HAKUNA kitu kibaya maishani kama kuonekana upo katika daraja la chini na
mtu wa kudharaulika kwenye jamii unayoishi. Kisaikolojia kuna madhara
makubwa.
Ni imani yangu kuwa kila mwanadamu timamu anapenda kuheshimiwa lakini
wengi wetu tunashindwa kupata heshima tunayoitaka kwa sababu hatufahamu
jinsi ya kuishi mbele ya wenzetu.
Kitaalamu, hakuna jambo ambalo hutokea maishani bila sababu maalumu
hivyo hata kudharauliwa kwako au kwetu ndani ya jamii tunayoishi
kunatokana na jinsi tunavyoenenda.
Mwalimu wangu wa somo la maisha na saikolojia, Eric Shigongo, aliwahi
kuniambia ‘Nothing happens in the sky, but the elements should be
there,’ akimaanisha kuwa hakuna kitokeacho angani pasipo kuwa na dalili
au sababu zake.
Naomba nianze kutoa njia za kukusaidia kurejesha heshima yako kwa
kuperuzi na wewe baadhi ya dokezo muhimu zinazoweza kukusaidia
kujitambua na kuweza kuyaepuka maisha ya kudharauliwa. MUONEKANO
Kwanza kabisa ni jinsi unavyoonekana. Muonekano ninaouzungumzia hapa ni
usafi wa mavazi na mwili kwa ujumla. Hata siku moja hakuna mchafu
anayeheshimika katika jamii anayoishi hata kama ana kipaji kikubwa kiasi
gani.
Kwa hiyo uchafu wa mavazi na mwili huchangia mtu kudharauliwa katika
jamii anayoishi. Linaweza kuwa jambo dogo sana lakini ni moja kati ya
sababu kubwa inayochangia kuporomoka kwa thamani yako mbele ya wenzako.
Mazungumzo
Hapa naomba nieleweke kuwa unachokizungumza kinaweza kukujengea heshima
au kukubomolea heshima. Kauli zisizo na busara zitakufanya udharaulike
kwa kila mtu. Uropokaji usiokuwa na mantiki huchangia kuporomosha
heshima yako hasa kama utakuwa muongeaji zaidi. Biblia inasema penye
wingi wa maneno hapakosi uovu.
UTENDAKAZI WAKO
Ndugu zangu, siku zote heshima ya mtu ni kazi. Watu wengi hawapendi
kufanya kazi kwa bidii huku wengine wakijiendekeza kwa tabia ya
kuombaomba, jambo hilo halifai kwa vile huchangia kubomoa heshima yako
mbele ya jamii. Fanya kazi usiishi bila kujishughulisha.
KUTOTIMIZA AHADI
Kama una tabia za kuahidi mambo halafu unashindwa kuyatekeleza, basi
unajiweka katika nafasi mbaya ya kutunza heshima yako katika jamii
unayoishi. Bora ukwepe kutoa ahadi kuliko kuahidi na kutotimiza.
SIFA ZISIZO NA MAANA
Nakumbuka msemo mmoja kutoka kwa mwandishi mwandamizi aliyekuwa mtaalamu
wa falsafa za maisha, marehemu Adolf Balingilaki, ambao unasema kwamba:
“Ukitafuta heshima kwa gharama ya juu, basi utalipwa dharau kwa bei nafuu.”
Msemo huu unamaanisha nini? Siku zote ukiwa unafanya mambo yako kwa
ajili ya kusifiwa au mazungumzo yako kuwa ya kujiinua, watu
watakudharau.
KUTOKUWA MWAMINIFU
Suala la uaminifu ni pana, kuna uaminifu wa fedha, siri, dhamana na
mambo kama hayo, hivyo ni vema kila unachoaminiwa lazima ukitunze kwani
ukiwa mtu wa kuvunja uaminifu fahamu kuwa utashusha heshima yako.
No comments:
Post a Comment