Nilirudi nyumbani nikiwa nimechelewa
sana na kama kawaida nilijua siku hiyo ilikuwa ni kipigo tu, kusema
kweli nilikuwa nimechoka, sikuchoka kwa kipigo bali nilichoka kutokana
na kazi nilizokuwa nimefanya siku hiyo. Nikisema kazi simaanishi kazi
zile za ofisini, hapana, mimi si mfanyakazi, si kwamba si kusoma hapana,
nina shahada yangu mfukoni ambayo niliisotea mika mingi darasani.
Baada ya kuolewa na kupata mimba nikiwa
bado sijapata kazi basi niliamua kumlea mwanangu kwanza na baada ya
mtoto kuwa mkubwa nilipotaka kutafuta kazi mume wangu alikataa. Kama
wanaume wengi aliniuliza “Kwani unakosa nini hapa? Au unataka uende
ukafanye umalaya wako huko?” Kusema kweli sikuwa nikikosa chochote kwani
mume wangu ni mtu mkubwa sana serikalini.
Kwakuwa nilikuwa nikipata kila kitu basi
hata sikusisitizia sana kuitafuta hiyo ajira, nilivumilia tu na Mungu
akajaalia nikapata mtoto wapili na watatu. Miaka kumi na mbili kwenye
ndoa sasa na tangu siku ya kwanza kuna vitu vingi vimebadilika kasoro
kitu kimoja tu, kupigwa karibu kila siku ya Mungu.
Nilivumilia kupigwa mpaka kufikia hatua
ya kuona kama kitu cha kawaida, nikaanza kuona kama sehemu ya majukumu
ya ndoa, kupigwa. Mpaka sasa bado naona hata aibu kuvua nguo mbele za
wanawake wenzangu kutokana na mistari ya mikanda, fimbo na makovu ya
maumivu ya kila siku. Lakini kama walivyo wanawake wengi ambao wako
kwenye hali kama yangu nilikuwa navumilia kila siku nikikesha nikiomba
labda Mungu atambadilisha lakini wapi?
Sitaki kuelezea sana niliyopitia lakini
niseme tu Mume wangu hakuanza tu kunipiga baada ya ndoa, hapana alikua
akinipiga hata kipindi cha uchumba. Yaani kila nilipokuwa nikimfumani
alinipiga na kuniomba msamaha. Hapa pia naomba mnielewe ninaposema
kupigwa simaanishi kupigwa makofi mawili matatu, namaanisha kupigwa kama
mbwa.
Lakini nilikuwa nampenda na nilivumilia
na kila mara aliniahidi kubadilika lakini ilimchukua muda sana
kubadilika na kuacha kunipiga. Tuachane na hayo turudi katika siku
ambayo sitakuja kuisahau katika maisha yangu yote na siku ambayo
naijutia na iliyonilazimisha kuandika hiki ninachoandika ili kama na
wewe uko kwenye hali kama yangu usisubiri ya kukute ndiyo ujutie.
******
Siku hiyo nilikuwa nimechoka sana kwani
baada ya kumkaliza shughuli za pale nyumbani nilipigiwa simu kuwa Mama
anaumwa, alikuwa amelazwa Muhimbili akishindwa kupumua. Alikuwa na pumu
ya muda mrefu hivyo harakaharaka nilienda kumuangalia. Mchakato wa
kuhangaika na madaktari, mchakato wa kuenda kutafuta dawa mji mzima
ulinifanya kuchoka sana.
Nilijaribu kumpigia simu mume wangu ili
kumuambia lakini hakupatikana hivyo nilimtumia meseji kuwa Mama anaumwa
na kalazwa Muhimbili. Sikukumbuka tena kumtafuta kwani akili haikuwepo,
mpaka usiku ule wa saa tatu natoka Muhimbili mume wangu alikuwa bado
hajanipigia simu na kila nikimtafuta kwenye simu yake alikua hapatikani,
sijui kwanini lakini laini zake zote mbili zilikuwa hazipatikani.
Kwa maana hiyo nilijua kua alikuwa
hafahamu kuhusu Mama hivyo nikifika nilikuwa na kazi ya kujielezea na
kama asingeelewa nilishajiandaa kwa kipigo. Nilifika nyumbani na
kufunguliwa na mfanyakazi wa ndani, mume wangu alikuwa chumbani, tangu
saa kumi na mbili aliporejea na kunikosa aliingia chumbani na hakukuwa
na mtu wa kumsemesha.
Mtoto wangu wa mwisho wa miaka mitatu
ambaye bado alikuwa hajaanza kumuogopa Baba yake ndiyo alikuwa anaweza
kuingi chumbani lakini naye alikuwa ameshalala hivyo alikuwa apeke yake
tu huko chumbani. Niliingia kwa uoga na kumsalimia lakini hakujibu.
“Nilikuwa muhimbili Mama anaumwa kalazwa…” Ilibidi nijiongeleshe tu ili
ajue asbabu ya mimi kuchelewa.
Lakini haikusaidia aliendelea kukaa
kimya akisoma kitabu chake ambacho hata sikumbuki kilikua kitabu gani.
Nilivua nguo harakaharaka ili kuingia bafuni kuoga, lakini nikiwa
nimefunga khanga moja nilimuona akisimama.
“Huyo Mama yako ndiyo amekuoa, inamaana
unaweza kuondoka humu ndani bila ruhusa yangu? Umefundwa wewe?
Unajifanya sijui ujinga unaofanya unajifanya umetoka Hospitali!
Hospitali kitu gani?” Alianza kuongea kwa hasira, nilianza kujitetea
lakini ndiyo nilikua nimeuwasha moto, alianza kunipiga makofi na
kunisukuma, nilidondoka chini alinifuata kulekule na kunishika nywele
zangu ndefu akaanza kuzivuta kunisimamisha.
Maumivu niliyoyapata siwezi simulia,
kama ni mwanamke unasuka rasta unajua ni namna gani kcihwa kinauma na
kuvuta unaposuka tu sasa hembu vuta picha mtu anashika nywele zako na
kukunyanyua juu juu kama karatasi. Nilishindwa kuvumilia, nilipiga
kelele huku nikimsukuma, ingawa ikumsukuma kwa nguvu lakini aliteleza na
kudondokea kitandani.
“Unanipigaee! Yaani unanirudishia!
Umeota mapembe eeeh! Sasa ngoja nikuonyeshe!” Aliongea kwa hasira akiwa
bado palepale kitandani, alianza kuvua mkanda huku akiangalia ni kitu
gani kingine rahisi cha kuokota na kunipiga nacho, sijui kwanini lakini
nilijikuta naanza kukimbia kuelekea sebuleni. Haikuwa kawaida yangu mara
zote huwa akinipiga nakimbilia chumbani ili watoto wasione lakini siku
ile nilikuwa nimechoka na nilijua kipigo chake kitakua cha mbwa.
*******
Alinifuata kule kule sebuleni na wakati
nikipita nikiijaribu kufungua mlango wa nnje ilinitoke alishanifikia,
alianza kunipiga makofi na kunichapa kwakutumia mkanda. Nilikua nikipiga
kelele lakini hakukuwa na mtu wa kunisaidia. Nilikuwa na mfanyakazi wa
ndani ambaye ni binti mdogo alikua anogopa, mwanangu wa kiume Fred ndiyo
kwanza alikua na miaka kumi akifuatiwa na kabinti ka miaka sita, wote
walikwa wamesimama wanaangalia tu huku wakilia.
Alinivuta na kunidondoshea kwenye kochi,
kanga moja niliyokuwa nimejifunga ilivuka na kubaki kama nilivyozaliwa
hakujali, aliendelea kunipiga makofi akiniinamia pale huku akipiga
kelele kuwaambia watoto waingie ndani lakini Fredrick mtoto wangu
hakukubali. Namaani alishachoka ile hali ya mimi kupigwa pigwa kila
siku, sijui alipata wapi ujasiri lakini alienda na kuokota blenda ambayo
ilikuwa juu ya meza ya chakula alikuja nayo kwa kasi na kumpiga Baba
yake mgongoni.
“Muache Mama! Utamuua Muache…” Alionge
akwa hasira huku akitaka tena kunyanyua kumpiga Baba yake, lakini Baba
yake alishageuka aliikamata ile Blenda na kwa hasira alimrudishia
kumpiga na moja kwa moja ilimdondokea kichwani. Kimya Fred alidondoka
chini na damu kuanza kutiririka, mume wangu alibaki ameduwaa, nikiwa
uchi vilevile nilinyanyuka na kwenda kumuangalia, alikuwa hatikisiki,
macho yamemtoka, damu zinamtoka puami na mdomoni.
“Mume wangu umeua! Mume wangu umeua!”
Nilianza kupiga kelele kujaribu kumuamsha mwanangu lakini hakuamka. Mume
wangu nguvu zilimuishia na kukaa chini, hakusogea hata kumshika mtoto
kuuangalia mapigo ya moyo, machozi yalianza kumtoka kama mtoto mdogo.
