Wanawake wenye msongo wa mawazo “stress” huongezeka uzito kwa haraka sana kwasababu mfumo wao wa mmeng’enyo wa chakula “metabolism”kupunguza
uwezo wa kufanya kazi. Mtikiso wa mawazo juu ya kazi yako, watoto wako,
mpenzi wako, ndoa yako, mahusiano yako pamoja na marafiki zako
vinatosha kabisa kukuletea msongo wa mawazo wa hali ya juu. Kwa msongo
wa mawazo unaohusiana na mambo haya, wataalamu wanasema inaweza
kukuongezea uzito wa hadi kilo 6.3 kwa mwaka.
Watafiti
wa chuo kikuu cha Ohio huko Columbus Marekani walifanya utafiti
uliowahusisha wanawake 58 ambao uzito wao wa wastani ulikuwa kilo 53.
Kati ya maswali waliyoulizwa kwenye dodoso zao ni pamoja na kama
kinachowapa msongo wa mawazo ni pale wanapowaza juu ya ndoa zao, wapenzi
wao, marafiki zao, kazi zao, au watoto wao. Baada ya hapo wanawake hawa
walipewa mlo wenye mayai, soseji, biskuti, nyama za bata mzinga n.k.
Mlo huu ulikadiriwa kuwa na “calories” 930. Baada ya chakula hiki
wanasayansi hawa wakawapima jinsi miili yao ilivyokuwa inasaga au
kumeng’enya chakula na kiwango cha sukari mwilini mwao. Matokeo ya
utafiti huu yalionyesha kwamba wanawake walioelezea kuwa na msongo wa
mawazo kwenye kitu zaidi ya kimoja (baina ya watoto, kazi, ndoa, mpenzi
au marafiki) waliweza kuchoma (kupunguza) wastani wa “calories” 104
pungufu ndani ya masaa 7 tofauti na wale ambao walionyesha kutokuwa na
msongo wa mawazo (hapa inamaanisha uwezo wa mwili kuchoma virutubisho
visivyohitajika mwilini ni mdogo sana kwa watu wenye msongo wa mawazo
kuliko watu wasio na msongo wa mawazo). Kwa kipindi cha miezi 12 zaidi
hali hii inaweza kusababisha ongezeko la uzito la hadi kilo 5 kwa
mhusika. Wanawake wenye msongo wa mawazo wananafasi kubwa pia ya
kuongeza kiwango cha sukari mwilini ambacho kinachangia pia katika
kuhifadhi mafuta mengi mwilini. Zaidi ya hilo, wataalamu wanasema kwamba
mtu mwenye msongo wa mawazo hushawishika zaidi kula vyakula vyenye
mafuta mengi pamoja na vyakula vingine vyenye hatari kiafya, ambayo hii
huongeza uwezekano wa uzito kuongezeka zaidi. Kiongozi wa utafiti huu
Profesa wa saikolojia Jan Kiecolt-Glaser wa chuo kikuu cha Ohio anasema
kwamba kwa kula vyakula vibaya kiafya kama vile vyenye mafuta mengi,
vyenye wanga mwingi n.k uwezekano wa kuongezeka kwa uzito unakuwa mkubwa
kwasababu miili yetu hupunguza uwezo wake wa kuchoma “calories” na hivyo kuchoma chache zaidi ya uwezo wa kawaida.
Mtaalam
huyu ameeleza kwamba, ukiangalia chakula walichopewa wanawake hawa
hakikuwa kibaya sana ukilinganisha na vyakula ambavyo wengi wetu
tunakula pale ambapo tunaharaka ya kutaka chakula na hatutaki kupoteza
muda kupika. Wengi wetu hatuko makini hata tunaponunua chakula au
tunapokula kwenye sherehe mbalimbali, tunajitahidi kula kila kilichopo
pasipo kuwa makini kwenye nini tunakula, kimepikwaje, kimepikwa na nini,
na kipoje kuhusiana na afya yako. Watafiti hawa wamekiri kutokufahamu
kuhusiana na hali ya mmeng’enyo wa chakula kwa wanaume hasa wanapokuwa
na msongo wa mawazo. Wanahisi kwamba matokeo ya utafiti huu yanaweza
yakawa tofauti kidogo kwa wanaume kwasababu wanaume wanamisuli. Hii
inamaanisha kwamba mfumo wao wa mmeng’enyo wa chakula ni watofauti
ukilinganisha na wanawake.
Tafiti
nyingine zimeonysha kwamba msongo wa mawazo hutufanya tule sana
hususani vyakula vya mafuta na sukari nyingi. Wataalam wanasema hii ni
mbinu ya asili ya mwili kukabiliana na hofu au vitisho. Mtaalam wa lishe
katika chuo kikuu cha Ohio Martha Belury anashauri kwamba ni vema
tukaweka vyakula vyenye lishe na vilivyo bora kwenye makabati na
majokofu yetu majumbani ili pale miili yetu inapotamani kuingiza chakula
fulani, basi kinachopatikana kwa wakati ule kiwe chenye afya kwa mwili
zaidi ya kuongeza kula vyakula vyenye athari kiafya.
Na: Chris Mauki. PhD
Social, Relationship and Counseling Psychologist
University of Dar es Salaam
+255 713 407182
No comments:
Post a Comment