Kama mwanaume lazima upate wakati wa kujua unatakiwa kufanya nini kwa ajili ya kulifanya penzi lako lizidi kuchanua.
USAFI BINAFSI
Asilimia kubwa ya wanawake wanapenda sana usafi. Ni aghalabu sana
kukutana na mwanamke asiyejipenda. Ndiyo maana wanaitwa mapambo ya
nyumba au la nyumba! Ni kwa sababu ya hulka yao ya kupenda sana usafi.
Mwanamke anavutiwa sana na mwanaume mtanashati. Usafi wako unamfanya
ajiamini kuwa na wewe. Hata nyumbani kwako, lazima uishi katika nyumba
safi. Hata anapokuja kukutembelea, anakuta mazingira masafi kuanzia
sebuleni hadi chumbani.
Anapokukuta katika hali ya usafi, inakuwa rahisi zaidi yeye kuanzia hapo alipokukuta na kuendelea mbele.
KUJIAMINI
Mwanamke anajisikia salama zaidi akiwa na mwanaume ambaye anajiamini –
mwenye uwezo wa kutetea hoja zake na kujieleza sawia. Siyo anayebabaika.
Suala la msimamo binafsi, kwa mwanamke ni kubwa kuliko hata kumnunulia
manukato mapya!
Mathalani unakuwa naye katika mtoko, angependa kukuona ukiwa katika hali
halisi ya maisha yako, usiyeyumbishwa na mwenye kutoa maamuzi
yasiyoyumba.
Wakati mwingine, mwanamke anaweza kukupima hata katika jambo ambalo
amekosea yeye, ataangalia unavyotoa maamuzi yako, lakini pia atafuatilia
kuona kama utakuwa mwepesi wa kuyabadilisha.
Anataka kuona msimamo wako muda wote. Mwenye kujiamini na mawazo yasiyo na matege wala makengeza!
KUJITETEA
Kipengele hiki hakina tofauti kubwa sana na kilichopita, lakini hapa ni
kwenye upande wa kujitetea zaidi. Wakati unapodai haki yako mbele ya
mwanamke wako, suala la kujitetea linapewa nafasi kubwa sana.
Wanawake hawapendi kuwa na wanaume ambao wapo tayari kuonewa. Wanataka
wenye uwezo wa kusimama kidete kuona haki zao hazichukuliwi kirahisi.
Hili si suala la kutetea tu haki yako pekee kama mwanaume, bali
inapobidi kusimamia haki ya mwanamke wako. Nisieleweke vibaya katika
hili, lakini mwanaume imara ni yule ambaye ana nguvu – anafanya mazoezi
na ambaye yupo tayari kwa lolote!
Inapowezekana, uwe na uwezo wa ‘kuzichapa’ ikiwa mtakutana na vibaka au
watu wabaya wenye lengo wa kukudhuru/kuwadhuru au kumdhuru mpenzi wako.
Mwanaume aliye ‘fiti’ ni chaguo la wanawake wengi. Si mnyonge. Mpole kupitiliza na aliye tayari kuonewa! Huyu hana nafasi.
KUJALI
Wanawake wanapenda sana wanaume wanaojali. Wanawaona wao ni kila kitu na
wanaotoa kipaumbele kwao. Kama huna tabia hiyo, ujue upo katika nafasi
kubwa ya kumkwaza mpenzi wako. Mjali mpenzi wako kwa kila hali.
Kumjulia hali kila wakati na kutaka kujua maendeleo yake, kutakupa nafasi kubwa sana ya kuendelea kudumu katika uhusiano hai.
UKARIBU
Kati ya vitu vinavyowapa mshawasha mkubwa wanawake ni pamoja na
kusogezwa karibu. Hapa ni kuwa naye katika mambo mengi unayoyafanya kila
siku.
Ni vizuri kuwasiliana naye mchana, ukitaka kujua aina ya chakula
alichokula siku hiyo au ikiwezekana mchagulie. Ni mambo madogo sana
lakini yanayoongeza nakshi katika mapenzi.
Yapo mengi sana ambayo kwa kuyafanya utakuwa umemsogeza mpenzi wako
karibu yako. Hebu tumia ubunifu wako ili uweze kuteka hisia za mwenzi
wako kisawasawa!
KUMSIFIA
Wanaume wengi hupuuzia hili, huona kama ni jambo lisilo na maana sana
kwao na wenzi wao. Hali ni tofauti sana kwa wanawake ambao hupenda
kuwasifia wanaume zao. Nitakupa mifano miwili ya namna wanandoa wa
jinsia mbili tofauti wanavyotambulishana kwa jamaa zao.
MWANAUME: “Peter kutana na mke wangu, anaitwa mama Diana. Nipo naye
mwaka wa tatu sasa, tuna watoto wawili, huyo Diana na mwingine anaitwa
Cris. Mama Diana, huyu ni Peter nilisoma naye A – Level, Tosamaganga
Sekondari.”
MWANAMKE: “Suzan, huyu ndiye mume wangu mpenzi...anaitwa Elifaraja
lakini mimi napenda zaidi kumuita Elly. Kiukweli nampenda sana mume
wangu jamani, tuna mtoto wetu mmoja, anaitwa Agness. (Akimgeukia mumewe)
Baby, huyu hapa ni rafiki yangu Suzan. Yaani tumekua naye mtaa mmoja
huko Arusha.”
