Ili mapenzi yaweze kuwa bora kwa kila aliye katika
mahusiano, huwa ni vyema kila mmoja kuiona thamani ya mwenzake. Ukipenda
kujiangalia mwenyewe si ajabu mwenzako kupata hisia za kuwa humthamini
wala humjali.
Muunganiko wenu katika mapenzi maana yake tayari mmekuwa kitu kimoja. Katika mimi unaweka sisi.
Ila pia ni vyema ikakumbukwa ladha na maana halisi ya
mapenzi ipo kwa anayekupenda na kukuthamini. Unapokuwa na uhakika kama
anakupenda na kukuthamini hapo ndipo nafsi yako itatulia na kuwa na
amani. Ndani ya mapenzi na mtu wa aina hii ni amani na utulivu kwa
kwenda mbele. Hakuna majuto wala majonzi ya kila siku.
Unapoamua kuwa katika mahusiano na mtu ambaye hakupendi,
bali unakuwa naye kwa kuwa tu unampenda jua umejiingiza katika utumwa.
Mapenzi ni suala la kihisia zaidi. Mwenzako anapokosa hisia na wewe
maana yake hata uwepo wako hauthamini inavyopaswa. Na hapo ndiyo tunaona
yale mahusiano ya kingono yanapozaliwa na si ya kimapenzi kwa maana
halisi.
Yaani mwenzako anapokuwa na mihemko ya kingono ndipo
anapokutafuta na si vinginevyo. Niliwahi kuongea na msichana mmoja
aliyewahi kuniambia anampenda kijana mmoja ambaye anauhakika kabisa yeye
hampendi. Alinambia uhakika huo kaupata kutokana na kijana huyo
kumtakia kuna msichana yupo anampenda na kumjali ila si yeye.
Kuonesha zaidi kumpenda msichana yule mwingine, jamaa
aliwahi kumwambia kama ikitokea hata huyu msichana akagombana na yule
mpenzi mwingine wa yule jamaa, kijana yule alikuwa radhi kumdhuru huyu
msichana.
Hata kwa matazamo wa haraka hapo unaweza kugundua ni kwa
namna gani huyu msichana alikuwa haitajiki. Ila cha kushangaza msichana
huyu(aliyeongea na mimi) alimwambia mvulana husika yuko radhi kuwa naye
hivyo hivyo.
Aliamua kuwa hivyo akiamini ipo siku jamaa atamuelewa. Kweli walikuwa pamoja. Ila unajua kinachomkuta sasa?
Kila jamaa anapogombana na yule msichana mwingine anamtumia
huyu kingono na mambo mengine yasiyo ya kimapenzi, na bila kutafakari
mara mbili huyu msichana anafanya kwa kile anachoamini hali hiyo
itamfanya huyu jamaa amfikirie zaidi. Kuna kitu cha kuangalia hapa.
Suala la mapenzi si suala la kuoneana huruma wala aibu.
Mapenzi ni hisia. Unapojitoa kwa mwenzako kwa kila jambo na unamuona
haelekei ujue hana hisia na wewe. Kwanini unakubali kuteseka na kuumia
kila siku kwa kumuangalia yeye tu?
Ndiyo, unampenda sana, unamjali sana na unamuhitaji sana,
ila kama yeye hakutaki wa kazi gani? Ni muda wa kujiangalia na wewe
sasa.
Ona thamani yako kama binaadamu, jionee huruma jinsi unavyoteseka kila siku kwa mtu asiyeona thamani yako.
Wewe ni binaadamu mwenye hadhi na thamani, bila kujali
muonekano wala rangi yako. Unahitaji mwenye kukuthamini na kukujali na
si anayekufanya kama mdoli wake ngono au kadi yake ya pesa. Kataa utumwa
wa mapenzi kwa kuiona thamani yako.
Ni vyema ukalia kwa kumkosa kuliko kuonekana unaye wakati
moyoni siyo wako. Hakuna sifa ya kuwa na mtu mwenye fedha au muonekano
mzuri ikiwa hakujali wala haupo moyoni mwake. Mapenzi ni amani na raha.
Mapenzi hufanya watu wafurahi na kusahau shida zao. Ila
jiulize kwanini kwako hayako hivi? Unaenda kwa mwenzako badala afurahie
uwepo wako, yeye anaona unajipendekeza. Unampigia simu na kumpa maneno
mazuri ya faraja, yeye anaona unamsumbua. Sasa wa kazi gani? Siku njema
wapendwa.
No comments:
Post a Comment