USALITI ni jambo baya katika uhusiano. Usaliti si ujanja japo wengi
wanaowaza kusaliti huwa wanajiona wajanja. Wanajiona wamewini pale
ambapo wanasaliti na wenzi wao kutogundua kama wanasalitiwa.
Siku zote anayesaliti huwa anajiona mjanja kwamba, yeye anasaliti wakati
mwenzake hasaliti. Kwa asilimia kubwa, wanaume hujiona kama usaliti ni
halali yao. Wanataka wao wasaliti lakini wapenzi wao wasithubutu
kusaliti.
Kwa nini hawataki wenzi wao wasaliti? Eti wanaumia. Hakuna kitu
kinachomchukiza mwanaume kama kusalitiwa. Kusaliti asaliti yeye,
akisaliti mwenzake ni kosa la jinai. Anaona amedhalilishwa.
Anajisikia fedheha kwamba mpenzi wake amemuonaje? Amemchukuliaje?
Hajakamilika idara gani? Anawaza sana. Anajiuliza jamii yote inayojua
kitendo hicho inamtazamaje? Kwamba ni boya kiasi gani hadi anaibiwa
kirahisi. Hana nguvu za kiume? Hana uwezo kifedha?
Hapo ndipo unapokuta mwanaume anaamua kuchukua uamuzi mgumu ikiwemo hata kuhatarisha maisha ya mwenzi wake.
Marafiki zangu, watu wanauana kwa sababu ya usaliti. Kwa mwenye penzi la dhati, kamwe hawezi kuvumilia usaliti.
Nikirudi katika mada yangu kama inavyojieleza hapo juu, kuna viashiria
mbalimbali ambavyo ukiviona kwa mwenzi wako basi ujue unasalitiwa.
Vifuatavyo ndivyo viashiria vyenyewe:
KUTOPENDA KUCHIMBWA
Mara nyingi anayesaliti huwa hapendi kuchimbwa mambo kwa undani. Anahofu
anaweza kuchanganya madawa. Hupenda mazungumzo mafupi na moja kwa moja.
Hapendi kuulizwa maswali mengi, ukimuuliza anayakwepa haraka na kutaka
kukupeleka kwenye mazungumzo anayoyataka yeye.
Ukimuuliza kuhusu mipango yenu, ukimuuliza kuhusu mustakabali wa penzi
lenu baadaye hukuondoa kwenye mstari na kukufanya usiwe na hamu ya
kumuuliza mara mbilimbili.
HAPENDI UJUE RATIBA YAKE
Mara nyingi mtu ambaye ana lake jambo huwa hapendi ujue ratiba yake.
Anataka usimzoee. Iwe anafanya maamuzi yake kulingana na yeye mwenyewe
anavyojua. Ikitokea unaijua ratiba yake, atakuwa ni mtu wa kutoa udhuru
kila wakati.
Leo atakwambia kuna mgonjwa anakwenda kumuona. Kesho atakwambia kuna
vikao na wafanyakazi wenzake. Siku nyingine atakuambia gari imepata
pacha, analazimika kusubiri mafundi hadi wafike ndio aweze kuanza safari
ya kurudi nyumbani.
Ukiona mtu ana visingizio vingi, jua kwamba njia zake si salama. Hataki
ujue nini anafanya kwa wakati fulani. Kwa ambaye hana makando kando,
anaeleza ratiba yake kwa uwazi. Hata kama inatokea dharura, anaieleza na
inaeleweka.
SIMU YAKE KITUO CHA POLISI
Anayesaliti mara nyingi hapendi kuacha simu yake kiholela. Simu inakaa
mfukoni kwake hata kama hakuna ulazima wa kufanya hivyo. Mpo nyumbani,
mpo kwenye mazungumzo ya kifamilia yeye simu yake ipo mfukoni.
Imetolewa mlio. Hataki uione maana inawezekana akatumiwa ujumbe, picha
na mambo mengine ya kimapenzi. Anayejiamini na yupo kwenye uhusiano
imara, hana sababu ya kufichaficha simu yake. Anaiweka hadharani.
Mwingine atakusetia simu yake. Ukimpigia kila wakati inaonekana iko
bize. Kila ukipiga inaonekana inatumika, kumbe yeye ndio anatumika
wakati huo. Anakusaliti.
ANACHATI SANA
Wanaosaliti wengi wao hupenda kutumia meseji katika mawasiliano yao.
Yani amewazoesha michepuko wake wote kusaliti. Hapendi kupokea sana
simu. Zaidi anapenda kuchati hivyo ni rahisi kuwasiliana na mchepuko
wake.
HAKUTAMBULISHI NDUGU, MARAFIKI
Msaliti anataka usiwajue watu wake wa karibu. Anahofia wanaweza
kuvujisha taarifa bila hata kujua wanauza silaha. Kuepuka hilo, anataka
umjue yeye na watu wake wachache.
Zaidi sana atakutambulisha kwa rafiki yake ambaye ni mchepukaji mwenzake. Wanajua namna ya kucheza michezo ya usaliti.
Usalitiwa kunauma. Kuepuka maafa ni vyema wapendanao wakawa waaminifu.
Kila mmoja aheshimu hisia za mwenzake. Amtunzie heshima, awe na hofu
kwamba akifanya hivyo anamuumiza mwenzake na kama ambavyo yeye ataumia
akifanyiwa.
Tukutane wiki ijayo. Waweza kunifuata katika mitandao yangu ya kijamii;
Instagram na Facebook natumia jina la Erick Evarist, Twitter ni
ENangale.
Monday, June 11, 2018
Hizi Hapa Ndio Mbinu za Mabingwa wa Kusaliti Katika Mapenzi
About Anonymous
Soratemplates is a blogger resources site is a provider of high quality blogger template with premium looking layout and robust design. The main mission of templatesyard is to provide the best quality blogger templates.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment