Alex alishikilia simu yake akijaribu
kumpigia mkewe lakini simu iliita bila kupokelewa, alionekana kuwa na
wasiwasi sana mpaka mfanyakazi mwenzake akamuuliza.. “Vipi, mbona una
wasiwasi sana, kuna nini?” Bila kuongea alitingisha kichwa kuashiria kua
hakuna kitu. Lakini kadri kadri gari ilivyokuwa inachanja mwendo ndivyo
alivyozidi kuwa na wasiwasi mpaka akashindwa kuvumilia.
“Mkuu samahani mnaweza kuniacha hapa
nikarudi nyumbani kidogo, nitakuja na basi?” Alex alimuuliza Bosi wake
ambaye alikua amekaa siti ya mbele, walikua na wafanyakazi wenzake
wakielekea Morogoro kwenye sherehe ya mfanyakazi mwenzao. “Kwani kuna
shida gani, kuna nini? Bosi aliuliza kwa wasiwasi… “Hakuna kitu mkuu, ni
nyumbani tu kule, sijaagana na Mama vizuri..sasa….”
Hakumalizia kuongea wafanyakazi wenzake
walianza kucheka na kumtania, nikweli walikuwa wakifahamu namna
alivyokuwa akimpenda mkewe na yeye mara nyingi hakuficha mapenzi yake.
Walijaribu kumshawishi lakini Alex alikataa katakata na kushuka,
walikuwa wameshakaribia Ubungo hivyo alichukua bodaboda aili kuwahi
nyumbani Temeke alipokuwa akiishi na mkewe.
Wakati wa kuondoka walikuwa
wamekorofishana kwani mkewe alitaka kwenda kwenye ile sherehe na yeye
alisisitiza kuwa ni kwaajili ya watumishi tu. Kilichomfanya mkewe
kukasirika nikuwa mke wa mfanyakazi mwenzake alimuambia mkewe kuwa
anaenda Morogoro hivyo mkewe kuona kama alikuwa anadanganywa.
Alex alirejea nyumbani na kumkuta mkewe
akiendelea na shughuli za pale. Mkewe alishangaa kumuona lakini
alimuambia “Nimeshindwa kuondoka tukiwa tumenuniana, safari ina mengi
lolote linaweza kutokea, sitaki kumbukumbu yangu ya mwisho kwako iwe ni
kukorofishana, naomba unisamehe na kama hutaridhika basi sioni hata haja
ya kwenda hiyo safari…”
Mkewe alistuka kusikia vile,
alimuangalia mumewe na machozi kuanza kumtoka. Nikweli walikuwa
wakipendana lakini hakujua ni kwakiasi kile. “Nenda kwa amani mume
wangu, Yale yameshaisha ni mimi mwenyewe nilichanganya kumbe
aliyeniambia mwenyewe anaenda kwa upande wa mke alialikwa huko na haendi
na mumewe, nilishasahau hayo na nilipanga ukifika nikupigie simu..”
“Whoooo!…” Alex alipumua kuashiria
kupata nafuu na ahueni flani. “Nilifikiri bado umekasirika hasa
nilipokuwa nakupigia simu hupokei..?”
“Simu! Hata sijaisikia mume wangu…
nimeiacha ndani kwenye chaji hata sijui kama ilikuwa inaita…” Aliongea
huku akitabasamu. Alex alimkumbatia mkewe kisha akapanda bodaboda ile
ile ili imuwahishe Ubungo apande magari ya Morogoro. Nikweli aliwahi na
kupata gari akaanza safari.
Walipokua wanakaribia Mikese, kilometa
chache kutoka Morogoro Mjini walikutana na ajali, gari dogo iliyokuwa
ikitokea Dar iligongana uso kwa uso na lori la mizigo na kupinduka.
Magari yalikua yamesimama kwani bado lori lilikua halijaondolewa. Watu
walishuka na alipofika chini alikuta gari dogo ambalo liligongana na
lori lilikua ni gari la ofisini ambalo lilikuwa wafanyakazi wenzake wane
na wote wlaifia palepale.
Alex alikua ni mtu wa tano ambaye
alipaswa kuwepo katika lile gari. Hakuamini kuwa upendo wake kwa mkewe
ndiyo uliokoa maisha yake, alipiga magoti palepale kumshukuru Mungu,
hakuna kitu ambacho angeweza kufanya kwa wafanyakazi wenzake, machozi
yalimtiririka kama maji, akiwamabia watu aliapswa kuwepo kwenye ajali
ile lakini Mungu alimuokoa. Alimpigia simu mkewe na kumshukuru kwa
upendo waliokuwa nao ambao uliyaokoa maisha yake.
*****MWISHO*****
No comments:
Post a Comment