Ndoa ni kitu ambacho naamini kila
mwanamke anakitamani, kuna umri katika maisha ya mwanamke ukifika akili
yake haiwazi kitu kingine zaidi ya kuolewa hasa kama anakuwa amepitia
mahusiano mengi ya kutendwa na kuumizwa. Kwangu umri huo ulifika miaka
kumi iliyopita, nikiwa na umri wa miaka 32 nilikuwa nimeshaachwa na
wanaume watano.
Nikisema kuachwa simaanishi wale wa
kuingia katika mahusiano na kuachana bali nazungumzia wale wakuwa kwenye
mahusiano siriasi mpaka kufikia hatua ya kutambulishana. Mpaka wakati
huo nilikuwa sifahamu tatizo lilikuwa nini kwani kusema kweli Mungu
kanijaaalia uzuri na mambo kule kwa sita kwa sita nayajua, hivyo kuachwa
na mwanaume kwangu kilikuwa kitu kilichoniumiza sana.
Ndoto za kuolewa zilishapotea,
nilishakata tamaa, sikutaka tena mwanaume wakuja kutambulisha nyumbani
halafu aniache kwenye mataa na kuingia kwenye aibu nyingine. Nikiwa
mfanyakazi wa Benki moja kubwa tu hapa nchini, mwenye mshahara mkubwa
nikiwa na nyumba yangu na gari nilikata shauri la kutokuolewa tena na
kuamua kutafuta mtoto.
Nilibadili kabisa wazo la kuolewa na
kuamua kuanza kutafuta mwanaume wa kuzaa naye tu. Hilo ndiyo lilikuwa
lengo langu na ili asinisumbue kwa maana ya kumtaka mtoto nilihitaji
mume wa mtu au kijana ambaye hana kazi ambaye hata nikimuambia mimba si
yake basi hatahangaika kunifuatilia au nikimuambia tu nina mimba basi
atanikana ili kukwepa majukumu.
Nakumbuka ilikuwa ni siku ya
jumatano, nikiwa kazini nimechoka, kama afisa mikopo aliingia kijana
mmoja wa makamo, akiulizia taratibu za kuchukua mkopo. Kwakumuangalia tu
nilimtamani lakini kwa mawazo yangu kuw anina gundu hata sikutaka
kuelekeza akili zangu kwake kwani kwa muonekano tu alikuwa ni kijana
anayejiweza, nilijua lazima atakuwa naamke au hata kama atakuwa
akimiliki binti mbichi kabisa hivyo hata asingevutiwa na mimi.
Alikuja tukaongea nikampa maelekezo
yote ya namna ya kuchukua mkopo, sijui nini kilitokea lakini baada ya
sisi kama Benki kutembelea biashara yake na nyumba yake aliyokuwa
akiiweka rehani mahusiano ya kimepenzi yalinzia hapo. Ndani ya muda
mfupi nilijua kijana yule alikuwa akiitwa Joseph au Jose, pamoja na umri
wake wa miaka 35 alikuwa bado hajaoa wala hakuwa na mchumba.
Mwanzo nilihisi ana matatizo
nikimaanisha labda sio riziki kwani kwa umri ule, uwezo wake wa kifedha
na muonekano wake alitakiwa kuwa ameoa, lakini nilikuja kugundua kuwa
alikuwa mzima kabisa tena mwenye shughuli hasa, tatizo lake kubwa nikuwa
alikuwa bize na kutafuta pesa kiasi cha kusahau kuoa. Tulianza
mahusiano harakaharaka na ndani ya miezi mitatu alitaka kuja
kujitambulisha kwetu.
******
Kwangu suala la kujitambulisha
ilikuwa mtihani mkubwa kwani niliwaza atakuwa sawa na wale wengine
watano, hivyo nilimkatalia katalia nikiogopa kumpoteza. Nilijifanya kama
nataka tuchunguzane kwanza mpaka aliponiambia, “Doris kwa umri nilionao
sidhani kama kuna kipya nitakigundua kwako ambacho kitanifanya
nisikuoe, nahitaji familia…” Aliongea kwa kumaanisha kiasi cha mimi
kumuamini lakini tatizo bado likawa kwangu, sikumuamini.
Kabla ya kumpeleka nyumbani
niliongea kwanza na Mama na baada ya kumueleza wasiwasi wangu niligundua
kuwa hata yeye alikuwa nao huo huo hivyo kabla ya yote aliniambia
niombe ruhusa kazini ili twende kijijjini kwetu Iringa “Tukamtengeneze
Jose kabla ya kumruhusu kuja nyumbani..”. sikubisha wala kufikiria mara
mbili, tulirudi Makete ambapo baada ya kukutana na wataalamu walinipa
dawa ya kumuwekea Jose kwenye chakula na kweli ilisaidia (nilivyoamini
mimi).
Ndani ya miezi mitatu nilifunga ndoa
ya kanisani, tena kubwa ya kifahari, baada ya kuhangaika sana kwa muda
mrefu, kupitia mateso mengi ya mahusiano hatimaye nilikuwa mke wa mtu.
Baada ya mwaka mmoja Mungu alitujalia kupata mtoto wakike na ndoa yetu
ikazidi kupata furaha, lakini bado nilikuwa sijiamini hivyo mara kwa
mara nilikuwa nikienda kijijini kuchukua dawa kwa ajili ya
‘kumtengeneza’ mume wangu na kuongeza nguvu ya penzi.
Wakati mwanangu akiwa na umri wa
miaka minne na mimi nikiwa na ujauzito wa mwanangu wapili miezi ya
mwanzo kabisa, kulitokea uizi flani pale ofisini, ingawa mimi sikuhusika
lakini ulipita uhamisho wa nguvu ambapo nilipata uhamisho wa kwenda
Kigoma, kwangu hiyo ilikuwa ni kama adhabu na nilipomuambia mume wangu
hakuwa tayari kulisikia hilo, hata mimi sikutaka kwenda mbali na mume na
kwakuwa pesa tulikuwa nayo niliamua kuandika barua ya kuacha kazi ndani
ya masaa 24.
Tulikubaliana na mume wangu
nijifungue kwanza na kumlea mwenetu kabla ya kutafuta kazi nyingine au
kufungua biashara. Katika kipindi hicho ndiyo kila kitu kilibadilika,
ile hali ya kukaa nyumbani tu ilinifanya kuwa mpweke sana mpaka kuanza
kujihisi kama sipendwi tena. Ingawa mume wangu alijitahidi kwa hali na
mali kunionyesha upendo wa hali ya juu lakini nilikuwa niki mmiss sana,
nilianza kuwa msumbufu kumpigia simu kila wakati, kutaka kuonge naye na
kutaka kujua yuko wapi.
Wakati nikiwa kazini nyakati zote za
mchana nilikuwa bize na kama mnavyojua benki tulikuwa tunachelewa sana
kutoka hivyo mara nyingi nilifika nyumbani na kumkuta amesharudi au
nikifika tu hachelewi. Baada ya kuacha kazi na kuwa Mama wa nyumbani
ingawa mida yake ya kurudi ilikuwa ileile lakini kwakuwa mchana kutwa
nilikuwa namsubiri niliona kama anachelewa.
Nilianza kuwa na gubu maugomvwi ya
hapa na pale na wivu wa kijinga, mume wangu alinielewa kwakuwa alikuwa
akijua ni sababu ya mimba na mara kadhaa hata kama alikuwa hajakosea
alikuwa akiniomba msamaha. Pamoja nakuwa alikuwa akijitahidi kunionyesha
upendo lakini sikuridhika, bado nilihisi kama ananisaliti kila
nikimuona na mwanamke tu bila kujiuliza ni nani nilipaniki. Sikuweza
kuvumilia niliamua kwenda kijijini kumuongezea dozi ili awahi kurudi
nyumbani na kunifikiria mimi tu.
******
Nilifanikiwa kupata dawa ambayo
nilipewa kwaajili ya kumuwekea mume wangu kwenye chakula nikiambiwa
nihakikishe kuwa ni yeye peke yake anakula hicho chakula. Hilo kwangu
halikuwa tatizo, usiku mmoja nilimuandaliwa mume wangu chakula kizuri
kisha nikampelekea chumbani kimahaba, mara kadhaa huwa napenda kumfanyia
hivyo, kumpikia chakula anachokipenda na sisi kula wawili tu chumbani,
hasa nyakati za usiku ambapo wengine wanakuwa wamelala.
Ili nisile naye nilijifanya naingia
bafuni kuoga, alitaka kunisubiri lakini nilimuambia sijisikii kula yaani
baada tu ya kupika nilianza kujisikia vibaya. “Mwanao sijui anaona wivu
hataki nifaidi vitu vizuri…” Nilimtania wakati nikiingia bafuni
nikisingizia mimba ndiyo haitaki kula naye. Niliingia bafuni na bila
wasiwasi nilianza kuoga, nilitumia muda mrefu bafuni ili amalize kile
chakula, lakini kabla ya kumaliza kuoga nilisikia kelele za mume wangu.
“Ritha! Ritha! Mwanangu! Mwanangu
….” Ritha ni jina la mwanangu wa kwanza, wakati namtengea mume wangu
chakula nilikuwa nimeshampandisha kitandani kulala hivyo niliposikia
jina lake linaitwa chumbani bila hata kufikiria kuvaa nguo nilitoka kama
nilivyozaliwa. Sahani ya chakula ilikuwa juu ya kitanda, huku mume
wangu akijaribu kumtingisha mwanangu aliyekuwa amelegea pale kitandani.
Bila kujijua namimi niliungana
nayeye pale kitandani nikipiga kelele za kumlilia mwanangu, alikuwa
hanyanyuki na alishaanza kutoa maudenda mdomoni. Mume wangu alimnyanyua
na kumpeleka kwenye gari, nilitoka vilevile uchi wa mnyama kutaka
kuongozana naye mpaka niliporudishwa na wifi yangu ambaye tulikuwa
tukiishi naye, alinivalisha nguo kisha wote tukaingia kwenye gari na
kuelekea hospitalini.
Mwanangu alifanyiwa vipimo vyote
lakini hakugundulika na kitu chochote, walipima na chakula alichokula
kuona kama kilikuwa na sumu lakini wapi, hakuwa na tatizo lolote. Alikaa
hospitalini kwa wiki nzima lakini hakupata nafuu, alikuwa haongei tena
na kila wakati alikuwa akitoa udenda tu. Mimi nilijua kilichokuwa
kimetokea, nilitamani kumuambia mume wangu lakini niliogopa kuachika,
nilitamani kumpigia simu mganga lakini hakuwa na simu.
Wakati nikiwa bafuni Ritha aliamka
na mume wangu bila kujua akaanza kumlisha chakula ndipo aliposhikwa na
hali ile. Ilibidi Mama kuenda kijijini kimya kimya kuongea na mganga
kuhusu ile ishu lakini haikusaidia chochote, alipewa dawa ya kumpa
ambayo hata baada ya kumpa haikusaidia na iliposhindikana sana mganga
alisema tumpeleke mtoto. Sikujua ni kwa namna gani ningeweza kumshawishi
mume wangu kumpeleka mtoto kijijini.
Lakini kama walivyosema wahenga utu
uzima dawa baada ya kumuambia Mama alienda kuongea na Mume wangu
akimuambia kuwa inawezekana yele ni mambo ya kimila hivyo kuruhusu
twende kijijini, kwakuwa hakuwa na namna na yeye alishachanganyikiwa
tuliondoka kuongozana naye mpaka kijijini mume wangu akiamini kuwa labda
mambo ya kimila ya upande wetu ndiyo yalisababisha yote yale.
Tulimpeleka kwa mganga ambaye
alihangaika naye kwa wiki mbili nzima bila mafanikio yoyote.
Ilishindikana hivyo tukalazimika kurejea Dar mtoto akiwa katika hali
ileile. Baada ya hospitalini kushindikana, kwa mganga nako kushindikana,
tulihamia kwenye maombi. Ingawa niliogopa kuumbuka lakini nilikuwa
tayari kuonekana mchawi ilimradi tu mwanangu apone, tulizunguka makanisa
yote na kuita mpaka mashehe kuja kumsomea lakini wapi, hali ya Ritha
haikubadilika hata chembe.
******
Maiasha yaliendelea, nilifanikiwa
kujifungua mtoto wakiume mzima akiwa na hali nzuri kabisa. Mume wangu
aliendelea kunipenda na kuendelea kuhangaika kuhusu Ritha ambaye
tulimtafutia mtaalamu wa viungo ili kumfanyia mazoezi, nilijua
haitasaidia lakini sikua na namna. Mama yangu hakuridhika hivyo
aliendelea kuhangaika akitafuta waganga mbalimbali wa kumponya mjukuu
wake lakini nayo pia haikusaidia.
Sikumoja nakumbuka Mama alikuja
nyumbani, nilikuwa peke yangu na watoto tu, tukawa tunaongea kuhusu hali
ya Ritha na namna ya kumsaidia. Alikuwa amepata mganga mwingine
Sumbawanga na tulikuwa tunajadili namna ya kumshawishi mume wnagu
kumpeleka huko. Wakati tukiwa tunaongea maneno yetu sebuleni, sikujua
kuwa wifi yangu tuliyekuwa tunaishi naye alikuwa ndani, nilijua tayari
alishaondoka kwenda chuo kumbe alikuwa hajisikii vizuri na alikuwa
amelala ndani.
