WAKATI mwingine unaweza kujikuta njiapanda muda wa kutaka kuchukua
maamuzi. Kila unachotaka kufanya unahisi kama unahitajika muda zaidi au
uvumilivu zaidi. Katika maisha vitu vya namna hiyo huwa vinatokea!
Umeshawahi kuwa na mtu na kujikuta kama humuelewi hivi, halafu
ukashindwa kujua ni uamuzi wa aina gani unafaa kuuchukua? Mtu ambaye
unajitahidi kwa kila hali kumuonesha namna unavyompenda ila wapi!
Anakuchukulia kawaida tu.
Wala haoneshi kuthamini wala kuheshimu upendo na mapenzi unayomuonesha.
Ulishawahi kuwa naye? Au ndiyo huyo uliye naye? Hapa suala ni moja tu.
Mueleze namna unavyojisikia kwa tabia yake.
Katika kumweleza huku unapaswa kutafuta siku ambayo ni tulivu, kwa maana
kila mmoja asiwe na kazi kwa muda huo ili maongezi yenu yapate heshima
inayostahili.
Tumia nafasi hiyo kuwasilisha yote ya moyoni unayojihisi juu ya tabia
yake. Mwambie katika hali isiyokuwa ya kulaumu wala jazba. Eleza namna
yote unavyoteswa na tabia yake isiyoonesha kukupenda wala kuuthamini
upendo wako.
Baada ya kuhakikisha tayari anajua namna unavyojisikia, sikiliza
atakachokisema. Kuwa makini kupima kauli zake na jinsi sura yake
inavyomaanisha. Wengine wanaweza kukupa majibu mazuri huku sura yake
ikiwa inaonesha dharau na kejeli. Haina maana!
Pima uzito wa maneno uliyomwambia na majibu atakayokupa. Ukiona vina
uwiano na ni majibu mazuri, mpe nafasi nyingine hata kama hiyo ni mara
ya pili anakukosea. Kuwa mvumilivu – bila uvumilivu hakuna mapenzi ya
kweli. Uvumilivu ni mama wa mafanikio.
Baada ya kuwa tayari umemweleza jaribu kusahau makosa yake na ufungue
ukurasa mwingine katika maisha yenu. Hapo haitakiwi tena kukumbushia
makosa yaliyopita.
Hiyo itamnyima uhuru wa kufurahi kikamilifu na wewe pia kuna uwezekano
mkubwa wa kuchochea migogoro isiyo ya lazima katika mapenzi yenu.
Maana unaweza kumkumbusha hili na yeye akakukumbusha lile. Na kila mmoja
hapo akataka kumuona mwenzake ndiyo mkosaji zaidi. Mapenzi hayawezi
kuwa mazuri kwa staili hiyo.
Baada ya kuwa mmemaliza tofauti zenu anza kuangalia mabadiliko chanya
katika matendo yake. Ni kweli kabadilika? Au kilichobadilika ni staili
tu ya kukunyima furaha ila balaa ni lile lile?
Kama alikuwa na skendo za vimada sasa huzisikii ila kila siku safari
zisizokuwa na sababu na ukijaribu kuuliza anakwambia “kuna mambo naweka
sawa”. Mambo gani? Hakwambii! Akirudi ‘break’ ya kwanza bafuni akaoge
kwanza ndiyo arudi muongee.
Ikiwa unamfanyia mpenzi wako kila lililojema katika mahusiano na bado
haoneshi kubadilika zaidi ya kukusema “we msemaji sana” au anatoa ahadi
tu zisizotekelezeka, kuna jambo la kufanya.
Kaa naye kisha mueleze kwa mara ya mwisho juu ya tabia yake na umueleze
hatua unayokwenda kuchukua kama asipobadilika. Mapenzi ni raha na amani.
Kama mtu hakupi hayo basi hakufai.
Kwa nini kila siku mahusiano yako yawe ya masimango na majuto
yasiyokwisha? Kila siku machozi yatoke kwako tu. Kwani wengine hawana
wapenzi? Mbona hawalalami wala kuumizwa?
Unapaswa kujua kitu – anayekupenda atakujali na kukuthamini. Hata siku
moja hatapenda kuona unahangaika na kulia kwa sababu yake. Ukiona mtu
anaona unaumia na kuteseka kwa ajili yake halafu hana habari na wewe jua
kuna namna. Siyo bure.
Kama hakuna ulichomkosea wala kumkera basi jua hana mapenzi na wewe.
Iweje akupende halafu asijali chozi lako? Kivipi aseme anakuthamini
wakati hajali maumivu yako? Kuwa makini. Kuwa makini zaidi!
No comments:
Post a Comment