Kama
mwenza wako ana tabia ya asili yoyote ile unayoihisi au kuifahamu,
inakupasa kuwa makini naye kwani tabia hiyo au hizo zinaweza kukuathiri
kisaikolojia au kimazingira.
Inaweza kukuathiri kisaikolojia kwa maana ni tabia ambayo ni ngumu kuiondoa katika
damu ya mtu ambaye amezaliwa na tabia hiyo, hivyo itakulazimu kutumia
muda mwingi katika kutafuta njia mbadala ya tabia asili ya mwenza wako.
Yawezekana ikawa ni vigumu kufahamu ni kwa namna gani unaweza kulizoea
tatizo lake na kuishi naye katika uhusiano wa kimapenzi. Ila kama
ulimpenda kwa dhati na hukulazimishwa kuwa naye, basi jifunze kumzoea na
kuepuke baadhi ya tabia hizo.
Kwa upande wa kimazingira, tabia ya asili inawezekana kuwa ni mwenza
wako kuwa mkorofi, mmbeya, malaya na kadhalika, jambo ambalo laweza
kukugombanisha na wazazi, ndugu, majirani na hata marafiki zako, kwani
kila kukicha kesi za ugomvi mtaani zitamhusu mkeo au mmeo, mara kapigana
na fulani, katukanwa na fulani au unahisi katembea na Kulwa au Zulfa wa
nyumba ya pili.
Kiukweli tabia za asili ni ngumu kuzizoea au kuziishi ila kwa kuwa
umeshaamua kuwa mwili mmoja, huna budi kukubaliana na tabia hizo ili
maisha yasonge.
Kwa ushauri wangu, ni vyema vijana wa sasa wakawa wazi katika maisha ya
uchumba na kuishi maisha halisi na kwa muda, tena mkiwa karibu. Hii
itasaidia kuzifahamu baadhi ya tabia za asili za umpendaye.
Kwa kuzifahamu, itakusaidia kufahamu ni kwa namna gani utaishi naye na
kama ikitokea akakukwaza, basi utajua ni kwa namna gani utamvumilia au
kumtuliza na maisha yakaendelea.
Uhalisia wa maisha ni eneo muhimu mno katika uhusiano. Kama kweli ni
muungwana, jiachie, acha kujifanya ni mstaarabu ilihali wewe siyo
mstaarabu, acha kujifanya unawapenda ndugu wa mwenza wako wakati moyoni
unawachukia. Huo ni unafiki na ni maisha ya kuigiza ambayo ipo siku
yatakushinda.
No comments:
Post a Comment