KARIBUNI wasomaji wangu katika safu hii ya mahusiano ambayo huwajia kila
siku ikilenga kufahamishana hili au lile kuhusiana na mambo ya mapenzi
au ukipenda unaweza kuita mahaba.
Awali ya yote, niwashukuru wale wote ambao wamekuwa wakitumia muda na
fedha zao kutuma ujumbe wenye lengo la kupongeza mada zinazotolewa
katika safu hii, huku wengine wakichangia pale walipoona inafaa kufanya
hivyo. Nasema asanteni sana.
Baada ya salamu hizo, tugeukie mada ya leo. Katika mada zilizopita
kuhusiana na suala zima la kupenda, wasomaji wangu wamekuwa wakichangia
kwa mitazamo tofauti, huku wengi wakionekana kutofautiana kwa misingi ya
kijinsia.
Mathalani, katika mada zilizohusisha suala zima la usaliti katika
mapenzi na dhana nzima ya kupenda, kumetokea mabishano makali kuwa kati
ya wanawake na wanaume, wanawake ndio ambao wamekuwa wakiwapenda wenzao
wao kwa dhati kuliko ilivyo kwa wanaume.
Lakini pia, wapo wanaume waliokuwa wakisisitiza kuwa wanawake ndio
vigeugeu katika suala zima la mapenzi kwani wengi wao si waaminifu hasa
pale wanapokutana na vishawishi vya fedha, magari na nyumba za kifahari,
kazi nzuri na mengineyo kama hayo.
Hao wanadai kuwa hata mwanamke umwonyeshe upendo kiasi gani, akikutana
na mwanamume mwenye fedha chafu atakayemhakikishia kuishi katika nyumba
ya kifahari, kutembelea gari la kifahari na mengine kama hayo, lazima
atamsaliti mume au mpenzi wake.
Lakini kwa wanaume, imedaiwa kuwa wao hawatabiriki, wanaweza kuonyeshwa
kila aina ya upendo na wake au wapenzi wao, lakini bado wakaendelea
kujihusisha kimapenzi na wasichana wengineo, hasa wale wenye mvuto wa
kisura na kimaumbile.
Kwa kifupi, wanaume wamelalamikiwa na wanawake kwa tabia zao za
kutoridhika na walivyonavyo, wakitamani kila wakionacho mbele yao yaani
kila mwanamke anayepita mbele yao hutamani ‘kumvua nguo’.
Lakini kwa mujibu wa tafiti mbalimbali, inadaiwa kuwa wanawake ndio
wenye mapenzi ya kweli kiasi kwamba wanapowapenda wanaume, huwapenda
kweli kweli.
Lakini pia, wapo wanaosisitiza kuwa wanaume ndio wenye mapenzi ya dhati
kiasi kwamba wanapopenda hupenda kweli na si maigizo kama ilivyo kwa
wanawake.
Naamini mada ya leo itakuwa imewagusa wengi hivyo nitoe nafasi kwenu
wasomaji wangu kutoa maoni yenu kabla ya kuwaletea ukweli juu ya mada
hii kutokana na tafiti mbalimbali zilizofanywa na wataalamu wa mambo ya
mahusiano. Maoni yenu nitayatoa katika toleo la Jumamosi hii.
Lakini hebu niwape kibwagizo cha mada ya leo kutoka kwake Michael
Bolton, mmoja wa waimbaji mahiri wa nyimbo za kimapenzi wa Marekani
aliyejizolea sifa na tuzo kede kede.
Bolton, katika wimbo wake wa When A Man Loves A Woman, anaelezea jinsi
inavyokuwa pale mwanamume anapompenda mwanamke. Pata uhondo wa kibao
hicho matata.
No comments:
Post a Comment