WANAWAKE wakiwapenda wanaume hubaki na mateso mioyoni mwao. Hii ni kwa
sababu ni vigumu kumtokea mwanaume moja kwa moja kumwaga sera kuwa
unataka ‘akung’oe’.
Ni kweli kwamba, hata kama mwanaume akimkubali mwanamke awe mpenzi wake
baada ya kutokewa, imani yake huwa hafifu kuhusu penzi la kweli la
mwanamke huyo. Anaweza kumtumia kwa siku kadhaa kisha akamwacha. Huo
ndiyo ukweli.
Wanawake waliowahi kuwatokea wanaume wanaweza kuwa na ushahidi mzuri
zaidi juu ya hilo. Pamoja na hayo yote, bado mwanamke anabaki kuwa
binadamu, mwenye hisia za upendo na kutamani baadhi ya vitu.
Anaweza kumpenda mwanaume na ni haki yake ya msingi kabisa. Kuwa katika
uhusiano na mtu unayempenda kwa dhati ni jambo zuri. Moyo huridhia na
kuwa huru katika uhusiano huo.
Hapa katika Let’s Talk About Love tunakupa dondoo zitakazokusaidia
kumsogeza mwanaume ambaye ameuteka moyo wako na hatimaye kuwa wako moja
kwa moja. Katika vipengele vilivyotangulia nilieleza kuwa, kwanza
mwanamke ni vyema ajitunze na aweke mwonekano wake wenye kuvutia muda
wote halafu pia nikaeleza kuhusu kumvutia mwanaume kwa mambo mbalimbali
hasa mavazi na mambo anayopendelea. Sasa tunaweza kuendelea.
ASIWE KWENYE UHUSIANO
Jambo lingine la kuzingatia kwa mwanaume huyo wakati wa harakati za
kumweka mikononi mwako ni kuhakikisha hayupo kwenye uhusiano na mtu
mwingine. Kuna baadhi ya wanawake wapo tayari kuwa na mwanaume hata kama
yupo na mpenzi mwingine; hilo ni kosa na naweza kusema ni umasikini wa
kufikiri.
Kama kweli umempenda, itakuwa na maana kama utaweka makazi ya moyo wako kwake milele na siyo kwa muda mfupi tu.
JISOGEZE ZAIDI
Tayari umeshakuwa na uhakika kuwa hana mtu, sasa unatakiwa kujisogeza
karibu yake. Jizoeshe kumsalimia mara kwa mara na kumsifia kuwa
amependeza.
Kamwe usioneshe dalili kwamba wewe ni ‘maharage ya Mbeya’, ishia kwenye
kujisogeza karibu yake kwa kumsifia na kufanya mambo mengine
yanayofanana na hayo na siyo zaidi ya hapo.
JENGA URAFIKI
Ukaribu wenu sasa unaweza kuwafanya marafiki wa karibu. Kama uko naye
ofisi moja au mnaishi mtaa/nyumba moja ni rahisi zaidi. Kuwa rafiki yake
wa kweli mwenye kujadiliana naye mambo ya msingi.
Katika urafiki wenu, kamwe usiwe mzungumzaji sana (hasa wa mambo
yasiyofaa), aidha usipende kukaa naye katika mazingira yenye vificho
ambayo yataweza kusababisha kuingia kwenye mtego mbaya.
ZUNGUMZIA ZAIDI MAISHA
Kuzungumzia zaidi maisha na kumshauri juu ya mambo muhimu ya maisha,
kutamfanya akuone wewe ni mwanamke makini mwenye malengo mazuri katika
maisha yako. Wanaume wanapenda sana wanawake ambao vichwa vyao vinafanya
kazi sawasawa.
Hii inaweza kuwa sababu itakayomfanya atamani kuwa karibu yako zaidi, jambo ambalo ndiyo shabaha ya moyo wako.
HAKUNA YEYE BILA WEWE
Kwa sababu tayari ni marafiki na mnashirikiana baadhi ya mambo,
tengeneza mazingira ya kuwa naye karibu zaidi. Mshirikishe kwenye mambo
yako, mfanye ajione si mkamilifu bila kuwa na wewe karibu.
Hili litawezekana kwa kuishika siku yake, kumtakia siku njema na
kumjulia hali yake kazini na maendeleo yake kwa ujumla. Kwa kuwa ni
marafiki, kwa ndani lazima hisia za mapenzi zitaibuka juu yako na
utamuweka kwenye nafasi ya kufikiri kuanzisha uhusiano na wewe.
NI WAKO TU!
Ukipitia hatua zote, bila shaka mwanaume huyo ni wako tu. Ikiwa pamoja
na vyote hivyo bado haonyeshi dalili au hajafunguka kuwa unamhitaji,
basi mwache, siyo riziki yako. Kwa nini ung’ang’anie usipopendwa?
No comments:
Post a Comment