Kwenye mapenzi kuna nyakati za kutofautiana, kukasirishana. Katika hali
ya kawada kipindi hiki huwa ni za hatari kwa sababu husababisha nyufa
kubwa za uhusiano na kulifanya penzi kukosa ladha.
Sote tunajua, watu hupigana, huachana, hujeruhiana, hutukanana,
hudhalilishana wakiwa na hasira. Hata hivyo si wote wanaojua wafanye
nini wanapojikuta wameingia kwenye hatua hiyo mbaya.
Msomaji wangu, hebu jaribu kukumbuka ugomvi mmoja uliotokea kati yako na
mpenzi wako na ikiwezekana jikumbushe mlivyoanza! Utabaini kuwa mlianza
kama utani na mkajikuta mmefura kwa hasira, mkatwangana makonde,
mkatamkiana maneno makali ya kuudhi na pengine mkaamua kuachana.
Yote hii ni kwa sababu mlikosa elimu ya mazungumzo. Ingekuwa mmoja wenu
hasa yule aliyekuwa wa pili kukasirika anafahamu hatua za kuzungumza na
mtu aliyekasirika angechukua jukumu la kutuliza machafuko na kuleta
amani kwenye mapenzi. Tazama hatua tano za kuzungumza na mpenzi
aliyekasirika. MPUNGUZE MHEMKO
Hasira hujaza kifua, huathiri mzunguko wa damu na ufahamu. Mtu
aliyekasirika huwa vigumu kwake kusikiliza au kutazama mambo kwa jicho
la tatu. Mwenye hasira huwa hafikirii matokea yajayo badala yake
hutazama zaidi tukio na jinsi ya kupata ushindi iwe kwa maneno au kwa
mapambano.
Katika hali ya namna hiyo, mtu mwingine akija na busara za kutaka
kumgeuza haraka haraka hawezi kumuelewa. Muhimu hapo ni kuacha
kumwadama, kujibizana naye, kumshawishi asikilize badala yake mpe nafasi
ya kusema atakavyo, abwate ajuavyo huku wewe ukimuitikia na kumkubalia
lawama zake. “Basi mpenzi mwenye makosa ni mimi.” Kauli za aina hii
zitampunguza hasira kwani atajiona msindi. MSOME SAIKOLOJIA YAKE
Kwa kuwa unamfahamu mpenzi wako kwa kina itakuwa rahisi kwako kumtambua
kuwa amepunguza hasira na kurudi katika hali yake ya kawaida. Ukisha
fahamu hilo chukua jukumu la kumsoma kisaikojia ili kujua kama yuko
kwenye hali nzuri ya kusikiliza yale uliyotaka kumwambia wakati
alipokuwa na hasira.
Zoezi hili linaweza kuchukua saa kadhaa na wakati mwingine hata siku
mbili. Lengo ni nini? Ni kupata matokeo sahihi ya kuondoa chuki za
mwenza wako na kumfundisha madhara ya kukasirika kwenye uhusiano wenu wa
kimapenzi. “J, nakupenda sana, lakini juzi uliniumiza, uliniambia mimi
malaya kwa kosa ambalo sikufanya?” Bila shaka muda huo atakusikiliza
zaidi kuliko ungebishana naye alipokuwa na hasira.
MRUHUSU AKUJIBU
Pamoja na kumsoma kisaikojia na kumwambia kinagaubaga makosa yake,
usimzuie kujitetea, mpe nafasi ya kuzungumzia kilichomkasirisha. “Unaona
bado unanitukana, sasa naamini siku ile ulikuwa umedhamilia.” Usisiseme
hivyo, mwache ajibu hoja hata kama atakuwa anakukandamiza na kuzidi
kujijengea ushindi. Mvumilie aoshe ubongo wake.
EPUKA MARUMBANO
Kama nilivyosema kwenye hapo juu, wapenzi wengine huwa wagumu kuelewa,
ni watu wa kuficha udhaifu wao na kutopenda kuonekana wamekosea. Watu wa
namna hii unapowarejeshea mazungumzo wanaweza kujikuta wanahamaki tena.
“Kwa hiyo ulikuwa unasemaje…nilifanya ndiyo,… wewe unaamuaje?” Mkifika
kwenye alama hiyo usikubali kurumabana naye mwache aseme halafu wewe
ingia kwenye hatua ya tano.
MUOMBE MSAMAHA
Hata kama atakuwa yeye ndiye mwenye makosa na amekataa kukiri, usijali,
chukua jukumu la kumuomba msamaha na kueleza tena nia yako ya
kumazungumzo ilikuwa ni kuelewana si kugombana. Kumbuka hata kama
amekiri kosa, bado unatakiwa kumuomba radhi kwa kurejea yaliyopita.
“Mpenzi inawezekana nikawa nimekuudhi kwa niliyosema, nakuomba sana
tusameheane.”
Bila shaka kwa haya machache msomaji wangu utakuwa umejifunza na
kuchukua hatua za kuzuia migogoro mikubwa inayotokana na hasira za
mpenzi wako. Leo niishie hapa, nikushukuu kwa kunisoma. Kaa mkao wa
kura, kile kitabu bora cha mapenzi nchini TITANIC, TOLEO LA NNE,
kitakuwa mtaani hivi karibuni. Usikose nakala yako.
No comments:
Post a Comment