HAPA tunazungumza kuhusu
mapenzi kama kawaida yetu. Leo nimekuja na mada ambayo naamini itawagusa
wengi. Marafiki zangu, kusaidia katika mapenzi ni jambo zuri tena lenye
mantiki sana.
Suala la kusaidiana si la upande mmoja. Linaweza kuwa kwa wote, kwa
mwanaume au mwanamke. Ni kati ya nguzo muhimu katika mapenzi, lakini kwa
bahati mbaya kuna wale ambao
wamekuwa na tabia ya kupenda sana fedha!
Unajua wenzi wanajuana kulingana na wanavyoishi, hivyo ni rahisi sana
kumgundua mwenzako kama anapenda sana fedha au ni kweli ana tatizo
linalohitaji msaada wako. Hii ni kasoro, lakini haimaanishi kwamba ndiyo
sababu ya kuachana.
Katika mada hii ipo dawa ya namna ya kudumu katika mapenzi motomoto na
mwenzi wa aina hii. Imekuwa ni kawaida kumsikia msichana akitamba mbele
ya wasichana wenzake kwa kusema: “Mimi nina kibuzi changu bwana kila
ninachotaka kinanipa, kinajua kisiponipa nakitosa tu, yaani nakichuna
kama sina akili nzuri.”
Umewahi kukutana na maneno ya aina hii? Bila shaka jibu ni ndiyo. Si
hivyo tu, wapo wanaume pia ambao ni kero kwa wapenzi wao, yaani
wamegeuka wanaume kama mabinti kwa tabia zao za kutegemea kupewa kila
kitu na wapenzi wao hata kama wanao uwezo wa kuvipata vitu hivyo kama
watajishughulisha.
Ninachotaka kusema leo ni kwamba, mapenzi ya kweli hayana uhusiano
wowote na fedha, ukiona mpenzi wako anaweka fedha mbele na ukishindwa
kumpatilizia anachokitaka anakasirika, jua penzi lake lina walakini,
hakupendi bali anataka kukutumia kisha kukuacha.
Katika mapenzi hatukatai suala la kusaidiana, mpenzi wako akiwa na shida
fulani akaomba umsaidie, kama unao uwezo msaidie na kama huna mueleze
ukweli kisha muangalie namna nyingine ya kumsaidia.
Itakuwa siyo busara kama utakuwa na tatizo lakini ukaona kwamba
ukimweleza mpenzi wako ataona unamchuna. Wapenzi wanaopendana kwa dhati
hawachunani bali wanasaidiana na hili ni kwa pande zote mbili.
Kinachokera ni kutoishiwa na matatizo na wakati mwingine unakuta kuchuna
kwingine ni kwa mambo ya starehe. Yaani sasa hivi umemuomba mpenzi wako
vocha, hajakaa vizuri umemtaka akija akuletee chipsi mayai, baadaye
unataka akutoe ‘out’, bila kujali kwamba wakati huo mpenzi wako ana
fedha au laah.
Katika mazingira hayo unadhani mpenzi wako atashindwa kukuchoka?
Akikuacha kwa sababu hiyo utamlaumu? Kimsingi ukiwa na mpenzi mwenye
tabia ya kutaka kukuomba fedha kila wakati tena katika matumizi mengine
ambayo siyo ya msingi, mbinu zifuatazo ni muhimu kuzifuata. Twende
tukaone.
MWELEZE UKWELI
Kama huna fedha wakati mpenzi wako anakuomba, mueleze wazi kuwa huna na
kamwe usijaribu kutoa ahadi ambazo huenda ukashindwa kuzitimiza. Usiwe
mtu wa kutoa ahadi za uongo, mara nitakununulia hiki na kile.
Mwanaume hatakiwi afahamike siku ana fedha au hana. Maana kuna wenzangu
ambao siku za mishahara wanabadilisha hadi kutembea! Mwanamke akijua
hilo naye ataongeza ‘mizinga’ ili afaidi.
JENGENI KUSAIDIANA
Jambo la muhimu ambalo wanaume wengi wanalisahau ni kutokuwafundisha
wapenzi wao wajibu wa kutoa. Utakuta kila kitu ananunua yeye, hata nauli
ya basi analipa, wakati mpenzi wake ana kazi yake.
Ifike wakati kwa makusudi, mwanaume ampe majukumu ya kufanya mpenzi
wake, hiyo itamsaidia mwanamke kujua namna fedha zinavyokuwa hazitoshi
na ataweza kubana matumizi.
ACHA UFUJALI
Kuna wanaume wengine tangu wanatongoza wanakuwa ni wafujaji wakubwa wa
fedha kwa kutoa ofa na zawadi kibao. Hii inaweza kumjengea imani mpenzi
wako kuwa unazo!
Unachotakiwa ni kudhibiti mapema matumizi yako hata kama fedha
itakuwepo. Ifahamike kuwa kutoa hakushibishi uhitaji, kadiri unavyotoa
ndivyo unavyoongeza mahitaji. Weka maisha yako katikati usijidai tajiri
kumbe ni kapuku tu.
BAKI NA HILI
Katika kumalizia niseme tu kwamba, mapenzi si kukomoana, bali
kusaidiana. Jenga tabia ya kumsaidia mwenzako ili siku na wewe ukiwa na
tatizo akusaidie.
Kitu unachotakiwa kukiepuka ni kuwa tegemezi hadi unakuwa kero. Kumbuka
kumpiga mizinga mpenzi wako kila mara kunapunguza mapenzi hivyo epukana
na tabia hiyo.
No comments:
Post a Comment