Mapenzi yana wigo mpana mno ambao mtu
anapaswa kuuangalia kwa jicho pana na akili pembuzi kabla ya kuingia,
namaanisha kwamba ni lazima kuchunguza kina cha maji kabla ya kuzamia. Sasa basi, zifuatazo ni faida tano utakazozipata ukiwa umenuniana na mpenzi wako.
HUSAIDIA KUPUNGUZA MIGOGORO
Ni ukweli usiopingika kuwa, katika hali
ya kawaida, ukiwa mbali na mtu fulani katika jamii unayoishi ni vigumu
sana kujikuta umekwaruzana naye. Hii ni kwasababu utakuwa hauingiliani
naye katika mizunguko yako, vivyo hivyo kwa wapenzi walionuniana.
Hali hii hupunguza kabisa migogoro ya
hapa na pale, kwani hiki ni kipindi ambacho mtakuwa mbalimbali jambo
ambalo huepusha maudhi ya kibinadamu.
Mfano, yawezakana katika kipindi
mlichonuniana na mpenzi wako, uliingia ujumbe wa mapenzi kwenye simu
yake kutoka kwa mtu aliyekosea namba. Kwa kuwa hauko naye karibu jambo
hili halitakuumiza maana hutaelewa nini kimeendelea tofauti na kama
ungelikuwa naye karibu.
Kwa hiyo kuna baadhi ya maumivu na
maudhi ambayo utaepukana nayo kwa kipindi cha kununiana kwenu. Ni kweli
kabisa kwamba hupunguza migogoro na mitafaruku ya hapa na pale, umeelewa
mpenzi msomaji wangu? Haya twende kwenye faida ya pili.
KUBAINI TABIA X ZA MWENZAKO
Hiki ni kipindi ambacho sasa
kitakusaidia wewe kubaini tabia na mienendo mibaya ya mwenzi wako. Hii
ni kwa kuwa utakuwa mbali naye hivyo naye hujiona kuwa yuko huru kufanya
jambo lolote analoona kuwa linafaa bila kujali uwepo wako kwani kila
mtu hana ‘time’ na mwenzake.
Kama kuna asili ya maisha yake ambayo
aliiacha baada ya kuingia katika uhusiano na wewe, ambayo ni mbaya zaidi
sasa hapa ataanza kuirudia kwa kujiona kuwa hana mtu wa kumzuia na
kumbana.
Kama ni mlevi kupindukia, mchafu, muongo
na tabia nyingine mbaya za kufanana na hizi basi ataanza kuzionesha
katika kipindi ambacho mmenuniana.
KUPATA MUDA WA KUTAFAKARI ZAIDI
Hapa naomba nieleweke vizuri kabisa
kwamba, ninapoongelea suala la kutafakari zaidi katika kipindi ambacho
wewe hauna maelewano mazuri na mwenzi wako, namaanisha kuwa utapata muda
mzuri zaidi wa kutafakari penzi lenu kwa ujumla.
Ni kipindi kitachokuongoza wewe kuwa na
uelewa wa ni aina gani ya mpenzi uliyenaye. Kivipi? Ni kwamba, katika
muda huu mara nyingi utataka kupata suluhu ya kununiana kwenu, lakini
pia katika kutafuta suluhu hiyo utapata fursa ya kutafakari kwa kina juu
ya penzi lenu huku ukimpima mwezi wako kwa mtazamo chanya.
KUFAHAMU AINA YA MARAFIKI ZAKE
Si kila rafiki wa mwenza wako ana nia
nzuri na uhusiano wenu au anafurahia penzi lenu. Mathalani, labda wewe
ni msichana na pengine miongoni mwa rafiki zake kuna mmoja au wawili
ambao hutamani sana kupata penzi lako.
Sasa katika kipindi ambacho utakuwa
umenuniana na mpenzi wako basi itakuwa ni nafasi nzuri kwao kuitumia
kunyunyizia sumu ya kumponda huku wakikutamkia maneno ya kukushawishi,
hivyo utakuwa umeelewa ni aina gani ya marafiki alionao mwenzi wako.
Hii si kwa msichana tu, hata kwa
wanamume kwani huenda kati ya rafiki wa ‘girlfriend’ wako, kuna
wanaokutamani, sasa wakiona huna uhusiano mzuri na mpenzi wako,
watatumia nafasi hii kukuambia maneno ya uongo juu yake na kukuonesha
kila dalili za kukutaka.
Hivyo utakuwa umefahamu ni aina gani ya rafiki ambao mpenzi wako anao. Tambua kwamba, marafiki wengi wana tabia zinazofanana.
KUBAINI AINA YA PENZI ALILONALO KWAKO
Katika kipindi hiki, utaweza kuelewa ni
aina gani ya penzi alilonalo huyo mtu wako juu yako. Kwa mpenzi aliye na
hisia za dhati kabisa kwako, katika kipindi hiki atakuwa ni mtu wa
kutafuta njia ya kupata suluhu ya tatizo lenu.
Pamoja na kwamba wewe utakuwa umenuna,
bado yeye ataonesha kukujali kama kawaida, atakupigia simu za hapa na
pale yaani ilimradi tu asikie angalau sauti yako, lengo lake likiwa ni
kutaka kurejesha ukaribu ambao sasa anaona kama akiupoteza itakuwa ni
maumivu kwake.
Kwa mantiki hiyo basi, utagundua ni kwa
jinsi gani anathamini penzi lenu na ni aina gani ya penzi alilonalo
kwako. Yote haya utabahatika kuyajua kupitia kipindi cha kununiana
kwenu.
Hata hivyo, niwatahadharishe kwamba,
kuandika haya isiwe ni tiketi ya wewe sasa kuanza kununiana na mpenzi
wako eti kwa kigezo kwamba utapata nafasi ya kumfahamu, la hasha!
Siku zote katika uhusiano wako epuka maudhi na migogoro isiyokuwa ya lazima.
No comments:
Post a Comment