyo kuwa mwenye mvuto mara mtakopokuwa na
umpendaye.
3. Onyesha tabasamu la pendo kwa mpenzi wako
Panga
muda wako ili uweze kumsalimu mpenzi wako kwa tabasamu. Acha mpenzi
wako ajue kuwa yeye ni wa kipaumbele, na ni muhimu kwako, usimpokee kwa
staili ya kumwonyesha humjali. Tabasamu linaweza kusema “I love you”
kuliko hata maneno au zawadi. Tabasamu halina gharama yoyote, ni la
bure na lipo wakati wowote, kinachokushinda kulitumia ni nini?
Hata
kama hujisikii kutabasamu, jitahidi kwa nama yoyote kuonyesha kuwa
unaweza pia kutabasamu. Jifanyishe pale mazingira yanapolazimu,
hususani katika dakika nne za mwanzo. Ikiwa utajifanyisha vizuri, hisia
njema zaweza kuibuka na yale maumivu ya ndani ya moyo kutoweka
taratibu.
4. Salimianeni kwa kukumbatiana na kwa busu
Kuwa na mtu anayetusubiri mara tutakapofika sehemu au mara tutakapofungua mlango ni jambo ambalo wengi wetu tunalipenda, kamakubusu
sio mtindo au pendeleo lako basi tafuta njia nyingine ya miili yenu
kugusana mara mnapoonana. Mfano kushikana mikono, kumshika mwenzako
nywele au kichwa, nk. Mgusano wa mwili ni muhimu na unashauriwa kwa afya
ya penzi lenu.
5. Tengeneza mazingra mwanana
Jipeni
muda wa kupumzika na kupumzisha akili kabla ya kuanza kuzungumzia
matatizo yenu. Kila anayeingia nyumbani nakukuta anapokelewa na makelele
na mikiki mikiki mara nyingi hutamani kuondoka.
Kila
anayekuwa nyumbani kwanza kabla ya mwenzake anawajibika kutengeneza
mazingira ya hisia nzuri, ingawa baada ya hapo wote wawili pia mnawajibu
wa kuendeleza hisia hizi njema na mazingira ya amani yaliyopo.
Wale
ambao wanafanya kazi nje ya nyumbani huhitaji utulivu kidogo mara
wanaporudi ili kutuliza akili na hisia zao, wengine watataka dakika 15
wengine dakika 20, watataka kujinyoosha kidogo, au kusikiliza muziki
fulani bila maongezi mengi, ingawa pia wapo wanaotaka kucheza na watoto
mara wanapofika nyumbani. Chochote na kwa hali yoyote uipendayo,
jaribu kujielezea, na mueleze mwenzako aelewe mtiririko wa hisia zako,
hii itawasaidia sana.
Na: Chris Mauki, PhD
Relationship, Social and Counseling Psychologist
University of Dar es Salaam
chrismauki57@gmail.com
No comments:
Post a Comment