KARIBU tena jamvini mpenzi msomaji wangu wa makala za XXLove kwa ajili
ya kupata chakula cha ubongo ili uelimike na kudumisha uhusiano wako wa
kimapenzi na maisha yako ya kila siku.
Mada yangu ya wiki mbili mfululizo zilizopita juu ya ulazima wa kulifanya penzi
lako kuwa hai (up date) iliibuka mjadala mkubwa. Wengi walionipigia
simu na kunitumia SMS walikiri kukosea katika vitu vidogovidogo lakini
pia waliwatupia lawama wenza wao.
Nilichowashauri ni kwamba wafanye wanachokiamini kwa vitendo ili kulinda
uhusiano wao na kuwaachia wenzi wao wakijitathimini. Ipo siku wenzi wao
nao watajishtukia kuwa kuna kitu wanakosea. Siyo vema mmoja
anapojisahau na mwingine naye ajifanye amejisahau kwani wote mtatumbukia
shimoni.
Baada ya kusema hayo, turudi kwenye mada ya leo ambayo nitawazungumzia
baadhi ya wapenzi au wanandoa wenye tabia ya kulumbana, kupigana,
kuchuniana mara kwa mara hadi kufikia hatua ya kulala mzungu wa nne,
kutengana vitanda au hata vyumba vya kulala (kama Mungu amewabariki kuwa
navyo).
Hebu tujiulize, hivi inakuwaje wapenzi mnagombana na kuanza kutengeneza
mipaka ya kugawana vyumba au vitanda? Hivi mlioana ili mgawane vitu
hivyo? Msema kweli ni mpenzi wa Mungu kama anavyosema Rais John Pombe
Magufuli, nami nasema kweli, kufanya hivyo si sahihi hata kidogo.
Hata kama mmekwazana, si sahihi kugawana vitanda au vyumba kwani kwa
kufanya hivyo ni kutengeneza au kuhalalisha uchepukaji miongoni mwenu.
Jifunze kuwa na hasira za muda. Hasira ambazo baada ya muda, utazifuta
na mwenzako atajua umezifuta na maisha yanaendelea kwa vicheko kama
kawaida na hata chakula cha usiku mnaendelea kulishana kama kawaida.
Jamani tukubaliane kuwa ndoa ni tamu.
Ila kama mtashindwa kusomana na kujuana tabia zenu, basi mtaiona chungu
kama shubiri. Kikubwa ni kila mmoja kumjua mwenza wake hapendi nini na
anapenda nini. Lakini pia wapenzi au wanandoa mnapaswa kuvumiliana
kwenye shida na raha kama ambavyo mliapa.
Sasa kwa nini mshindwe kuvumiliana kwa sababu ya misukosuko ya hapa na
pale ambayo inapita? Usikubali kumkimbia mpenzi wako au kuhama kitanda.
Kama unaona umemkwaza au amekukwaza, basi jitahidi kufanya juu chini
kusawazisha mambo, kumfanya mwenzi wako awe na amani, upendo na furaha
kama mwanzo. Siku zote hakikisha uhusiano wako unakuwa wa amani na
furaha.
Tumia nguvu na akili yako yote kumshawishi na kumridhisha mwenzako kuwa
kile ulichokifanya ni kosa na kwa kuwa unampenda, hauko tayari kumuudhi
kwa kurudia kosa kama hilo.
Mkiwa na tabia ya kugawana vitanda au vyumba, mnaweza kujikuta
mnashindwa kujizuia baadhi ya mambo na yawezekana ikawa ni rahisi kwa
kuchepuka kwa sababu hali hiyo inatoa nafasi ya kutengeneza mazingira ya
usaliti. Haipendezi, mnadhani mnatoa picha gani kwa watoto wenu wa
kizazi hiki cha sasa ambao wanafahamu kila kitu kinachoendelea, tofauti
na watoto wa kizazi cha miaka ya nyuma? Ni matumaini yangu nimeeleweka
na makala hii utaitumia kama tiba ya tabia hiyo kama inakuhusu wewe au
mwenza wako. Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine murua.
No comments:
Post a Comment