Nilistuka baada ya kusikia mtu
analia huko chumbani baada ya kusikia tuliyokuwa tukizungumza kwnai
tuliongea yote. Nilikimbia kuangalia lakini aliwahi kufunga mlango na
kila nilipogonga hakufungua, nilimsikia akionge ana simu akisema “Kaka
njoo nyumbani…kuna matatizo yametokea…” Kweli hata nusu saa haikuisha
mume wangu aliingia, hapo ndipo wifi alipotoka chumbani na kumwaga
mchele wote.
Kilikuwa ni kilio kitupu, nilipiga
magoti kuomba msamaha lakini Jose hata hakunisikiliza, kila
alipomuangalia mwenetu alikuwa akitokwa machozi kama mtoto mdogo.
“Ulikosa nini? Ulikosa nini…mpaka kufanya yote haya…? Aliniuliza Jose
huku bado akiendelea kububujikwa na machozi, sikuwa na jibu zaidi ya
kuendelea kulia kwani kusema kweli sikukosa chochote kwake.
Kutokujiamini na wivu wa kijinga
ndiyo kulisababisha yote hayo. Hakutaka hata kuniangalia, aliingia ndani
na bila kuchukua chochote alimchukua Ritha na kuondoka naye yeye na
mdogo wake. Sikujua wameenda wapi mpaka wiki moja baadaye aliporudi na
wazee na kufanya kikao, waliitwa viongozi wa dini ili kusuluhisha lakini
alisema yeye hayuko tayari tena kuendelea kuishi na mimi.
Alimchukua Ritha na kuondoka naye,
wakati huo Ben mtoto wangu mdogo wa mwisho alikuwa bado mdogo hivyo
alimuacha lakini alipotimiza mwaka mmoja alikuja kumchukua. Nilitamani
kupigania ili angalau nipate haki ya kuwalea wanangu lakini nilikosa
nguvu, kwa niliyokuwa nimefanya sijui ningeanzia wapi, pia Jose
alinitisha.
Aliniambia “Nakuachia kila kitu ila
siku nikisikia hata unawakaribia wanangu nakuchinja, sikuui nakuchinja
wewe na Mama yako…kaa mbali na familia yangu…!” Aliniambia hivyo wakati
akimchukua Ben. Ingawa niliachiwa kila kitu kwa maana ya nyumba na gari
lakini maisha yangu sasa hayana uelekeo,, bado nazidi kumuomba Mungu
anisamehe na kumponya mwanangu.
Ingawa sasa hivi Jose amelegeza
msimamo na anaruhusu niwaone watoto lakini bado hajanisamehe. Pamoja na
kumpeleka kwenye maombi karibu kila siku lakini bado Ritha yuko kwenye
hali ileile hajapata nafuu na amekuwa mlemavu wa kudumu. Kwangu mapenzi
siyatamani tena, kazi sina tena, nilifungua kabishara lakini hata
hakachanganyii kwani kila jirani ananiona mchawi, hakuna anayetaka
kununua kwangu.
Nimeamua kupangisha nyumba na
kuhamia mtaa mwinngine, nilitamani kuhama kabisa Dar na kuanza maisha
sehemu nyingine lakini itanifanya kuwa mbali na wanangu kwani sasa
angalau naruhusiwa kuwaona. Maisha yangu nikama yamesimama, sijui nini
chakufanya, sina hisia za mwanaume, kila mtu amenitenga hata ndugu zangu
wa damu nao hunisalimia kwa mashaka, yaani ni ile salamu tu basi hakuna
hata anayetaka kuwa karibu na mimi.
****MWISHO*****
Mapenzi ya dawa kweli yapo lakini
mwisho wake si mzuri, anaweza kukupenda na kukupa kila kitu lakini siku
dawa ikiisha au ukapata mwenye ujuzi zaidi basi ndiyo mwisho wako.
Kutumia waganga ni kutokujiamini tu, wapo watu wanaopendwa kwa dhati,
wenye wapenzi wakujitoa lakini kwakuwa walianza kwa kutumia waganga bado
hawaamini kuwa wanapendwa na kudhani nguvu ya dawa ndiyo iliyowavuta
wapenzi wao.
Ubaya wakutumia dawa nikuwa hata
upendwe vipi, hata akuonyeshe mapenzi kiasi gani bado utaendelea kujiona
kama takataka, mtu asiyependwa hivyo kujikuta unaabudu waganga. Kama
Mungu amekupa mpenzi bila kutumia dawa nikwanini uhangaike na dawa
kumuweka kwako. Kwanini uwe mtumwa wa waganga wa kienyeji. Haijalishi
una umri gani wewe jua kuwa Mungu ana mtu wako kakuandalia, huna haja ya
kumshirikisha shetani.
No comments:
Post a Comment