Mzee mmoja mwenye umri wa miaka 70 katika kaunti ya Homa Bay nchini
Kenya, amejitoa uhai baada ya kuachwa na mkewe wa pili kwa kumkimbia na
kumuachia upweke wa hali ya juu.
Tukio hilo limetokea wiki hii baada ya mke wa mzee huyo Samuel Oloto
Onjoga, kutoroka nyumbani katika hali isiyoeleweka na kwenda kuishi
katika soko lililo karibu, kitendo kilichomuachia upweke na huzuni.
Chifu wa eneo hilo, Bw Joseph Ndege ameviambia vyombo vya habari kwamba
Bw. Onjoga alijitia kitanzi kwa kutumia kamba ya mkonge kwenye mwembe
ulioko nyumbani kwake.
"Tulimpata akining’inia kwenye mwembe ulio kando ya nyumba yake,
alitumia kamba ya mkonge kujinyonga, mzee huyo alikuwa na upweke baada
ya mke wake wa pili kumtoroka na kwenda kukodisha nyumba katika soko
lililo karibu baada ya kuzozana,” amesema Chifu huyo.
kwa mujibu wa wanakijiji wenzake mke wa kwanza wa marehemu alifariki
miaka mitano iliyopita, na kuoa mke huyo wa pili miaka miwili iliyopita,
na kwamba huenda mzee huyo ambaye ni mfanya biashara wa mifugo alipatwa
na matatizo ya kimawazo kwa kuishi peke yake nyumbani, ilhali alikuwa
pia na matatizo ya kiafya.
Kamanda wa polisi wa Kaunti ya Homa Bay, Bw Marius Tum, amesema polisi
wameanzisha upelelezi kubainisha ukweli kuhusu kifo hicho, huku mwili
wake ukihamishwa katika mochwari ya hospitali ya kaunti ndogo ya
Rachuonyo kusubiri kufanyiwa upasuaji wa kubainisha chanzo cha kifo.
No comments:
Post a Comment