SIKU hizi ugomvi kwenye mahusiano imekuwa kama ni jambo la kawaida. Watu
wanagombana kwelikweli. Utakuta mtu haipiti mwezi mmoja bila kugombana
na mpenzi wake. Anampenda, hayupo tayari kumpoteza lakini maisha yao
kila siku ni ugomvi. Mara nyingi ugomvi unapotokea, ladha ya pendo
hupungua.
Inachukua muda kurudi kwenye upendo wa awali mara baada ya wapendanao
kugombana. Wahusika wanakuwa wanaukataa ugomvi lakini wapi, baada ya
muda unatokea. Nimekuwa nikipokea malalamiko mengi kutoka kwa wasomaji
kuhusu suala zima la ugomvi.
Ngoja ‘tushee’ hapa kwa pamoja ujumbe huu kutoka kwa dada mmoja
aliyejitambulisha kwa jina la Sasha: “Kaka naomba msaada wako, nimekuwa
nikigombana mara kwa mara na mpenzi wangu. Imefika mahali hadi napoteza
kabisa hamu ya mapenzi. Hata ninapotaka kukutana naye, nawaza tu lazima
kutatokea ugomvi.
“Wakati mwingine naamua kumuepuka kwa kutokutana naye au kutomsemesha
kabisa. Napata furaha ninapokuwa peke yangu kuliko ninapokuwa na mpenzi
wangu, inafika mahali mpaka nawaza niachane naye au vipi, naomba
nisaidie kaka.”
NINI CHA KUFANYA?
Unapokutana na hali kama hiyo, unapaswa kutulia na kufanya maamuzi
sahihi. Usikurupuke. Jiulize ni nini hasa kinachosababisha mgombane?
Sema vizuri na moyo wako. Usijipendelee, kama unaona kuna kitu
kinachosababisha mgombane na wewe ndio chanzo unapaswa kukishughulikia.
Kama unaona kuna kitu mwenzako anakikosea, tafuta muda ambao mpo kwenye
furaha na uzungumze naye kwa lugha rafiki. Muoneshe kwamba haipendezi
mnapokuwa mnagombana mara kwa mara. Mueleze kwamba mnapofanya hivyo
penzi lenu linapoteza msisimko. Mueleze kwamba ni hatari kuishi katika
malumbano maana ni rahisi kujikuta mmeachana. Mfahamishe kwamba kama
wote lengo lenu ni moja, kufika mbali kimahusiano kuna sababu gani ya
kulumbana kila siku? Mnagombea nini?
CHUKULIANENI
Hili ndio somo muhimu katika mazungumzo yenu. Mueleze kwamba ili muweze
kuishi vizuri mnapaswa kuchukuliana upungufu. Nyinyi mmekutana ukubwani.
Kila mtu amelelewa katika maadili tofauti. Amekulia katika mazingira
tofauti na mkaungana kutengeneza umoja wenu. Mnapaswa kuzungumza lugha
moja. Kila mmoja amsome mwenzake kwamba nini anapenda na nini hapendi.
Kitu gani huwa kinamuudhi mwenzako? Ukishakijua, epuka kumfanyia maana
umeshajua hiyo ndiyo sababu ya nyinyi kugombana.
VUMILIANENENI
Kutokana na kila mtu kuwa na tabia na hulka zake, mnapaswa kuvumilia.
Inawezekana kabisa mwenzako akawa na tabia flani ambayo kimsingi si
njema lakini unachotakiwa kufanya ni kuibeba. Ishi naye kwa kuirekebisha
taratibu. Tumia mbinu za kuzaliwa kumfanya abadilike. Mathalani,
unaweza kumchukulia filamu yenye mafunzo kuhusiana na tabia yake na
kumuwekea bila kujua kama umemfanyia makusudi. Unaweza pia kumpa
majarida mbalimbali au magazeti yenye ujumbe unaohusu tabia yake naye
akajifunza.
MFANYE AWE RAFIKI
Kumfanya mpenzi wako awe rafiki yako kutakufanya ujue mpenzi wako
anapenda nini na nini hapendi. Hakikisha unakuwa naye karibu,
mnazungumza kama marafiki hivyo kukupa mwanya mzuri wa kumuelewa vitu
ambavyo huwa havipendi. Unapomweka karibu, anaweza kuwa anakusimulia juu
ya mtu flani ambaye amemkwaza labda kwa kumfanyia jambo flani, ni
rahisi na wewe kugundua kwamba hapendi kufanyiwa jambo hilo, ukaepukana
nalo.
KUVUMILIANA KUNA KIWANGO
Fanya hayo yote lakini ukiona mnashindwa kabisa kuendana tabia na kila
siku mnaendelea kugombana basi ni bora ukajiengua katika uhusiano huo.
Utampata ambaye mnaendana. Vumilia katika kipindi flani, mbadilishe pale
inapobidi kwa kutumia mbinu mbalimbali lakini mwisho wa siku ukiona
haiwezekani, achana naye.
No comments:
Post a Comment