Artikel Terbaru

Responsive Ads Here

Sunday, April 22, 2018

MAPENZI: UHUSIANO ULIOPO UNA MANUFAA MAISHANI MWAKO ? AU UNAPOTEZA MUDA TU, CHEKI HAPA


Ili uhusiano wako uwe na maana lazima uangalie mara mbili na ujiridhishe kuwa una manufaa na wewe. Kuna mengi tumezungumza katika matoleo yaliyopita lakini leo tunafikia ukingoni.

Marafiki, uhusiano usio na amani, kuharibu fedha kwa anasa hauna maana katika maisha yako. Sanasana unazidi kujiongezea matatizo tu. Kwa mfano, si utaratibu mzuri kutumia fedha nyingi kwa kulipia nyumba za wageni, taksi na mahitaji mengine kwa ajili ya anasa.


Yupo msomaji mmoja alinitumia meseji wiki iliyopita alinishangaza sana, kiukweli sikumjibu! Lakini nitamjibu kupitia gazeti damu moja na hili, Risasi Jumamosi, toleo la wiki hii. Yeye alisema, eti ana mke wake, lakini ana nyumba ndogo, amempangia nyumba na kumwekea kila kitu ndani. Amempa mtaji wa biashara ambayo inamsadia kumwendesha bila kumtegemea.

Swali alilouliza ni kwamba, je, kwa kufanya hivyo, atakuwa amefanya ufujaji wa fedha? Nadhani hata wewe msomaji wangu unaweza kujibu swali hili. Hebu tuendelee na mada yetu. UNAMPA FURAHA MWENZI WAKO? Katika kuangalia ulichokifanya kwa ajili ya mapenzi au mapenzi yalichokufanyia ni lazima ufikirie juu ya jambo hili; unamfurahisha mpenzi wako?

Maana kutomfurahisha ni tatizo kubwa katika ustawi wa penzi lenu. Haiwezekani mkawa mnaishi na mwenzi wako lakini kila siku ugomvi, hakuna maelewano, unamdharau, unamnyanyasa, matusi yasiyokauka nk. Lazima uishe na mwenzako kwa upendo wa hali ya juu, onesha jinsi unavyofurahia kuwa na mwenzi wako na unatakiwa kuhakikisha kwamba mwenzi wako anafurahia kuishi na wewe siyo muishi ili mradi siku zinakwenda.

Kumfanya mpenzi wako asononeke au kumnyima raha kwa namna yoyote ile, kunakufanya ukose mafanikio kwa sababu ya machozi yake. Kama ulikubali kufunga naye ndoa, kwa nini hutaki kumpa haki yake ya unyumba? Acha kumnyanyasa mwenzako. MOYO WAKO UNASEMAJE? Suala la kuusikiliza moyo wako si la majadiliano, lazima uupe moyo wako kipaumbele kwa kila kitu kinachohusu mapenzi.

Usikubali kuishi katika mapenzi ya kitumwa, usikilize moyo wako unavyosema. Huna sababu ya kuishi na mwenzi ambaye huna mapenzi naye, kitu cha msingi ambacho kinapaswa kuzingatiwa mpenzi ni kwamba kabla hujafunga ndoa ni vyema ukauacha moyo wako ukaamua kwa dhati. Ni kweli upo tayari kuishi naye? Unampenda kwa mapenzi ya dhati? Lazima ujiulize na uwe na majibu yakinifu! Kuwa na ndoa mahali ambapo huna mapenzi napo ni tatizo.

Upe moyo wako haki ya kuamua ni wapi unapoona ni sahihi. Kukubali kuingia katika ndoa na mwenzi ambaye moyo wako unamtilia mashaka maana yake ni kwamba utakuwa umeingia kwenye gereza la moja kwa moja la mapenzi. ANZA KUFIKIRIA UPYA! Kuishi katika utumwa au kutokuwa imara katika uhusiano ni safari ndefu, inayochosha na yenye maumivu makali.

Kudumu katika uhusiano wenye migogoro ya kila aina kwa muda mrefu, kwa hakika ni kipindi kigumu sana.
Anza maisha mapya, fikra zako zibadilike, amini kwamba hakuna chenye mwanzo kikakosa kuwa na mwisho. Amini kwamba Mungu alivyomuumba Adam, alimuumba Hawa pia kwa ajili ya kumsaidia Adamu. Hicho ni kielelezo tosha kwamba hata wewe unayesoma mada hii, yupo aliye maalum kwa ajili yako. Huna sababu ya kuendelea kuburuzwa katika uhusiano batili.

Kila kitu kinawezekana, amua kwa dhati ya moyo wako na ninakuhakikishia kwamba utaanza maisha mapya ya kimapenzi. Inawezekana kama ukiamua kukubali kwamba kubadili historia ya maisha yako ya kimapenzi kupo mikononi mwako.

No comments:

Post a Comment