WANAWAKE wakiwapenda
wanaume hubaki na mateso mioyoni mwao. Hii ni kwa sababu ni vigumu
kumtokea mwanaume moja kwa moja kumwaga sera kuwa unataka ‘akung’oe’.
Ni kweli kwamba, hata kama
mwanaume akimkubali mwanamke awe mpenzi wake baada ya kutokewa, imani
yake huwa hafifu kuhusu penzi la kweli la mwanamke huyo. Anaweza
kumtumia kwa siku kadhaa kisha akamwacha. Huo ndiyo ukweli.
Wanawake waliowahi
kuwatokea wanaume wanaweza kuwa na ushahidi mzuri zaidi juu ya hilo.
Pamoja na hayo yote, bado mwanamke anabaki kuwa binadamu, mwenye hisia
za upendo na kutamani baadhi ya vitu.
Anaweza kumpenda mwanaume
na ni haki yake ya msingi kabisa. Kuwa katika uhusiano na mtu
unayempenda kwa dhati ni jambo zuri. Moyo huridhia na kuwa huru katika
uhusiano huo.
Hapa katika Let’s Talk
About Love tunakupa dondoo zitakazokusaidia kumsogeza mwanaume ambaye
ameuteka moyo wako na hatimaye kuwa wako moja kwa moja. Katika vipengele
vilivyotangulia nilieleza kuwa, kwanza mwanamke ni vyema ajitunze na
aweke mwonekano wake wenye kuvutia muda wote halafu pia nikaeleza kuhusu
kumvutia mwanaume kwa mambo mbalimbali hasa mavazi na mambo
anayopendelea. Sasa tunaweza kuendelea.
ASIWE KWENYE UHUSIANO
Jambo lingine la kuzingatia
kwa mwanaume huyo wakati wa harakati za kumweka mikononi mwako ni
kuhakikisha hayupo kwenye uhusiano na mtu mwingine. Kuna baadhi ya
wanawake wapo tayari kuwa na mwanaume hata kama yupo na mpenzi mwingine;
hilo ni kosa na naweza kusema ni umasikini wa kufikiri.
Kama kweli umempenda, itakuwa na maana kama utaweka makazi ya moyo wako kwake milele na siyo kwa muda mfupi tu.
JISOGEZE ZAIDI
Tayari umeshakuwa na
uhakika kuwa hana mtu, sasa unatakiwa kujisogeza karibu yake. Jizoeshe
kumsalimia mara kwa mara na kumsifia kuwa amependeza.
Kamwe usioneshe dalili
kwamba wewe ni ‘maharage ya Mbeya’, ishia kwenye kujisogeza karibu yake
kwa kumsifia na kufanya mambo mengine yanayofanana na hayo na siyo zaidi
ya hapo.
JENGA URAFIKI
Ukaribu wenu sasa unaweza
kuwafanya marafiki wa karibu. Kama uko naye ofisi moja au mnaishi
mtaa/nyumba moja ni rahisi zaidi. Kuwa rafiki yake wa kweli mwenye
kujadiliana naye mambo ya msingi.
Katika urafiki wenu, kamwe
usiwe mzungumzaji sana (hasa wa mambo yasiyofaa), aidha usipende kukaa
naye katika mazingira yenye vificho ambayo yataweza kusababisha kuingia
kwenye mtego mbaya.
ZUNGUMZIA ZAIDI MAISHA
Kuzungumzia zaidi maisha na
kumshauri juu ya mambo muhimu ya maisha, kutamfanya akuone wewe ni
mwanamke makini mwenye malengo mazuri katika maisha yako. Wanaume
wanapenda sana wanawake ambao vichwa vyao vinafanya kazi sawasawa.
Hii inaweza kuwa sababu itakayomfanya atamani kuwa karibu yako zaidi, jambo ambalo ndiyo shabaha ya moyo wako.
HAKUNA YEYE BILA WEWE
Kwa sababu tayari ni
marafiki na mnashirikiana baadhi ya mambo, tengeneza mazingira ya kuwa
naye karibu zaidi. Mshirikishe kwenye mambo yako, mfanye ajione si
mkamilifu bila kuwa na wewe karibu.
Hili litawezekana kwa
kuishika siku yake, kumtakia siku njema na kumjulia hali yake kazini na
maendeleo yake kwa ujumla. Kwa kuwa ni marafiki, kwa ndani lazima hisia
za mapenzi zitaibuka juu yako na utamuweka kwenye nafasi ya kufikiri
kuanzisha uhusiano na wewe.
NI WAKO TU!
Ukipitia hatua zote, bila
shaka mwanaume huyo ni wako tu. Ikiwa pamoja na vyote hivyo bado
haonyeshi dalili au hajafunguka kuwa unamhitaji, basi mwache, siyo
riziki yako. Kwa nini ung’ang’anie usipopendwa?
No comments:
Post a Comment