Polisi wilayani Babati mkoani Manyara
inamshikilia askari wa jeshi hilo Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU),
Cosmas James akituhumiwa kumuua mzazi mwenzake, Regina Daniel (23) kwa
kumpiga risasi nne.
Chanzo cha mauaji hayo inadaiwa ni mzozo ulitokea Regina alipomfuata James lindoni kudai fedha za matumizi ya mtoto.
Akithibitisha tukio hilo, Kaimu Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Manyara, Longinus Tibishubwamu amesema lilitokea mjini
Babati Ijumaa Oktoba 27,2017 saa 12:30 jioni.
Amesema askari huyo alikuwa lindoni katika Benki ya NMB tawi la Babati, mtaa wa Usalama, Kata ya Bagara.
Kaimu Kamanda Tibishubwamu amesema Regina ni mkazi wa Mtaa wa Ngarenaro mjini Babati.
Amesema uchunguzi wa awali unaonyesha
kabla ya kifo cha mwanamke huyo kulitokea mzozo kati ya wawili hao
kuhusu fedha za matumizi ya mtoto.
"Wakati wakiendelea na mzozo, ndipo
askari huyo kwa kutumia silaha aliyokuwa nayo alimpiga Regina risasi nne
kwenye paji la uso, kifuani na shingoni," amesema.
Amesema askari huyo alitumia silaha aliyokuwa nayo lindoni aina ya SMG mali ya Jeshi la Polisi.
Baada ya tukio, amesema askari huyo
aliitelekeza silaha lindoni na kwenda kujisalimisha polisi. Amesema
askari waliokwenda eneo la tukio waliokota maganda matatu ya risasi na
waliichukua silaha hiyo.
Kaimu Kamanda Tibishubwamu amesema
mtuhumiwa yupo mahabusu kwa mahojiano kabla ya hatua nyingine
kuchukuliwa na mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Mji wa
Babati ya Mrara.
Askari wa FFU mjini Babati,
aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina amesema anashangazwa na tukio
hilo kutokana na upole alionao James.
Amesema James ni askari mwenye nidhamu, hivyo hafahamu jambo gani limempata hadi akamuua mzazi mwenzake.
No comments:
Post a Comment