Mimi ni binti wa miaka 22, sifanyi
kazi yoyote na nipo tu nyumbani. Tatizo langu ni huyu mpenzi wangu,
tumekuwa naye kwenye uhusiano kwa miaka miwili na na mpenda sana ingawa
mwenzangu kabadilika yaani hata sijui nianzie wapi, kila nikiwaza
nachanganyikiwa kabisa.
Yeye ni mtu mzima kidogo kuliko mimi
ana miaka 30, anafanya kazi na ana kipato kizuri tu. Mwanzoni alikuwa
akinipenda na kunihudumia kwa kila kitu, kwakuwa alikua tayari
ameshajitambulisha kwa wazazi wangu basi tulikuwa huru sana na mara
nyingi nilikuwa nikienda kulala kwake na kusema kweli tulikuwa tukiishi
kama mke na mume.
Lakini mwaka jana alibadilika sana,
akawa hanijali tena kama awali na nikawa nikienda kwake anakasirika sana
au anatafuta sababu za kuniambia niondoke kwakuwa ana mambo mengi au
wageni ambao hataki nionane nao. Basi niliamua kuvumilia lakini
nikichunguza sababu za yeye kubadilika, huwezi amini niligundua anatembe
na rafiki yangu mkubwa ambaye tulikuwa kama mapacha tukielezeana kila
kitu.
Nililia nusu kuchanganyikiwa,
nilipomuuliza alikiri na kunijibu maneno ya kashfa. Lakini kwakuwa
nilimpenda nilimsamehe ingawa hata hakuomba msamaha. Ili kulilinda penzi
letu niliamua kumtegeshea mimba kwani nilijua anahitaji sana mtoto mara
nyingi huongea hivyo na kweli alipojua kuwa mimi ni mjamzito
alibadilika na kurudia kwangu, alikuja kwetu kutoa mahari na mimi
nikahamia kwake moja kwa moja wakati tukijipanga kufunga ndoa.
Samahani kwa maelezo mengi lakini sijui namna ya kufupisha. Baada ya kuendelea kuishi kwake hakuendelea na maandalizi ya harusi wala nini aliishia kutoa tu mahari na kukaa kimya, nikimuuliza anasema ngoja kwanza afanye maandalizi ya mtoto kwakuwa mtoto anahitaji gharama kubwa na harusi nayo inahitaji gharama kubwa, nikishajifungua ndipo tutafunga ndoa. Nilimuelewa kwakuwa alionekana siriasi na alishaniahidi kuwa kaachana na yule rafiki yangu.
Lakini kumbe nilikuwa najidanganya,
wiki iliyopita nilifumania meseji anachat na rafiki yangu, kumbe yule
rafiki yangu baada ya kuona kuwa mimi ni mjamzito nayeye bila aibu
alibeba mimba, mimi nina mimba ya miezi mitano yeye ana mimba ya miezi
miwili. Nililia sana nusu kuchanganyikiwa, sikutaka kumuambia lakini kwa
hali niliyokuwa nayo alijua kuwa nimejua na hapo ndipo ugomvi
ulipoanzia.
Hatukuwa tukizungumzia tena kuhusu
mimba ya rafiki yangu bali kuhusu mimi kuchungulia simu yake.
Alikasirika sana na kuanza kunipiga, alitoa vitu vyangu nnje na
kunifukuza akisema hawezi kuishi na mwanamke kama mimi ambaye siheshimu
vitu vyake. Kama utani nilifukuzwa na kuamua kurudi nyumbani na ndani ya
siku mbili tu yule rafiki yangu alihamia kwake na walianza kutangaza
kuwa wanaoana.
Nimeumia sana yaani sijui hata
chakufanya, nyumbani kwetu hali duni naishi na Mama na wadogo zangu
ambao wote hawana kazi ya kufanya. Sijui nini kilinikuta nilijikuta
nawaza kuitoa hii mimba mbayo sasa ina zaidi ya miezi mitano kuelekea
sita. Watu wananiambia nitakufa lakini sina namna sina hata pesa,
mwanaume simu hapokei na nikienda kwake namkuta yule rafiki yangu ambaye
hunitukana na kuniambia kiko wapi nilikuwa naringa yeye amemuwekwa
ndani na simtoi.
Naona kama yule mwanaume si akili
yake kalishwa dawa kwani mimi ni mzuri zaidi na alikuwa akinipenda mimi,
naomba ushauri wako kwani nikisoma post zako unaonekana kama mtu
muelewa unayeweza kunisaidia. Nataka nitoe miamba klakini sijui kama
itatoka Mama anataka kunipeleka kwa mganga wa kienyeji ili yule mwanaume
arudi kwangu, sijui nifanye nini. Nisaidie nipe uelekeo sijui hata
pakwenda, sina kazi sina chochote.
JIBU LA MAHUSIANO LIVE;
Kwanza pole sana na yaliyokukuta
natamani kutiririka sana hapa lakini kutokana na hali yako na ulipofikia
sitaki kufanya hivyo. Nikuambie tu hali uliyonayo inawakumba wasichana
wengi, ambao hudhani kwa kubeba mimba au kumzalia mwanaume ndiyo kuweza
kumshika, ndiyo tiketi ya kuelekea kwenye ndoa. Ukweli nikuwa mwanamme
anayekupenda hahitaji mimba ili kukuoa au kuwa na wewe.
Najua kwa hali uliyonayo unapitia
machungu mengi lakini huu si muda wa wewe kupaniki. Kwanza nianze na
suala la kutoa mimba, hakuna dhambi mbaya kama hiyo, ingawa wasichana
wengi huona kitu rahisi lakini usijaribu, tena kwako hali ni mbaya zaidi
kwani mimba ni kubwa, miezi mitano hiyo mtoto ashakuwa mkubwa unaweza
kutoa mimba na wewe ukafa.
Nimesisimkwa kuona unaweza kufanya
kitu kama hicho, hata kukiwaza tu, naomba pepo hilo baya likutoke. Kila
mtoto huja na baraka zake na wala usiwaze kuhusu namna ya kumlea. Miezi
mitano ni mimba kubwa sana nikama unaua mtoto mkubwa, nakushauri
usifanye
Kuna mamilioni ya watu wanahitaji watoto huna haja ya kuingia kwenye dhambi hiyo. Kuhusu kwenda kwa mganga achana na mawazo hayo, huyo mwanaume hajalogwa wala nini? Hakupendi na acha kujishusha kiasi hicho. Umrembo sana nina hakika utajifungua salama mtoto mzuri acha kujidhalilisha kwa mwanaume ambaye hakujali.
Hata ukimloga mara mia mbili hawezi
kuwa wako kama hakupendi hakupendi tu atakuja kwako kwa muda
atakuzalisha tena na kukuacha. Shukuru Mungu kakuonyesha sura yake
mapema kabla ya kuingia kwenye ndoa. Kuwa single mother ni kitu cha
kawaida kabisa, huna haja ya kuumiza kichwa. Pole sana yameshatokea, jua
tu mwanaume hashikwi kwa mimba, kama kakupenda kakupenda tu hatajali
kama una mimba au hata unauwezo wa kuzaa atakuoa tu na kuwa na wewe.
Kwa bahati mbaya sana mabinti wengi
huingia katika mtego huu wa kulazimisha mimba ili kupata tiketi ya
kuolewa. Nikweli anaweza kukuoa lakini asiwe Mume wako, Mume ni zaidi ya
kukubaliana kanisani na msikitini kuwa mnaoana. Anaweza kukuoa ukawa
umeingia kwenye ndoa ya mateso na halitakuwa kosa lake kwani moyo wake
haukuwa kwako tangu awali.
No comments:
Post a Comment