Mfanyakazi alitoka nilimuamsha mume wangu ili tumpeleke mtoto
hospitalini ndipo alipozinduka na kunaynyuka kwenda kuwasha gari.
Nilitaka kutoka vilevile nikiwa uchi
mpaka mfanyakazi nitolea nguo nikavaa. Tulifika hospitalini na
kuambikuwa ameshafariki. Hospitalini sijui nini kilifanyika kwani
hakukuwa na cha PF3 wala nini, wakati huo akili yangu haikuwa sawa hivyo
sikujali mambo hayo lakini nilijua wakati tunajiandaa na mazishi. Kila
nilipowaambia watu kilichotokea waliniona kama kichaa kwani maelezo
yaliyotolewa kua mwanangu alifariki kwa ajali ya gari.
Sio maelezo tu bali pia mfanyakazi wa
ndani alisema hivyo hivyo, mashahidi wapekee niliokua nao ni mtoto wangu
wa miaka sita na mwingine wa miaka mitatu. Haiishii hapo gari
lililopata ajali lilikuwepo, sijui mume wangu alifanya nini lakini gari
lake alilokuwa akitumia lilikuwa limeboindekabondeka kama vile limegonga
mti.
Ili kuwaaminisha watu badala basi hata
ya kupelekwa gereji lilivutwa mpaka nyumbani na ndani kulikuwa na damu
zimegandia sijui hata zilitoka wapi kwani zilikuwa ni nyingi tena siti
ya mbele wakati tulitumia gari jingine kwenda hospitali. Ilinibidi tu
kunyamaza kwani nilijua hakuna namna ambavyo ningeweza kumfanya mume
wangu kulipa kwa aliyoyafanya. Hakuomba msamaha zaidi yua vitisho kuwa
nikisema ataniua huku akinitishia kwa kuwadhuru watoto.
Bado niko kwenye ndoa na sina pakwenda,
sipo kwaajili ya pesa bali kwaajili ya wanangu. Sijui ni nini kitatokea
kama nikiondoka kwani ameshakataa katakata kuniruhusu niondoke nao.
Nimwaka wa pili sasa tunaishi kama kaka na dada, sina furaha na
sitegemei kuipata. Nalea tu wanangu na nimeshakata tamaa ya maisha.
Nimeamua kuandika kisa changu hiki ili
wanawake wengine kujua kuwa unapokubali kupigwa na mwanaume hubebi
maumivu peke yako. Wanao wanaona hata kama unaficha vipi na unawaathiri,
wanakupenda na wanaumeia unavyoteswa kwani wewe ni Mama yao. Hembu wewe
fikiria mtu anampiga Mama yako halafu huwezi kumtetea utajisikiaje.
Simlaumu mume wangu kwa kifo cha
mwanangu, halikuwa Kosa Lake. Kosa lilikuwa la kwangu kuvumilia mateso,
kuona kipigo kama sehemu ya ndoa. Ningeondoka mapema, ningekataa kipigo
tangu siku ya kwanza haya yote yasingetokea. Nimejaribu sana kumlaumu
mume wangu lakini wapi, mkosaji ni mimi kwani mimi ndiyo nimevumilia na
kumlea.
Ingawa alianza kunipiga tangu kipindi
cha uchumba lakini hakuanza tu ghafla, alianza taratibu makofi ya hapa
na pale na kwakua nilikuwa nikimchekea na kujaribu kumtetea huko
kichwani mwangu, alizoea mpaka ikawa kitu kidogo tu haongei ni makofi.
Kama ambavyo wewe kila siku unavumilia, unasema ndiyo ndoa zilivyo,
unasema ipo siku atabadilika na mimi ndiyo hivyo hivyo nilikuwa
navumilia kabla na baada ya ndoa.
Siku hizi hanipigi, ameshabadilika
lakini haisaidii tena, haina maana tena kwangu kwani sina hisia tena za
mwanaume mwili nikama umepigwa ganzi. Pumzika kwa amani Fred wangu,
shujaa wangu uliyekufa ukinitetea, umekufa kifo ambacho hukustahili na
yote hiyo ni kwasababu ya mimi Mama yako. Naomba unisamehe, unisamehe
kwa kuvumilia ujinga, unisamehe kwa kujiangalia mimi bila kujua kuwa
nilikuwa nakuumiza wewe na wadogo zako, natumaini huko uliko utanisikia
na utanisamehe.
****MWISHO****
No comments:
Post a Comment