TUMSHUKURU Mwenyezi Mungu ambaye ametuwezesha kuonana tena tukiwa
wazima. Lakini pia tumshukuru kwa kutuletea kitu kinachoitwa mapenzi.
Mapenzi yamekuwa yakichukua nafasi kubwa sana katika maisha yetu ya kila
siku na yamekuwa yakichangia kwa kiasi kikubwa furaha kwa kila mtu.
Kama huamini, angalia wale waliotokea kupenda na wao wakapendwa, utabaini nyuso zao zimetawaliwa na
furaha isiyo na kifani. Lakini mapenzi hayo hayo yamekuwa ni chanzo cha vilio kwa baadhi ya watu.
Mpenzi msomaji wangu, kupenda hakuna macho! Moyo ukishapenda hausikii la
kuambiwa. Katika hili ndiyo maana unaweza kumuona mwanaume kazimika kwa
demu ambaye hawaendani kabisa lakini moyo wake ndiyo umeshapenda.
Ilishawahi kutokea msichana akampenda kijana mmoja ambaye ni fukara
kupita maelezo. Yeye akawa ndiyo anamhudumia kwa kila kitu. Akamfanyia
mpango wa ajira na mwisho wake wakafunga ndoa.
Sasa hivi wanaishi maisha ya furaha na amani. Wamegeuka mfano wa kuigwa
kwa jinsi wanavyopendana lakini huko nyuma msichana huyo alikuwa
akichekwa kwa kutoa penzi kwa mwanaume asiye na mbele wala nyuma.
Hayo ndiyo mapenzi jamani! Lakini pia katika kufurukuta kumtafuta mpenzi
wa kuwa naye maishani, mwanaume anaweza kujikuta unaangukia kwa demu
ambaye tayari ana mpenzi wake.
Moyo wako unakuambia yeye ndiye mtu sahihi katika maisha yako lakini tayari ana mtu wake, unafanyaje ?.
Utapambana kuhakikisha unapata kile ambacho moyo wako umekipenda au
utakubaliana na ukweli kwamba huwezi kuwa naye kwa kuwa ana mtu wake?
Inapofikia hatua hiyo unaweza kujikuta upo njia panda hasa pale ambapo
huyo mwenye mtu wake naye anaonesha kuwa na chembechembe za mapenzi
kwako.
Kuna mambo kadhaa ya kukusaidia kukabiliana na hali hii.
Chunguza.
Tumia muda wako mwingi kuchunguza juu ya uhusiano wake. Uhusiano wao
umesimama na wanaonekana ni watu wenye ‘future’? Nasema hivyo kwa
sababu, yawezekana uhusiano wa huyo uliyetokea kumpenda ni wa kuzuga tu
na huenda wewe ndiye mwenye ‘future’ naye. Ndiyo maana nikasema chunguza
uhusiano wake kwanza.
Usitafute uadui.
Baada ya kuchunguza, ukibaini kwamba uhusiano wao hauko ‘siriasi’, vuta
subira, lolote linaweza kutokea na likaufurahisha moyo wako. Lakini kama
utaona ni watu walio siriasi na wanaelekea kuoana, usitafute uadui
bure, kaa pembeni.
Una nafasi kwake ?.
Sawa umetokea kumpenda msichana aliye na mtu wake, umeshawahi kujiuliza
kama una nafasi ndani ya moyo wake? Anaonesha dalili fulani za kukupenda
kama unavyompenda na ni mtu anayeonesha kukumisi anapokuwa mbali na
wewe? Utakapobaini una nafasi kwake, uamuzi wa kumpotezea hautakuwa na
nafasi.
Ni rahisi kubadili uamuzi wake ?.
Unadhani huyo uliyetokea kumpenda anaweza kubadili maamuzi ya kumuacha
huyo aliyenaye kama kweli hawana ‘future’? Utagundua hilo kwa kuongea
naye na kumsikia kama anaweza kufanya maamuzi hayo ili awe na wewe.
Pingana na moyo wako
Ifike wakati upingane na moyo wako. Unajua moyo wako kukuambia kuwa
unataka kuwa na uhusiano na demu ambaye tayari ana mpenzi wake wakati
mwingine utakuwa unakupotosha.
Kwa hiyo ukiona vipi, pingana nao. Acha kumng’ang’ania msichana mwenye
mpenzi wake licha ya ukweli kwamba, huenda wewe ndiye mwenye nafasi ya
kuwa mume wake na siyo huyo aliye naye.
Urafiki ni poa ?.
Umempenda sana na hauko tayari kumkosa katika maisha yako lakini
imetokea kwamba tayari yuko na mtu na umebaini huna nafasi kwake kabisa?
Usiumie, omba angalau urafiki. Siyo urafiki wa kivile sana ila angalau
pale unapotaka kusikia sauti yake kwa kumsalimia tu, upate nafasi hiyo.
Usiumie, yupo mwingine.
Haina haja ya kujitafutia vidonda vya tumbo bure kwa kuwa tu umebaini
uliyetokea kumpenda tayari ana mtu. Chukulia ni hali ya kawaida, mademu
wazuri ambao wanaishi singo wapo kibao huko mtaani, ni suala la wewe
kutulia tu. Amini yupo mwingine ambaye atayafanya maisha yako yawe ya
furaha.
Naomba nihitimishe kwa kusema kwamba, unapotokea kumpenda mtu fulani,
pambana kuhakikisha unampata kwa sababu ukimkosa maisha yako yanaweza
kuwa gizani. Ila pale utakapoona uwezekano wa kuwa naye haupo,
usilazimishe ndugu yangu. Kumbuka haya ni maisha tu!
No comments:
Post a Comment