ANGALIA TOFAUTI
Bila shaka kwa namna wawili hao walivyotambulishana unaweza kuona
tofauti kubwa. Mwanaume amemtambulisha mkewe kawaida kabisa, hajaonesha
manjonjo au namna anavyompenda na kumthamini mwenzake, lakini mwanamke
amefanya hivyo.
Sikia nikuambie, KUMSIFIA mwanamke, kuna nafasi kubwa sana kwake.
Chunguza kwa makini, hata kunapokuwa na mgongano katika familia, halafu
wakatokea wageni, baada ya utambulisho na mazungumzo ya hapa na pale,
wageni wakiondoka kunakuwa na uwezekano mkubwa zaidi wa kumaliza mpasuko
katika familia.
Jenga utamaduni wa kumsifia mpenzi wako, unamuweka katika kilele cha
upendo. Anajiona kamili, peke yake na mwenye nguvu kwako. Anajiamini na
unamfanya azidi kukupenda kwa kuwa anaamini yupo na mwanaume ambaye
anajivunia kuwa naye.
MALENGO
Wanaume wengi wana ulemavu mmoja; hawapendi kuwashirikisha wanawake
katika mambo yao. Wanapenda kufanya mambo yao kwa siri na wakati
mwingine ikilazimika kumwambia mkewe basi kwa mshtukizo baada ya
kukamilisha jambo husika.
Hii si sahihi. Dunia ya leo imebadilika rafiki zangu. Inawezekana wazee
wa zamani walikuwa sahihi, maana ilikuwa ni suala la kununua ng’ombe na
kuwaweka katika zizi kwenye kijiji cha jirani, halafu wanapewa malisho
mazuri, baada ya miaka miwili wanazaliana, hapo ndipo anamweleza mkewe.
Siku hizi dunia imebadilika, kuna mambo mengi. Kuna suala la hasara
katika biashara, utapeli n.k. Mkeo ndiye rafiki yako mkubwa kuliko wote,
ndiye ndugu yako wa karibu zaidi kuliko yeyote. Yes! Mkeo ndiye ndugu
yako maana umetengeneza naye familia. Mmeshirikiana kuzaa watoto na
kujenga maisha pamoja.
Yeye anapaswa kujua mambo yako, ndiye mtetezi wako nambari wani. Mweleze
juu ya malengo yako, wakati mwingine anaweza kukusaidia sehemu ambayo
hukutarajia.
Hata hivyo, kumshirikisha katika malengo yako, kunampa nguvu na nafasi
ya kujiona mama katika familia yenu. Msaidizi kamili wa nyumba yenu.
KIPAUMBELE
Kuna wakati wanawake huwa na mambo yao binafsi. Kazini au kifamilia.
Inawezekana akatatizika katika eneo fulani ambalo kwa namna moja ama
nyingine atahitaji usaidizi wako. Ikitokea mkeo akawa katika hali hiyo,
msikilize.
Mathalani ana tatizo la kifamilia, amekuambia mmoja wa wazazi wake
anaumwa, msaidie. Si lazima kifedha, lakini kuonesha kujali kwako tu,
kutampa matumani kwamba anaishi na mtu sahihi. Acha kupuuza mambo yake;
hata yale madogo, kama ya ‘mtoto wa dada amerudishwa ada shuleni’.
Msikilize, mshauri panapofaa kufanya hivyo na ukiweza msaidie hata
kifedha. Katika upande wa pili ni hivyo hivyo. Labda una tatizo binafsi,
kazini kwako au kifamilia, mshirikishe.
Unaweza kushangaa jambo ambalo uliamini unaweza kulimaliza peke yako,
kwa kumshirikisha likawa jepesi zaidi na mambo yakaendelea vyema.
Kipaumbele kwa namna yoyote ile, kunaongeza mapenzi zaidi kwa mwanamke.
TENDO LA NDOA
Hiki ni kipengele nyeti, kinachohitaji lugha nzuri ya kirafiki
kukifafanua. Hakuna siri, tendo la ndoa ni moja ya kiwakilishi cha ndoa.
Maana hata maandiko yanasema: “Mwanamke ataacha wazazi wake na kwenda
kwa mumewe, nao watakuwa mwili mmoja.”
Kimsingi tendo la ndoa lina nafasi yake. Ni muhimu likaheshimiwa na
kutengewa muda maalum wa kufurahia. Si papara. Kwa bahati mbaya wanaume
huwa si wafuatiliaji sana wa kujua namna ya kuwafurahisha zaidi wenzao.
Wenyewe wanajiwazia wenyewe. Wanafikiria namna ya kuwakomoa wenzao.
Si sahihi.
Tendo la ndoa halina maana ya kukomoana. Jenga mazoea ya kufanya
maandalizi kamili kabla ya tendo. Sikiliza hisia za mwenzako. Ukiweza
kumjulia mke wako katika eneo hili, ni wazi kwamba utazidisha upendo
wake kwako, lakini pia atakuwa katika kuta za uaminifu. Akatafute nini
nje wakati wewe ndiye mganga wake unayeweza kumtibu barabara?
Kuna kitu nimesahau kweli? Kama kipo nitafute pembeni, kwa hapa haya
yatoshe kukufanya uelewe nilichotaka kukuelekeza. Nikuache na neno moja;
uamuzi wa kuijenga ndoa yako upo mikononi mwako. Ukitaka iwe
shaghalabaghala, pia ni wewe tu!
No comments:
Post a Comment