Mara
nyingi wapendanao huwa na njia mbali mbali wanazozijua wao katika
kukorofishana au kusuluhishana pale walipo korofishana. Labda njia au
staili hizi wameamua na kudhamiria kuzitumia au yamkini zimejijia tu na
kujikuta wanazitumia. Jinsi unavyotofautiana, au kugombana wewe na
mpenzi wako yamkini ni tofauti na vile rafiki yako afanyavyo na mpenzi
wake. Aina hizi hamjifunzi shuleni, hamfundishwi na wazazi wala maeneo
ya ibada. Ni wewe kuzitilia mkazo na kuzielewa sasa.
Ingawa
aina hizi za migongano zinatofautiana baina ya watu na watu na
hazifanani, watafiti wa sayansi ya jamii wamejaribu kuziweka katika
makundi matano yafuatayo:
1. Washindani (Competitors)
Watu
wa aina hii mnapotofautiana kidogo hupayuka kwa sauti kama vile mko
katika vita, wengine hulia kwa sauti. Kiu na lengo lao ni kushinda vita
hiyo na kukunyamazisha wewe uliyetofautiana nao. Wao hujijali zaidi
wenyewe na sio kumjali hata kidogo yule wa upande mwingine. Matakwa yao
daima ndiyo yakuwekwa mbele na siyo ya mtu mwingine yeyote.
2. Waepukaji (Avoiders)
Mara
nyingi mkitofautiana na watu wa jinsi hii na mkataka kukuzungumzia kile
kitu kilichokuwa kwazo utasikia wakisema “sitaki tuliongelee hilo
jambo” au “Usinikumbushe hayo”, au “ hayo yameshapita yanini
tuyakumbushie tena”. Watu hawa huweza kuzuia vile wavipendavyo au
kuvitamani na pia hawahusiki sana na matamanio ya wapenzi wao. Mfano;
kama yeye hapendi maua au mitoko, hajali hata kama wewe unapenda maua au
mitoko. Wakati ugomvi au kutofautiana kunapo zidi basi kusitisha
kuzungumza na kuamua kukaa kimya kwa lolote lile hali ambayo huleta
ugumu kwa mpenzi mwingine kwa kutojua nini mwenzake ana maanisha au
anahitaji. Watu wa jinsi hii kuzira ndio wataalam. Magomvi ya staili hii
hudhuru sana ukaribu (intimacy) baina ya wapendanao na ni hatari sana
kwa sababu ni rahisi kuua au kuvunja ndoa, au mahusiano.
3. Walazimisha muafaka (Compromisers)
Hawa
ni wale wanaolazimisha muafaka kwa kuweka mazingira yao binafsi. Hawa
mara nyingi mnapotofautiana na mnataka kumaliza tofauti zenu waweza
kusikia wakisema “mimi ntafanya hivi kama na wewe utafanya vile”,
“Usipofanya hivi na mimi sifanyi vile” Wapendanao wa jinsi hii hujijali
zaidi wao binafsi kuliko wanavyo wajali wenzao. Wale wanaouwezea
mgongano wa staili hii huweza kupunguza kwa kiasi kikubwa tofauti zao
lakini kwa kushusha kiwango cha mahitaji yao ili kila upande uweze
kutosheka kidogo kidogo.
Mfano
nimewahi kupata kesi ya wanandoa waliotofautiana sana juu ya suala la
kumhudumia mtoto baada ya kurudi kazini, wote wamechoka na baba alikuwa
analala sana usiku pasipo msaada wowote. Wakalazimika kukubaliana kwamba
mara wakirudi, baba atashuhughulikia kila kitu kinachomhusu mtoto hadi
muda wa kulala, na usiku wote, baba hatabugudhiwa, maana ni zamu ya
mama, hapa vita ikapoa, na kwa aina hii ya suluhisho nikagundua kuwa
watu hawa ni compromizers.
4. Washiriki (Collaborators)
Watu wa jinsi hii hutumia ile filosofia kwamba “kama huwezi kupigana nao basi jiunge nao” (if you can’t beat them join them). Hawa wanafanya tofauti na waepukaji (avoiders)
Hawa hukimbilia makubaliano yenye kutafuta suluhisho, na mara nyingi
katika kutafuta kutosheleza mahitaji ya pande zote mbili. Mara kwa mara
hujiona na kujihisi wanaoweza nahii hujionyesha katika jinsi wanavyojali
maslahi yao na ya wenzao. Malengo ya watu wa kundi hili sio ushindi
katika tofauti zenu bali kuhakikisha kila mmoja anaridhika.
5. Wasaka amani (Accommodators)
Hawa ni wale
watafutao amani kwa gharama yoyote, na hili ndilo lengo lao. Wanavutiwa
sana na kuhakikisha amani inarudi, na katika kufanya hilo huweza
kusamehe mahitaji yao, kuwaridhisha wanaowapenda.
Hawa
ndio wale unaowasikia wakisema “kama hili gari ndilo linaleta tabu basi
wewe lichukue tu ili mradi tuishi vema”. Staili hii ni kinyume na ile
ya washindani (competitors). Watu wa kundi hili huingia katika
migongano na wapenzi wao lakini mwisho wake kujitoa, hughairi ili tu
kuitafuta amani. Huwa tayari kuyazika matakwa yao kwasababu tu ya furaha
ya mwingine.
Ukiukuta ugomvi wa washindani utaishia:-
- Toka kwangu, acha kila kitu hapa, na kununulia, nakulisha, nakuvisha, nimekutoa mbali sana, kwanza jiangalie ulivyo sikuhizi, hukua hivyo wewe, nimekupendezesha sana tu.
- Nachukua kila kilicho changu hapa, mambo mengine utajua wewe mwenyewe.
- Tugawane sawa kwa sawa, kwanza wote tumetafuta hapa.
- Tutajua haki iko wapi hapa, na lazima mwenye haki ajulikane.
- Wako tayari kukata nusu picha mlizopiga pamoja ili tu mgawanyike, nakila mmoja aondoke na kipande chake.
Ukikuta ugomvi wa wasaka amani au accommodators
- We chukua kila unachokitaka tu mi niko sawa na hilo.
- We fanya kile unachokiona ni sawa mimi haitonisumbua sana.
- Wala usipate shida kutoka, mimi nitakupisha hapa.
Kila
mmoja wetu anastahili yake aliyoizoea, ingawa maranyingine hubadilika
kutoka moja kwenda nyingine. Tafiti zinaonyesha kuwa muunganiko wa
makundi yaliyotajwa hapo juu (Collaborators, Compromisers, na Accommodators) huzaa mahusiano mazuri ambayo huweza kudumu kwa muda mrefu.
Ni
dalili ya kuwa mtu mzima pale mnapotofautiana katika mambo ya msingi na
sio kukwaruzana na kupigana kutwa kucha kwa vijimambo visivyo na tija.
Kama kuna kitu cha muhimu na unachokiamini kimepingwa basi kipiganie na
uachane na vijimambo vidogo vidogo. Wakati wote kumbuka kuwa hekima
hupunguza wingi wa hasira. Najua kuwa wote tuna nishati nyingi tu
miilini mwetu, tuzitumie nishati hizi katika yale yatakayokuza na
kuujenga ukaribu wetu na siyo yale yatakayo ubomoa.
Imeandikwa na :
Chris Mauki. PhD
Social, Relationship, and Counseling Psychologist
University of Dar es Salaam
chrismauki57@gmail.com
www.chrismauki.com
No comments:
Post a Comment